HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 15, 2022

WALIMU WAKUU 17,000 KUPATIWA MAFUNZO YA UONGOZI NA USIMAMIZI WA SHULE-ADEM.

   Na Janeth Raphael MichuziTv - Dodoma 

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM imesema Imejipanga kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu wapatao 17,000, kutoa mafunzo ya utawala Bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt.Siston Mgullah, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023 ,mbele ya waandishi wa habari leo Novemba 15,2022 Jijini Dodoma.

Dkt.Mgullah amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha wa 2022-2023 wakala hiyo imejipanga kudahili Walimu 2343 katika Kozi za CELMA, DEMA na DSQA, kuandaa Kiongozi cha Mwalimu Mkuu na kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.

"Wakala umedahili Walimu 1,839 katika mafunzo ya Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA) na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) ili kuwapa ujuzi na maarifa walimu katika usimamizi, ufuatiliaji na tathimini katika elimu,"Amesema Dkt.Mgullah

Na kuongeza kuwa "Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani, kwa Maafisa 3,860 (REOs, RAOs, DEOs, WEOs) ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wenye kuleta tija katika elimu,"Amesema Dkt.Mgullah

Mtendaji huyo amesema kuwa Wakala hiyo imetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani kwa walimu 7,612 ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji katika shule wanazosimamia.

Dkt.Mgullah ameongeza kuwa Wakala pia umeendesha mafunzo ya muda mfupi kwa Walimu Wakuu na Waratibu wa Taaluma 147 kutoka katika Shule za Msingi na Sekondari Zanzibar, chini ya mradi wa Mwanamke Initiative Foundation (MIF).

Pia ,Wakala umeendesha mafunzo ya Kamati za Shule kwa Washiriki 126 katika Mkoa wa Songwe ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika Shule na umeandaa mtaala wa shahada ya menejimenti ya uthibiti ubora wa elimu ili kuimarisha usimamizi na utoaji wa elimu bora katika ngazi zote za elimu.

"Tumefanya Tafiti sita na tumuwasilisha kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kubaini mapungufu na kuandaa mafunzo wezeshi kwa wahusika,

Na kuongeza kuwa " Tumeandaa Moduli 3 katika eneo la Uongozi na Usimamizi wa Shule ili kuendesha mafunzo ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa ujenzi wa umahiri kwa walimu wa Shule za Sekondari Zanzibar na umeandika vitabu vya kujenga umahiri katika utekelezaji wa Mtaala wa Sekondari ili kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza kwa ajili ya Shule za Zanzibar,"Amesema Dkt.Mgullah.

Dkt.Mgullah amesema kuwa moja kati ya malengo ya Wakala hiyo ni kuimarisha usimamizi wa utoaji wa elimu bora shuleni kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo ya elimu, kuziba ombwe la maarifa na ujuzi ambalo kiongozi au mtendaji hakupata katika mafunzo ya awali ya Ualimu na kuongeza idadi ya viongozi wenye maarifa ya uongozi na usimamizi wa elimu.

"Katika kipindi cha mwaka 2020/2021, Wakala umefanya tafiti mbalimbali zikiwemo za tathimini ya matokeo ya Mafunzo ya KKK kwa Walimu wa Darasa la III na IV yaliyofanyika Tanzania Bara, utekelezaji wa uthibiti ubora wa shule na utoaji wa mrejesho kwa walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika shule za Msingi,"Dkt.Mgullah

Pia Mtendaji huyo amesema kuwa wanafuatilia utendaji kazi wa Wakuu wa Shule waliopata mafunzo ya Uongozi na Utawala katika Elimu, wanafuatilia matokeo ya mafunzo ya Stashahada ya uongozi na usimamizi wa Elimu na tathmini ya athari za kozi ya Astashahda ya Uongozi, Usimamizi na Utawala wa elimu iliyofanyika katika mikoa minne.

Kwa Upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa amesema kuwa Serikali imeweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchi nzima ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8. Chuo hiki ni moja ya juhudi za Serikali za kusimamia ubora wa elimu.

"Fedha hizi ni nyingi ambazo zinahitaji usimamizi wa karibu, hivyo wale viongozi wa kwenye taasisi zinazosimamia elimu lazima wawe na ujuzi na mbinu nzuri za kusimamia maendeleo ya elimu ili tuweze kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali," Amesema Msigwa

Msigwa amesema Viongozi wanaosimamia Taasisi za Elimu wanatakiwa wakasome katika chuo hiki ili wakapate ujuzi wakasimamie vizuri taasisi hizo.

Pia Msigwa ametoa wito kwa waajiri kutosita kuwaruhusu viongozi wa taasisi za elimu kwenda kusoma ADEM.

Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM ulianzishwa Agosti 31, 2001 ukiwa na majukumu ya kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu kwa viongozi na watendaji mbalimbali wa elimu katika ngazi zote na kutoa ushauri wa kitaalamu katika mambo yanayohusu uongozi na usimamizi wa elimu.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM, Dkt.Siston Mgullah, akizungumza wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023 ,mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Novemba 15, 2022 Jijini Dodoma.
Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo Gerson Msigwa,akizungumza leo Novemba 15,2022 Jijini Dodoma Mara baada ya Wasilisho la Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM, Dkt.Siston Mgullah, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023 ,mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani).
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM, Dkt.Siston Mgullah (hayupo pichani), wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023 ,leo Novemba 15,2022 Jijini Dodoma.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad