HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 4, 2022

WANAHABARI WATAKIWA KUWEKA KIPAUMBELE KUELIMISHA JAMII MAGONJWA YA MLIPUKO

 

Na.Faustine  Gimu ,Dodoma.

Waandishi wa  Habari wametakiwa kuweka kipaumbele kuandika habari za kuelimisha jamii namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo  UVIKO-19 pamoja na kuhamasisha umuhimu wa chanjo.

Wito huo umetolewa leo Novemba 4.2022 jijini Dodoma na  Afisa afya jiji la Dodoma Thobias Kigwinya wakati akitoa mafunzo ya kuwajengea uelewa wanahabari Mkoa wa Dodoma  namna ya kuripoti habari zinazohusu magonjwa ya mlipuko ikiwemo Uviko-19 yaliyoandaliwa na Taasisi ya Habari ya Internews.

Afisa afya huyo amesema wanahabari wana mchango mkubwa katika katika kuelimisha jamii katika uhamasishaji wa kujikinga na magonjwa  ya mlipuko na umuhimu wa utumiaji wa chanjo  hivyo ni wajibu kwa kila mwanahabari kuandika habari zenye usahihi na zisizokuwa na mkanganyiko kwa jamii juu ya magonjwa ya mlipuko.

Hata hivyo Kigwinya ameendelea kuwahakikishia wanahabari kuendelea kushirikiana na wataalam  wa afya  katika kuelimisha  kuhamasisha jamii umuhimu wa chanjo ya uviko-19 kwani ni salama na haina madhara yoyote.

“Chanjo ya Uviko-19 ni salama na haina madhara yoyote ,inapunguza madhara ya ugonjwa huo hivyo chanjo sio kitu cha kubeza wanahabari tusaidiane kutoa elimu sahihi kwa jamii”amesema.

Akizungumzia maadili  ya uandishi wa Habari  za magonjwa ya mlipuko ikiwemo Uviko-19  Mjumbe wa Bodi Umoja wa Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania[UTPC] Yusuph  Musa amesema  ni muhimu kuzingatia uadilifu,na usahihi wa taarifa pamoja na kuzingatia usiri wa taarifa.

“Unakuta watu hawana uelewa kuhusu chanjo unaandika kichwa cha habari wananchi wagomea chanjo badala ya kuandika wananchi wahitaji uelewa kuhusu chanjo hivyo ni muhimu sana kuzingatia maadili ya uandishi “amesisitiza.

Nao baadhi ya waandishi wa Habari wahamasishaji wa chanjo ya Uviko-19 mkoa wa Dodoma akiwemo Bilson Vedastus  pamoja na Bahati Msanjila wamesema ni muhimu kutumia vyanzo vya kuaminika  na kuzingatia uzalendo kuhusu habari za chanjo na magonjwa ya mlipuko.

“Katika suala la uandishi unapoandika habari za Uviko-19 na magonjwa ya mlipuko  jitahidi sana kuangalia vyanzo vya kuaminika  mfano tovuti ya wizara ya Afya ,pia ni muhimu kuangalia mambo kwa kina ,uzalendo,habari isilete taharuki na kuangalia vyanzo vingine vya taarifa vinavyoaminika”amesema Bilson.

“Ni muhimu kuepuka lugha za kuogofya  na kuzingatia maudhui  na panahitaji kuwepo kwa mjadala  kuwajengea uelewa wananchi “amesema Msanjila.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad