TANZANIA YANADI FURSA ZAKE ZA UWEKEZAJI NCHINI URENO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 21, 2022

TANZANIA YANADI FURSA ZAKE ZA UWEKEZAJI NCHINI URENO

  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya Uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ikiwa ni pamoja na kuzifanyia maboresho baadhi ya sheria za usimamizi wa biashara ili kuongeza ufanisi kwa sekta binafsi katika uzalishaji.

Mhe. Dkt. Stergomena ametoa kauli hiyo  jijini Lisbon wakati akifungua rasmi Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania  na Ureno lililoloandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Ureno na Taasisi ya Biashara na Uwekezaji ya Ureno na  kuishirikisha Jumuiya yaWafanyabiashara wa Ureno.

Mhe. Dkt. Tax amesema dhamira kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara hususan kwa kuishirikisha ipasavyo sekta binafsi. Amesema tayari Serikali imefanya majadiliano ya mara kwa mara na sekta biafsi ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Amesema katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini masuala mbalimbali yanaboreshwa zikiwemo huduma, sheria, miundombinu pamoja na kuishirikisha kikamilifu sekta binafsi ambayo ni muhimu katika kuchangia uchumi wa nchini.

“Tupo hapa leo ili kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Ureno hususan katika masuala ya biashara na uwekezaji. Tanzania inaendelea kuhamasisha uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji. Katika maboresho hayo ni pamoja na Serikali kushirikiana kwa karibu na  sekta binafsi ili kuiwezesha sekta hii kuwa na ufanisi na kuchangia uchumi ipasavyo” amesema Dkt. Tax.

Amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu kama barabara, bandari, reli, viwanja vya ndege na upatikanaji wa maji na umeme ili kuwawezesha wawekezaji kutopata changamoto zozote pale wanapokuja nchini kuwekeza.

 “Serikali imefanya jitihada za makusudi za kuhakikisha miundombinu yote ya msingi kama maji, umeme, barabara, reli, usafiri wa anga na mawasiliano ya simu vinapatikana kwa ngazi tofauti tofauti. Kupitia maboresho haya ni imani yetu  wawekezeji watapata ujasiri wa kuwekeza Tanzania na si mahali pengine popote”, amesisitiza Dkt. Tax.

Amesema masuala mengine yanayohamasisha uwekezaji, biashara na utalii nchini ni pamoja na ushiriki wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Filamu ya kutangaza Utalii nchini ya The Royal Tour, Sera ya Mambo ya Nje yenye msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi ambayo imekuwa chachu katika kuwajengea ujasiri wawekezaji nchini pamoja na ushiriki wa Tanzania kwenye majukwaa mbalimbali ya kimataifa ya biashara na uwekezaji kama Maonesho ya Biashara ya Dubai ya mwaka 2020. Vyote hivi  vimeipaisha zaidi Tanzania duniani na kuchangia ongezeko la watalii na wawekezaji nchini.

Dkt. Tax alitumia fursa hiyo pia kuwakaribisha wawekezaji na wananchi wa Ureno kwa ujumla kutembelea Tanzania ili kujionea vivutio mbalimbali vya utalii huku akiwahamasisha kuangalia Filamu ya Utalii ya Royal Tour ambayo ameilezea kuwa ni ya aina yake kwani mhusika mkuu katika Filamu hiyo ni Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri anayeshughulikia Biashara na Uwekezaji wa Ureno, Mhe. Bernardo Ivo Cruz amepongeza ziara ya Mhe. Dkt. Tax nchini humo akisema imekuja wakati mwafaka ambao wakati dunia ikiendelea kushuhudia changamoto mbalimbali za kiuchumi, Tanzania na Ureno zinaangalia  namna ya kushirikiana katika biashara na uwekezaji ili kujikwamua kiuchumi.

“Tanzania ni mshirika wetu muhimu katika biashara na uwekezaji na tupo tayari kuimarisha ushirikiano huu. Nakupongeza Mhe. Waziri kwa kufanya ziara katika kipindi hiki na tunaahidi kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji ikiwemo Kilimobiashara, Uchumi wa Bluu, Miundombinu na Sekta zingine za uwekezaji” alisema Mhe. Cruz.

Pia aliongeza kusema nchi yake inao Mpango wa miaka sita wa ushirikiano katika biashara na uwekezaji kuanzia mwaka 2021-2027 ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na mpango huo.

Akiwasilisha mada kuhusu Fursa za Uwekezaji zilizopo nchini kwa washiriki wa Jukwaa hilo, Mkurugenzi wa Biashara na Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Revocatus Rasheli amewahamasisha wawekezaji na wafanyabiasha kutoka Ureno kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji nchini huku akisema tayari anayo mkononi miradi 100 chini ya Sekta ya Umma na miradi 36 chini ya Sekta Binafsi ambayo ipo tayari na kwamba ni kiasi cha wawekezaji hao kuchagua na kuwekeza.

Aliongeza kusema Tanzania katika kuhamasisha uwekezaji imetenga ardhi yenye ukubwa wa Hekta milioni 1.6 kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo ambapo tayari Hekta 6,000 zipo Mkoani Morogoro kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo.

Pia alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji hao kuwekeza kwenye sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kujenga Hoteli, Nyumba za Makazi na  Kumbi za Mikutano.

“Serikali ya Tanzani ainazo fursa nyingi za uwekezaji. Nawakaribisha kuwekeza kwenye kilimo, uvuvi, madini, miundombinu lakini pia ujenzi wa hoteli, nyumba za makazi na kumbi za mikutano hususan katika miji mikuu ikiwemo Dar es Salaana na Makao Makuu ya Nchi yetu Dodoma ambako mahitaji ni makubwa zaidi” alisisitiza Bw. Rasheli.

Kadhalika, Mkurugenzi huyo amesema Ureno ni mdau muhimu katika ushirikiano na Tanzania na kwamba ipo haja ya kuongeza  biashara kati ya nchi hizi mbili ambapo  amesema hadi sasa Ureno imesajili miradi 13 nchini yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni Tisa ambayo imetoa fursa za ajira 325 kwa watanzania.

“Ziara hii ni muhimu sana kwetu Tanzania na Ureno, ni imani yetu kuwa ziara hii itaongeza wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Ureno kuja nchini ili kwa pamoja nchi hizi zinufaike kupitia ushirikiano mzuri uliopo” alisisitiza Bw. Rasheli.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanziabar (ZIPA) Bw. Emmanuel Mashimba amesema Serikali ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira wezeshi katika kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara na kwamba Ureno ni miongoni mwa nchi muhimu ambazo Zanzibar ipo tayari kushirikiana nazo katika sekta za uchumi wa bluu, utalii na miundombinu.

Mhe. Dkt. Tax yupo nchini Portugal kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 20 hadi 22 Oktoba, 2022. Akiwa nchini humo, Mhe. Dkt. Tax pamoja na mambo mengine atakutana kwa mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Joao Gomez Cravinho pamoja na kusaini Hati ya Makubaliano ya kuanzisha Majadiliano ya Kisiasa kati ya Tanzania na Ureno.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akiwa kwenye mazungumzo rasmi na Waziri wa Nchi wa Ureno anayeshughlikia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Bernardo Ivo Cruz mara baada ya kuwasili kwenye Makao Makuu ya Ofisi za Taasisi ya Biashara na Uwekezaji za nchi hiyo zilizopo jijini Lisbon. Akiwa katika taasisi hiyo, pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt. Tax alifungua rasmi Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno ambalo liliishirikisha Jumuiya ya Wawekezaji kutoka nchini humo. Mhe. Waziri Tax na yupo nchini Ureno kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia tarehe 20n hadi 22 Oktoba 2022

Mhe. Dkt. Tax akifungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno lililofanyika Lisbon. Pamoja na mambo mengine Mhe. Dkt Tax alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa Ureno kuwekeza nchini
Waziri wa Nchi wa Ureno anayeshughulikia masuala ya Biashara na Uwekezaji, Mhe. Bernardo Ivo Cruz naye akizungumza wakati wa Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Ureno

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Baiashara na Uwekezaji ya Ureno, Bw.Kuis Castro Henriques naye akiwakaribisha kwenye Ofisi za Taasisi yake washiriki wa Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno
Mkurugenzi wa Uwekezaji na Biashara kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Revocatus Rasheli akinadi fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo nchini kwa washiriki wa Jukwaa
la Uwekezaji kati ya Tanzania na ureno lililofanyika Lisbon
Balozi wa Tanzania nchini Ureno mwenye makazi yake nchini Ufaransa, Mhe. Samwel Shelukindo (kulia) akishiriki Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno. 

Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme (wa pili kulia) akiwa na Brigedia Generali Mbaraka Mkeremy wakifuatilia Jukwaa la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno

Washiriki wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania  na Ureno wakifuatilia mada zilizowasilishwa kwao

Washiriki wengine wakifuatilia matukio

Washiriki wengine kutoka Tanzania wakifuatilia mada wakati wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno lililofanyika Lisbon
Mhe. Dkt. Tax akimpatia zawadi kutoka Tanzania Mhe. Cruz. Zawadi hiyo ni mchanganyiko wa bidhaa za Tanzania kama vile Kahawa, Korosho, Batiki, Asali na Viungo vya Chakula

Mhe. Dkt. Tax akiagana na Mhe. Cruz mara baada ya ufunguzi wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Ureno

Picha ya pamoja
No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad