HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, November 30, 2022

TANZANIA YAPONGEZWA KWA HARAKATI ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA


MABALOZI  wa Umoja wa Ulaya (EU,) nchini wamezindua siku 16 za harakati za kupinga ukatili wa kijinsia sambamba na Nchi hizo kufanya warsha za Umma nchini kote kwa kufanya midahalo na kuwaleta wadau pamoja ikiwemo Serikali na kupaza sauti kwa watoa maamuzi ili waweze kushughulikia vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika makao ya ubalozi wa Ufaransa nchini kwa niaba ya mabalozi wa EU, Balozi wa Umoja wa Ulaya Manfredo Fanti amesema, nchini Tanzania EU kwa kushirikiana na wadau kutoka ndani na nje ya nchi wanatetea na kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanawake kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ya kitaifa ikiwa ni pamoja na kujenga uelewa wa kuzuia, kuripoti na kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kuwa na jamii salama zaidi.

Amesema, katika maadhimisho ya siku 16 za harakati za kupinga ukatili iliyoanza Novemba 25 na kuhitimishwa Desemba 10 mwaka huu kwa kauli mbiu ya ‘Chukua Hatua Kuzuia Mauaji ya Wanawake dhidi ya Wanawake’ itajenga uelewa zaidi juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utetezi wa kukomesha vitendo vya ukatili kwa wanawake na wasichana.

Pia ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kupambana dhidi ya vitendo hivyo hususani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuweka kipaumbele katika masuala ya kijinsia na kuunda Wizara maalumu inayoshughulikia masuala hayo.

Amesema katika maadhimisho hayo Balozi za Ubelgiji, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Uholanzi, Uhispania, Uswidi na ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, asasi za kiraia, watunga sera, vikundi vya kijamii na wanaharakati wanaendelea na hafla za Umma kote nchni ili kujenga uelewa na mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.

 Moja ya mambo yatakayoangaziwa kupitia midahalo, warsha na maandamano ya amani ya kupinga ukatili itafanyika katika mikoa 12 ya Tanzania na kushirikisha jinsia zote na kutoa tuzo kwa wapingaji wa ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa nchini Nabil Hajlaoui amesema ni jukumu la kila mmoja kulinda haki za wanawake na wasichana na kuhakikisha kunakuwa na usawa.

‘’Rais Samia alipoingia madarakani moja ya msisitizo aliouweka ni usawa wa kijinsia, Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha kunakuwa na kizazi cha usawa kimataifa kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa hapa Tanzania.’’ Amesema.

Amefafanua kuwa, ukatili wa wanawake ni moja ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu  ulimwenguni na Ufaransa itaendelea kusimama na Tanzania katika kusimamia haki za wanawake kupitia miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa ‘Girls Empowerment through Agriculture and Permaculture’  uliolenga kuwawezesha wanawake kupitia kilimo hai kupitia asasi za FCS Trust, Msichana Initiative, PPIZ na SAT.

Balozi Nabil amesema, Ufaransa chini ya mwavuli wa Umoja wa Ulaya wanatetea na kulinda haki za wanawake na wasichana ili kujenga kizazi chenye usawa kimataifa ‘Equality Generation Form.’

Akizungumza katika ufunguzi huo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili Serikali na wadau mbalimbali ikiwemo EU kupitia Balozi  wamejipanga katika maadhimisho hayo kwa kuhakikisha uelewa na nguvu ya kukomesha vitendo vya ukatili inaanzia kuanzia ngazi ya familia.

Amesema hali ya ukatili nchini bado ni changamoto takwimu zinaonesha kupungua kwa vitendo vya ukatili hususani kwa watoto bado ni ndogo kutokana na baadhi ya vitendo hivyo kumalizwa kindugu na  kutoripotiwa kwa matukio hayo ukilinganisha na mpango mkakati wa kupunguza vitendo hivyo kwa asilimia 50 iliiyowekwa kupitia mpango kazi wa kutokomeza vitendo ukatili kwa watoto na unyanyasaji wa kijinsia wa mwaka 2017/2018.

Amesema katika mwaka 2021 matukio ya unyanyasaji kwa watoto yalifikia 11,499 ukilinganisha na matukio zaidi ya kumi na tano elfu kwa mwaka 2022 huku asilimia 60 ya matukio hayo yakifanyika nyumbani waliko wazazi na ndugu, asilimia 40 yakifanyika shuleni au njiani.

‘’Mpango unaokuja sasa 2022/2026 umejikita katika kuimarisha kamati na kutumia mifumo ya kidigitali itakayowasadia wananchi kutoa taarifa kwa wakati pamoja na kushirikisha wanahabari watakaokuwa wanaripoti taarifa za kamati hizo na mifumo kufanya kazi.’’ Amesema.

Waziri Gwajima amesema, kuna mifumo mbalimbali ya misaada zikiwemo nyumba salama kwa manusura wa vitendo hivyo na Serikali kwa kushirikiana na wadau wanashirikiana ili kuongeza idadi ya hifadhi kwa manusura hao na hiyo ni pamoja na kuwepo kwa madawati ya jinsia katika vituo vya polisi na magereza, shule za Msingi na Sekondari na Vyuo Vikuu.

Kuhusiana na huduma ya Saikolojia Waziri Gwajima amesema, katika kupambana na janga la afya la akili wanaandaa sheria ya huduma ya ustawi wa jamii kwa wote wenye taaluma ya ustawi wa jamii ili huduma hizo za ustawi wa jamii ziiweze kupatikana kama huduma nyingine.

Amesema  mchango wa asasi za kiraia ni mkubwa sana katika masuala ya ukatili wa kijinsia ambao wamekuwa wakishirikiana na Serikali, wadau wa maendeleo na viongozi wa dini hasa katika wakati huu wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amelipa suala la jinsia kipaumbele kwa kuunda Wizara maalum.

Mabalozi wanachama wa EU walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Balozi wa Umoja wa Jumuiya ya Ulaya Manfredo Fanti, Balozi wa Ufaransa Nabil Hajlaoui, Balozi wa Ubelgiji Peter Hughebaert, Balozi wa Finland Theresa Zitting, Balozi wa Ujerumani Regine Hess, Balozi wa Ireland Mary O’Neill, Balozi wa Italia Marco Lombardi, Naibu Balozi wa Uholanzi Job Runhaar, Balozi wa Uhispania Fransisca Maria Pedros Carretero, mshauri kutoka Ubalozi wa Denmark Lena Hothes na Mkuu wa Kitengo cha Siasa, Biashara na Ukuzaji wa Sweden Joakim Ladeborn.

Kampeni ya Siku 16 za Uanaharakati iliyoanzishwa mwaka 1991 inasisitiza kwamba Ukatili dhidi ya Wanawake, kwa namna yoyote le ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza wakati wa mkutano huo na kuushukuru Umoja wa Ulaya (EU,) kupitia Balozi zake nchini ambao wamekuwa wakishiriki katika mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake na wasichana nchini.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Manifredo Fanti akifuatilia mawasilisho katika mkutano huo uliowakutanisha mabalozi wa EU na waandishi wa habari na kufanyika katika makao ya Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Ufaransa nchini Nabil Hajlaoui akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa Ufaransa itaendelea kusimama na Tanzania katika kusimamia haki za wanawake kupitia miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa ‘Girls Empowerment through Agriculture and Permaculture’  uliolenga kuwawezesha wanawake kupitia kilimo hai kupitia  asasi za FCS Trust, Msichana Initiative, PPIZ na SAT. 



 

 
 Matukio mbalimbali wakati wa mkutano huo.

 

 
 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad