Mamlaka
ya Masoko Ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imeanzishwa chini ya Sheria ya
Masoko ya Mitaji na Dhamana sura ya 79 na kupewa jukumu la kuendeleza,
kuratibu na kusimamia masoko ya mitaji nchini.
CMSA kwa
kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa inayohusika na Usimamizi na watoaji
wa viwango vya Kimataifa vya masoko ya mitaji ulimwenguni yaani
International Organization of Securities Commissions (IOSCO)
inashiriki katika kuadhimisha wiki ya wawekezaji ulimwenguni iliyoanza
Oktoba 3 mpaka Oktoba 7 2022.
Lengo
la kushiriki katika Wiki ya Wawekezaji Duniani ni kuongeza uelewa
kuhusu umuhimu wa elimu kwaUmma na ulinzi wa maslahi ya wawekezaji kwa
kuangazia jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka za usimamizi wa
masoko ya mitaji katika maeneo haya muhimu.
Wiki ya Wawekezaji
Ulimwenguni inahusisha Mamlaka za usimamizi wa masoko ya mitaji ambazo
ziko chini ya IOSCO pamoja na wanachama wengine wa IOSCO katika mabara
sita ambazo hufanya shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa
njia za mawasiliano na huduma zinazomlenga mteja, kukuza ushindani wenye
tija unaolenga kuongeza wigo wa mikakati mbalimbali ya utoaji wa elimu
ya wawekezaji, kuandaa warsha na makongamano, pamoja na kutumia Mamlaka
zao kuendesha kampeni za kitaifa.
Wiki
ya wawekezaji inatoa nafasi ya upendeleo maalumu kwa wanachama wa IOSCO
kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau wote wanaotoa elimu ya uwekezaji
kwa umma kwa ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Kauli mbiu ya
mwaka huu ni “Uhimilivu wa wawekezaji na Mitaji Endelevu”.
Wiki
ya Wawekezaji Ulimwenguni inatarajiwa itaongeza uelewa wa fursa na
faida za kutumia masoko ya mitaji nchini ambao unalenga “ Kutambua
Ushindani na Maendeleo ya Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. Wiki ya
Wawekezaji Ulimwenguni pia inalenga kuongeza ushiriki wa wawekezaji
katika masoko ya mitaji hivyo kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa
wa Huduma Jumuishi za Kifedha na Mpango Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya
Sekta ya Fedha.
Pia ushiriki wa CMSA katika Wiki ya Wawekezaji
Ulimwenguni umeambatana na maono ya Serikali ya awamu ya sita chini ya
uongozi uliotukuka wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania, ambao unalenga kuweka mazingira wezeshi kwa
maendeleo ya sekta ya fedha kwa kuchochea maendeleo na ukuaji wa uchumi
Nchini.
Katika kuadhimisha wiki hii, CMSA itafanya shughuli
mbalimbali zinazolenga kuongeza uelewa, upatikanaji, ushiriki na kulinda
maslahi ya mwekezaji katika masoko ya mitaji kuanzia tarehe 3 mpaka 7
Oktoba 2022. Programu hii inalenga kuimarisha uelewa kuhusu masoko ya
mitaji hivyo kuchangia kwenye ajenda ya Taifa ya kuboresha Huduma
Jumuishi za kifedha na maendeleo ya uchumi.
CMSA kwa
kushirikiana na wadau wa masoko ya mitaji imezindua programu hii tarehe
3 Oktoba 2022 saa 4 kamili asubuhi katika ofisi za Mamlaka.
Tunawatakia wadau wetu wote mafanikio katika kuadhimisha Wiki ya Wawekezaji Ulimwenguni.
Imetolewa na:
CPA. Nicodemus D. Mkama,
Afisa Mtendaji Mkuu,
Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA)
Ghorofa ya 6 , Jengo la PSSF, Mtaa Ohio / Garden ,
No comments:
Post a Comment