HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 9, 2022

USIYOYAJUA KUHUSU MTO RUVUMA

 
Na Albano Midelo

MTO Ruvuma ni miongoni mwa vivutio vitano vya utalii vinavyoubeba Mkoa wa Ruvuma.Vivutio vingine ni ziwa Nyasa,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,ushoroba wa Selous-Niassa,Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na utalii wa kiutamaduni na kihistoria.

Mratibu wa Utalii Kanda ya Kusini Deborah Mwakanosya anasema Mto Ruvuma umeubeba Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa umepita katika wilaya zote tano ambazo ni Songea,Mbinga,Nyasa,Namtumbo na Tunduru.

Mwakanosya anasema Mto Ruvuma ndiyo Mto mrefu kuliko yote katika nchi za Afrika Mashariki na miongoni mwa mito maarufu barani Afrika ukiwa umeanzia kwenye misitu ya milima ya Matogoro Manispaa ya Songea na kumwaga maji yake Bahari ya Hindi.

“Mto Ruvuma umedhihirisha maajabu ya Mungu ambayo hayawezi kusimuliwa katika mikoa mingine nchini,ispokuwa Mkoa wa Ruvuma,katika milima ya Matogoro Manispaa ya Songea tunakutana na chanzo cha mto Ruvuma,ukiona chanzo hicho,ni mfano wa kisima kidogo sana ambacho kimetoa mfereji mdogo,lakini kazi yake huko mbele huwezi kuongelea katika hali ya kawaida na kueleweka kwa jamii’’,anasisitiza Mwakanosya.

Anasema kisima hicho kidogo chenye mfereji mdogo kwenye milima ya Matogoro kipo meta 1500 toka usawa wa bahari kimekwenda kuunda mto maarufu duniani unaoitwa Ruvuma ukiwa na urefu za kilometa zaidi ya 800 na upana wa kati ya meta 300 hadi 500 kutegemea na eneo lililopo kwa sababu kuna baadhi ya maeneo mto huo una upana mkubwa zaidi.

Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo,Mto Ruvuma  umebeba fukwe mbalimbali zinazovutia wageni wengi ambapo anazitaja fukwe nyingi za kuvutia zinapatikana kwa wingi katika hifadhi ya Taifa ya mazingira asilia ya Mwambesi iliyopo wilayani Tunduru.

Anasema katika hifadhi hiyo ,Mto Ruvuma umetengeneza visiwa na fukwe nzuri za kuvutia ambazo zinamwezesha mtalii kuogelea na kuona wanyama wengi ambao wapo katika hifadhi hiyo kando kando ya Mto Ruvuma wakiwemo tembo,mamba,simba,jamii ya swala na samaki wa aina mbalimbali.

Hata hivyo Mratibu huyo wa Utalii Kanda ya Kusini anasema ili mto huo uweze kufika katika Bahari ya Hindi na kumwaga maji yake,unaanzia wilaya ya Songea milima ya Matogoro,unapita katika shamba maarufu la AVIV ambalo wanaendesha kilimo cha umwagiliaji wa zao la kahawa kupitia mto Ruvuma ambapo wameajiriwa watumishi zaidi ya 3000.

Kutokea hapo mto huo umepita hadi katika eneo la Tulila wilayani Mbinga ambako Shirika la watawa wa katoliki wa mtakatifu Agnes wameweka mradi mkubwa wa umeme wa maji kwenye maporomoko ya Mto Ruvuma Chanzo hicho kinamilikiwa na watawa wabenediktine wa Mtakatifu Agnes Chipole Jimbo Kuu Katoliki la Songea.

Akizungumza kwa niaba ya Mama Mkuu wa Shirika hilo,Sr.Richards Chiwinga(OSB) anasema wana mashine mbili ambazo zina uwezo wa kuzalisha megawatts tano.

Analitaja bwawa la Tulila kuwa lina ukubwa wa meta za ujazo milioni 1.14,likiwa na urefu wa meta 750 toka usawa wa bahari na usawa wa maji(level) ni meta 748 na kwamba maji yakizidi kiwango hicho yanamwagika.

Maporomoko ya Mto Ruvuma katika eneo la Tulila yana  mandhari nzuri ya kuvutia unaweza kufanya utalii wa kupiga picha, kuogelea, kuendesha mtumbwi, pia kuna fukwe nzuri kutoka katika mto Ruvuma ambao ni miongoni mwa mito maarufu barani Afrika ambao unamwaga maji yake Bahari ya Hindi.


Mto Ruvuma katika Wilaya ya Nyasa umepita kwenye Pori la Akiba la Liparamba ambako katika eneo la Nakatuta kuna maporomoko mazuri ya maji ya mto Ruvuma ambayo yanavutia wageni wengi pia katika eneo hilo mtalii anaweza kufanya utalii wa kuvua samaki na kupanda kwenye tabaka la jiwe kando kando ya Mto Ruvuma..

Safari ya mto Ruvuma kutoka Liparamba imeendelea hadi eneo la Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambako kumejengwa daraja kubwa lenye urefu wa meta 98 linalogawa Tanzania na Msumbuji kupitia Mto Ruvuma.

Mwakanosya anabainisha zaidi kuwa Mto Ruvuma umeendelea hadi katika wilaya ya Namtumbo kwenye Jumuiya za uhifadhi wanyamapori vijijini ambazo ni Kimbanda,Kisungule na Chingoli na kwamba Mto Ruvuma unaendelea hadi katika msitu wa Hifadhi ya mazingira asilia Mwambesi wilayani Tunduru.

“Mto Ruvuma katika hifadhi ya Mwambesi kuna vivutio vya aina zote ikiwemo michezo ya kuendesha mitumbwi ambayo kwa mara ya kwanza Tanzania mchezo wa kuendesha mitumbwi ulizinduliwa mwaka 2019 katika eneo la Wenje Mto Ruvuma na watalii 22 ambao walitoka nchi 16 duniani  walishiriki’’,anasisitiza Mwakanosya.

Mratibu wa Utalii Kanda ya Kusini anabainisha zaidi kuwa maji ya Mto Ruvuma yalitumika katika  Vita ya Majimaji iliyopiganwa mikoa ya kusini kuanzia mwaka 1905 hadi 1907.

“Katika Mto Ruvuma eneo la Mwambesi kuna maporomoko ya Sunda ambako anahifadhiwa ndege mdogo zaidi duniani anaitwa pantiole ambaye anakula Samaki akiwa hai hivyo anaogelea kwenye maporomoko hayo kujipatia  Samaki ambaye anakula akiwa hai ’’,anasisitiza.

Anabainisha zaidi kuwa maporomoko ya Sunda  katika Mto Ruvuma ndiyo eneo pekee ambalo lilitumika kama darubini ya watu waliokuwa wanapigana vita ya porini iliyoitwa Golira war ambapo eneo kubwa la vita hiyo lilikuwa ni nchi Jirani ya Msumbiji.

Mwakakanosya anasema wananchi walipokuwa wanatoroka   kwenye vita hiyo walitumia Mto Ruvuma kuvuka ili kupata pumziko hivyo Mto Ruvuma ulitumika kwa ajili ya kuleta amani ya nchi Jirani ya Msumbiji.

 Tanzania ilikuwa ni kitovu cha kupigania uhuru wa nchi zilizo kusini mwa Afrika zikiwemo Msumbiji hivyo kupitia Mto Ruvuma imekuwa sio tu kivutio bali pia Mto huo umeleta heshima kwa nchi Jirani ya Msumbiji.

Mto huo ukishapita katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma unaendelea na safari yake hadi katika daraja la Umoja wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara na kuendelea hadi mkoani Mtwara.

Mwamba Lihami  ni Afisa  Mahusiano katika Kituo cha Uhamiaji Mtambaswala wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara ambako limejengwa daraja la Umoja katika Mto Ruvuma lenye urefu wa zaidi ya meta 700 likiunganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji.

Lihami anasema katikati ya daraja la Umoja ndiyo mpaka wa Tanzania na Msumbiji  ambapo amesema mita 900 kutoka darajani ndiyo makutano ya mito mikubwa miwili ambapo kulia ni Mto Ruvuma ambao unaanzia milima ya Matogoro Songea na kushoto ni Mto Rujenda ambao umeanzia kwenye ziwa Kihuta nchini Msumbiji,

Anasema mito hiyo miwili inapokutana inaonesha kitendo adimu cha mito hiyo kukutana hivyo eneo hilo linaweza kutumika kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya Jiografia wanaweza kuona uhalisia na kujifunza kwa urahisi makutano ya Mto Ruv

uma na Rujenda.

Analitaja jambo lingine ambalo mtu anaweza kujifunza katika eneo hilo ni muonekano wa majimbo mawili ya nchini Msumbiji likiwemo jimbo Niassa na Delgado hivyo Mto Rujenda kutoka nchini Msumbiji unakuwa ni mpaka wa majimbo hayo mawili ambapo Tanzania na Msumbiji mpaka ni Mto Ruvuma.

Anasema eneo linaloonekana katika jimbo la Niassa kupitia Mto Ruvuma ni Hifadhi kubwa ya Wanyama nchini Msumbiji inayoitwa Hifadhi ya Taifa ya Niassa na kwamba  nchi ya Msumbiji ina jumla ya hifadhi za Taifa 11 kati ya hizo hifadhi ya Niassa ni ya pili kwa ukubwa  ikitanguliwa na Hifadhi ya Limpopo.

“Baada ya udhibiti wa majangili na wawindaji haramu nchini Msumbiji na Tanzania ,hivi sasa Wanyama wanazaliana kwa wingi kwenye hifadhi ya Niassa na Tanzania pia inanufaika kwenye hifadhi zinazopakana na hifadhi ya Niassa ambazo ni Lumesule,Mwambesi na  ushoroba wa Selous-Niassa ambapo Wanyama wamezaliana kwa wingi hasa tembo’’,anasema Lihami.

Anakitaja Kijiji cha Negomano nchini Msumbiji ambacho kinapakana na Mto Ruvuma kupitia daraja la Umoja  ambapo neno  Negomano kwa kireno lina maana makutano ya mito miwili ya Ruvuma na Rujenda hivyo wakoloni wa Kireno waliamua kuweka ngome yao katika eneo la Negomano.

Anasema ndani ya  Mto Ruvuma katika eneo la Daraja la Umoja wapo Wanyama wengi wa majini kama viboko na mamba na kwamba Wanyama katika eneo hilo wanaonekana kirahisi na kwamba Mto Ruvuma kutoka eneo la Mtambaswala unaambaa kupitia Masasi hadi  eneo la Msimbati Mtwara hadi Bahari ya Hindi.

Hata hivyo anasema Mto Ruvuma kama ilivyo katika Mkoa wa Ruvuma una manufaa mengi katika Mkoa wa Mtwara ambapo katika Kijiji cha Masuguru  wilayani Nanyumbu  kunatarajia kuanzishwa mradi mkubwa wa maji ambayo chanzo chake ni Mto Ruvuma na kwamba mradi huo unatarajia kuwanufaisha wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu na vijiji vyake vyote.

Anasema katika wilaya ya Masasi pia wananchi wananufaika na Mto Ruvuma ambapo katika Kijiji cha Chipingo kuna mradi mkubwa wa maji ambao tayari unafanya kazi na wananchi wanafaidika na maji ya Mto Ruvuma.

Naye Devis Orio ni Mhifadhi ,Hifadhi za Bahari ya Ghuba ya Mnazi na Maingilio ya Mto Ruvuma anasema hifadhi hiyo ilianzishwa mwaka 2000 kwa tangazo la Serikali chini ya Sheria za Hifadhi za bahari na maeneo tengefu.

Anaitaja hifadhi hiyo kuwa ina eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 650 ambazo kati ya hizo kilometa 220 ni eneo la nchi kavu na zilizobaki ni eneo la bahari, anazitaja rasilimali zilizopo kwenye eneo la bahari ya Ghuba na maingilio ya Mto Ruvuma zipo nyingi zikiwemo zlilizopo baharini na nchi kavu.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali  Laban Thomas anasema Mkoa wa Ruvuma umejaliwa kuwa na vivutio vya utalii vya aina mbalimbali na kwamba Mto Ruvuma ni miongoni mwa vivutio hivyo ambavyo vinafaa kwa uhifadhi,utalii na uwekezaji.

Hata hivyo anavitaja vivutio vingine vinavyoupamba Mkoa wa Ruvuma kuwa ni ziwa Nyasa,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,hifadhi ya mazingira asilia Mwambesi na vivutio vingine vingi.

Mto Ruvuma unamwaga maji yake katika Bahari ya Hindi kwenye eneo Msimbati mkoani  Mtwara nchini Tanzania na Rasi ya Delgado nchini Msumbiji.

Mwandishi wa makala haya ni  Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini  Mkoa wa Ruvuma
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad