HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 4, 2022

RC KINDAMBA ATANGAZA VITA NA WANAOHUJUMU MBOLEA YA RUZUKU, NANE WADAKWA WAKISAFIRISHA MBOLEA KWENDA MALAWI KINYUME NA SHERIA

 



BAADA ya kukamatwa kwa malori (Fusso) mawili yakiwa na mifuko 403 ya mbolea ya kukuzia aina ya UREA inayodaiwa kuwa ni ya ruzuku, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Waziri Kindamba amejitokeza na kusema wamekamata watu nane wanaodaiwa kuunda mtandao wa kuhujumu jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwapunguzia makali wakulima kupitia mbolea ya ruzuku.

Amesema, wote wanaohusika na usafirishaji haramu wa mbolea wilayani Ileje hawapo salama, iwe ni dereva aliyebeba, mmiliki wa gari, wakala wa mbolea za ruzuku, kampuni la uingizaji wa mbolea nchini, afisa kilimo kama naye amehisika wote waliohusika wataingia kwenye msukosuko.

Waziri Kindamba ametoa kauli hiyo leo tarehe 4 Novemba, 2022 akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara wilayani Ileje akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, pamoja na viongozi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA) kwa lengo la kujionea shehena hiyo ya mbolea iliyokamatwa ambapo Mkuu wa Mkoa alitumia fursa hiyo kuwaonya wafanyabiasha.

Kindamba amesema mfanyabiashara yeyote aliyeamua kufanyabiashara haramu ya kuihujumu serikali, ikiwemo kujiingiza kwenye biashara ya kusafirisha mbolea ya ruzuku kwenda kuuza nje ya nchi ajieandae kufirisika.

“Naomba niwaambie tuu kuwa hakuna siku ambayo serikali imefumba macho na njia ya mkato haijawahi kuwa njema, hivyo wale wote walioamua kuihujumu serikali , wakiwemo wafanyabiashara wajiandae kufirisika” alisisitiza Kindamba.

"Nimekuwa nikisema maneno haya lakini watu wanayachukulia mzaha, kwenye sako la nyani na ngedere haponi, yeyote atakayehusika na biashara ya mbolea za ruzuku akaenda akatia kidole basi jua umepotea" Mkuu wa Mkoa Kindamba alisisitiza.

Mkuu wa Mkoa kindamba alieleza kuwa mzigo umekamatwa katika kijiji na Kata ya Chitete kwenye njia zisizorasmi ukitoroshwa kwenda nchi jirani ya Malawi ambapo gari moja lilipotelea kusikojulikana na ufuatiliaji kubaini lilipo unaendelea.

Akizungumzia gari iliyofanikiwa kukimbia ikiwa na shehena nyingine ya mbolea, Kindamba amesema kuwa kutokana na ushirikiano unaotolewa na waliokamatwa wao pia watakamatwa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kinyume nao.

Amesema, mzigo huu ulikamatwa tarehe 2 Novemba, 2022 saa 11 Alfajiri na kubainisha oparesheni ipo na itaendelea kwa masaa 24 siku saba za wiki hivyo hakuna namna wabadhirifu watakwepa mkono wa sheria.

Akizungumzia taarifa za uhamiaji kwa waliokamatwa wakitorosha mbolea, amesema taarifa zao za uhamiaji zina mashaka kwani hawakupita kwenye mipaka rasmi hivyo vyote vilivyofanyika katika kusafirisha mbolea hiyo ni haramu, na hakuna uhalali hata kidogo kwa watoroshaji hao.

Aidha, Kindamba ametoa wito kwa watanzania wote kutoa taarifa pindi wanapobaini vitendo vya wizi wa mbolea za ruzuku kufanyika ili juhudi za Rais Samia kuwakomboa wakulima zisipotee bure.

Amesema, hawa wanaohujumu mbolea za ruzuku wanatuibia sote hapa wanahujumu wananchi wa tanzania, wanahujumu watu wa songwe hivyo ukibaini kuna namna yoyote ya ubadhirifu kwenye mbolea za ruzuku taarifa itolewe na kueleza kuwa jambo hili lapaswa kufanywa kwa ushirika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt, Stephan Ngailo amesema mbolea iliyokamatwa ni ya ruzuku kwa kuwa kuanzia Agosti 8 mwaka huu mbolea yote iliyopo nchini inauzwa kwa mfumo wa ruzuku.

Dkt. Ngailo ameongeza kuwa Tanzania ni lango linalotumiwa na nchi jirani kufikisha mbolea kwenye nchi zao hivyo ili uweze kusafirisha mbolea kwenye nchi hizo lazima ufuate taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia tasnia ya mbolea na kufanya kinyume cha hapo hatua kali zitachukuliwa dhidi yako.

Magari yaliyokamatwa na yako mikononi mwa vyombo vya ulinzi ni gari lenye namba T .463 CNN aina ya Fusso iliyokuwa imebeba mifuko 201.

Gari nyingine ni lenye namba T.202 DGU aina ya Fusso iliyokuwa imebeba mifuko 202, pamoja na pikipiki yenye namba MC 885 DFC ililyotumika Kwa ajili ya kufanya doria ili kufanikisha kupitisha mbolea hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Waziri Kindamba (wa pili kutoka kulia) akizungumza na wanahabari walioshiriki mkutano baina yake, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (wa kwanza kulia)na watendaji wa mamlaka katika eneo yalikohifadhiwa magari yaliyokamatwa yakiwa na shehena ya mbolea iliyokuwa ikitoroshwa nje ya nchi kinyume na taratibu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (mwenye kofia) akizungumza na wanahabari walioshiriki kikao na Mkuu wa Mkoa wa Songwe na Kamati ya Ulinzi na Usalama juu ya Hatma ya magari yaliyokamatwa yakiwa na shehena za mbolea yakisafirishwa nje ya nchi kinyume cha taratibu leo tarehe 4 Novemba, 2022

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Waziri Waziri Kindamba akiwa katika picha na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo (kulia) na Mwanasheria wa TFRA, Geofrey Munisi (kushoto) mara baada ya kuwasili ofisini kwa mkuu wa Mkoa, Songwe tayari kwenda kujionea shehena ya mbolea iliyokamatwa ikitoroshwa nje ya nchi na kuhifadhiwa kwenye kituo cha polisi cha Ileje Mkoani Songwe

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad