Sekta ya Uchukuzi yazoa makombe SHIMIWI 2022 - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, October 16, 2022

Sekta ya Uchukuzi yazoa makombe SHIMIWI 2022

  Na Mwandishi Wetu, Tanga

WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) imezoa vikombe vya ushindi mbalimbali kwenye michezo ya 36 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) iliyomalizika Oktoba 15, 2022 jijini Tanga.

Uchukuzi imetwaa vikombe vya ubingwa wa jumla wa mchezo wa riadha, kombe la kuleta wachezaji 174 ambao ni wengi zaidi kuliko timu nyingine, kombe la ushindi wa pili wa kuvuta kamba kwa wanawake; huku wachezaji wake wametwaa medali baada ya kushika nafasi mbalimbali katika mchezo wa mbio za baiskeli kwa wanawake zilizokuwa za Km 25 mchezaji Scolastica Hasili ameshika nafasi ya pili.

Katika mbio za mita 100 wanawake na wanaume Jamila Mkomwa wa tatu na Baraka Mashauri (wa kwanza); Mashauri tena kawa wa pili katika mita 200; huku Aidan Andrean na Mastura Kaizer wameshika nafasi ya kwanza mita 400 kwa wanaume na wanawake; wakati Scolastica tena ameshika nafasi ya pili katika mita 800; na mbio za kupokezana vijiti za mita 100x4 wanaume wameshika nafasi ya pili na wanawake ya tatu.  

Katika mchezo wa soka, bingwa wa mchezo huo ni timu ya Hazina kutoka Wizara ya Fedha na Mipango; wakifuatiwa na Mahakama Tanzania na Wizara ya Ulinzi na Jeshi  la Kujenga Taifa; wakati  katika netiboli mabingwa ni Ofisi ya Rais Ikulu, wakifuatiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wametwaa ubingwa wakifuatiwa na Mahakama Tanzania na mshindi wa tatu ni Wizara ya Mambo ya Ndani; huku  kwa wanawake mabingwa ni Mahakama Tanzania wakifuatiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) na watatu ni Ofisi ya Waziri Mkuu Sera.

Kwa upande wa mchezo wa riadha waliotwaa ubingwa wa jumla kwa kutwaa medali nyingi ni Sekta ya Uchukuzi wakifuatiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii; na watatu ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; kwa upande wa mbio za baiskeli wanaume bingwa ni Bohari ya Dawa, wakifuatiwa Wizara ya Afya na watatu ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi; wakati kwa wanawake mabingwa ni Wizara ya Mambo ya Ndani, wa pili ni Sekta ya Uchukuzi na watatu ni Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi).

Kwa upande wa mchezo wa darts kwa wanaume mabingwa ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi  la Kujenga Taifa; huku ushindi wa pili umekwenda kwa Bohari ya Dawa na watatu ni Wizara ya Katiba na Sheria; huku kwa wanawake mabingwa ni Bohari ya Dawa, wakifuatiwa na Wizara ya Nishati na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC); wakati timu yenye nidhamu ni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi na kiongozi bora ni Julius Paul kutoka RAS Mara.

Nahodha wa timu ya Kamba wanaume kutoka Ofisi ya Rais Ikulu Hassan Malole akipokea kombe la ubingwa wa mchezo huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba (wa kwanza kushoto) wakati wa kufunga mashindano ya 36 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamefanyika kuanzia Oktoba 1-15, 2022 jijini Tanga. 
Ramadhani Wakilongo kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) akipokea kombe la ushindi wa jumla wa riadha wakati wa kufunga mashindano ya 36 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamefanyika kuanzia Oktoba 1-15, 2022 jijini Tanga. 

Bingwa wa mchezo wa Kamba wanaume Ofisi ya Rais Ikulu wakiwavuta timu ya Mahakama Tanzania kwa mivuto 2-0 kwenye fainali iliyochezwa wakati wa kufunga mashindano ya 36 ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ambayo yamefanyika kuanzia Oktoba 1-15, 2022 jijini Tanga. 


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad