UWANJA WA NDEGE WA BUKOBA NI SALAMA KWA MATUMIZI YA USAFIRI WA ANGA - TCAA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 9, 2022

UWANJA WA NDEGE WA BUKOBA NI SALAMA KWA MATUMIZI YA USAFIRI WA ANGA - TCAA

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) imewatoa hofu watumiaji wa usafiri wa Anga nchini kuhusu usalama katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba uliopo katika Manispaa ya Mji Bukoba Mkoani Kagera baada ya kutokea kwa ajali ya Ndege ya Precision Air ATR 42-500 yenye namba PW 494 iliyoanguka kwenye ziwa Victoria mita chache kutoka uwanja wa ndege wa Bukoba, ikijiandaa kutua siku ya Jumapili Novemba 06, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA), Hamza S.Johari amewaomba watanzania na hasa watumiaji wa Usafiri wa Anga kuwa watulivu kwa kuwa uwanja wa ndege wa Bukoba ni salama kwa matumizi ya Usafiri wa Anga na kuomba wanaotoa taarifa potofu kuwaachia wataalamu wa uchunguzi wa ajali za ndege kuendelea na uchunguzi wa ajali iliyotokea.

Amesema kwenye Sekta ya Usafiri wa Anga ajali hii sasa ni sehemu ya kujifunza, ili kupitia kwa haya yaliyotokea na kujiwekea mikakati jambo la namna hii lisiweze kutokea tena katika usafiri wa anga huko mbeleni kwani usafiri wa anga ndio usafiri salama Duniani.

Pia amesema kitaalam inapotokea viwanja vya ndege upande mwingine kuwa karibu na maji, viwanja vya namna hiyo vina faida kwasababu kwenye maji kuna vikwazo vichache sana na hata ndege ikianguka kwenye maji madhara yake yanakuwa madogo ukilinganisha na nchi kavu ambapo zinaweza kupelekea moto.

Amesema uwanja wa ndege wa Bukoba una urefu wa kilometa 1.5 na uwanja huo unauwezo wa kuhudumia ndege zenye uzito mpaka wa tani 29. Na kuongeza kuwa ndege ya Precision Air ATR 42-500 yenye namba PW 494 iliyopata ajali ilikuwa na uzito wa tani 18.5.

Mkurugenzi Johari ameongeza kuwa ndege hiyo kwa aina yake ili iweze kutua inahitaji urefu wa mita 900 na wakati wa kupaa inahitaji urefu wa kilometa 1.1, hivyo kutakana na vigezo hivyo uwanja wa ndege wa Bukoba unakidhi vigezo hivyo .

Ametoa angalizo kwamba, kusambaza taarifa mbalimbali za ajali bila utaratibu uliowekwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga Duniani ni kosa na tunaweza kuiweka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoridhia na kusaini mkataba wa Chicago katika maangaiko yasiyokuwa ya msingi, hivyo ni vizuri kutulia na kuwaacha wataalamu wakafanya kazi yao vizuri na bila kuingiliwa.

Ametoa mfano kwamba , jana kuna mtu katengeneza video yake ya uongo ikionesha ndege ilivyokuwa inakwenda pale mpaka inadondoka ndani ya maji na ameweka nembo ya Shirika la Ndege la Precision Air, kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na hali hii imeongeza taharuki kwa watumiaji wa usafiri wa anga pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kuamini kuwa kile kilichotengenezwa kimetolewa na mamlaka husika na wengine wanajiuliza hii imetoka kwenye rada za TCAA.

Mkurugenzi Hamza ameongeza kuwa Jumuiya za huko nje zinashangaa kuna kitu gani kimetusibu maana bado tuna msiba huku baadhi ya watu hawatulii nchi hii wakawaacha wataalam wakafanya kazi zao kitaalam na kuja na majibu mazuri ili kuutangazia umma kuhusu sababu kubwa iliyopelekea ndege kudondoka kwenye maji.

Ametoa shukrani kwa wadau wote wakiwemo wavuvi, Sekta Binafsi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege(TAA) kwa kuweza kusimama kidete kuhakikisha watu kwenye ndege wanatoka salama.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA), Hamza S.Johari akizungumza na waaandishi wa habari kuhusu hali ya usalama wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba baada ya kutokea kwa ajali ya ajali ya Ndege ya Precision Air ATR 42-500 yenye namba PW 494 iliyoanguka kwenye ziwa Victoria mita chache kutoka uwanja wa ndege wa Bukoba, ikijiandaa kutua siku ya Jumapili Novemba 06, 2022.
Baadhi ya maofisa kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Mkuu  wa TCAA, Hamza S.Johari alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya usalama wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Rubani wa Ndege Kapteni Noel Komba akizungumza kuhusu uwanja uwanja wa ndege wa Bukoba wakati wa mkutano wa  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA), Hamza S.Johari alipokuwa anazungumza na waaandishi wa habari kuhusu hali ya usalama wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba baada ya kutokea kwa ajali ya ajali ya Ndege ya Precision Air ATR 42-500 yenye namba PW 494.
Mkutano ukiendelea 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad