Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANANCHI wa Kijiji cha Ngage Kata ya Loiborsoit Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamelalamikia utaratibu mbovu wa ugawaji wa mashamba uliofanywa na Mwenyekiti wa kijiji na wajumbe wa serikali ya kijiji hicho.
Kutokana na hali hiyo wananchi wa kijiji hicho walilalamikia ukiukwaji wa kanuni, taratibu na sheria kwenye ugawaji wa mashamba yao uliofanywa na viongozi hao ikaundwa kamati kupitia mkutano mkuu wa kijiji uliofanyika Januari 31 mwaka huu.
Diwani wa kata ya Loiborsoit, Siria Baraka Kiduya akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani amesema wananchi wa kijiji hicho wanalalamikia ukiukwaji mkubwa wa ugawaji wa mashamba hayo.
Kiduya amesema kamati hiyo iliundwa baada ya wananchi hao kutokuwa na imani na Mwenyekiti wao wa kijiji na wajumbe wao ambapo ilibainika maovu mengi.
Amesema ilibainika kuwa, kulikosekana kwa barua za maombi ya mashamba kwa watu wasio wakazi wa kjiji, kupewa mshamba kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18 na baadhi ya viongozi wa kijiji na watu wasio wakazi wa kijiji kujimilikisha ekari 30 wakati ilipaswa kugawiwa ekari mbili.
“Pia waligawa mashamba kwenye baadhi ya maeneo ya malisho, kugawa mashamba ndani ya mita 60 kutoka usawa wa ukingo wa mto na kukuta baadhi ya watu wanaoonekana kwenye stakabadhi kulipia mashamba ila kiuhalisia hawajawahi kulipia au kupewa mashamba,” amesema Kiduya.
Amesema mkutano mkuu wa pili wa kijiji ulifanyika Agosti 10 ambao ulipitisha majina ya watu 257 dhidi ya waombaji 2,000 na wananchi waliopata mashamba kwa awamu ya kwanza na yapili ni watu 487.
Amesema hata hivyo wanaishukuru serikali kwa kusimama kidete katika ufanikishaji wa ugawaji wa mashamba hayo.
"Tunamshukuru Mhe DC Dkt Suleiman Serera, Mwenyekiti wa Halmashauri Baraka Kanunga, Mbunge wa Jimbo Christopher Ole Sendeka, Mkurugenzi mtendaji Samwel Warioba, Afisa Ardhi Baltazari Sulle, Afisa Tarafa ya Ruvu Remit Edosi Ndikwiki Ofisa mtendaji wa kata Johari Kilyamhogo na Ofisa mtendaji wa Kijiji Susan Ngillah," amesema Kiduya.
Amesema kata ya Loiborsoit ina uhitaji mkubwa wa soko kwa sasa ili kurahisisha mahitaji kwa jamii na daraja ni changamoto kwa wakazi wa kata hiyo hivyo ni muhimu kujengwa ili kurahisisha huduma za kijamii na kuunganisha waanchi wa wilaya ya Simanjiro na wilaya ya Same.
“Pia tunaomba kituo cha afya kwenye kata ya Loiborsoit kutokana na ongezeko la wakazi kuwa kubwa na pia upatikanaji wa mbolea ya ruzuku kwenye kijiji cha Ngage na Loiborsoit B japokuwa namba za usajili zimepatikana,” amesema.
No comments:
Post a Comment