RITA YAWATAKA WANANCHI KUANDIKA WOSIA ILI KUPUNGUZA WIMBI LA WATOTO WA MITAANI - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 21, 2022

RITA YAWATAKA WANANCHI KUANDIKA WOSIA ILI KUPUNGUZA WIMBI LA WATOTO WA MITAANI

Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini(RITA) umewataka wananchi kuwa na tabia ya  kuandika wosia mapema ili kupunguza wimbi la watoto wa mitaani ambalo linaonekana kuongezeka siku hadi siku nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa leo hii na Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji mkuu wa Wakala, Bi. Angela Anatory ofisini kwake  jijini Dar es Salaam na kusema wananchi wanatakiwa kujua jambo la kuandika wosia ni suala mtambuka kutokana na kukua sana kwa teknolojia nchini hivyo elimu hii kuwa wazi katika jamii. 

‘’Uandishi wa wosia una umuhimu mkubwa sana kwa jamii yetu ya kitanzania ambapo pamoja na mambo mengine utapunguza idadi ya watoto wa mitaani ambao kwa kiasi kikubwa hukimbia majumbani mwao kutokana na kunyanyaswa na ndugu pindi wazazi au mzazi anapofariki dunia.

 Lakini pia inapunguza utegemezi wa jumla kwa ndugu walioachwa na watoto kwani wosia unabainisha ni jinsi gani mali iliyoachwa na marehemu iweze kuwanufaisha wahusika(Wafaidikaji)’’. Alisema Bi. Anatory.

Akiongelea faida za kuandika wosia, Bi. Anatory anasema wosia unaweka mambo bayana kwa familia na jamaa, mtu anakuwa na uhuru wa kumchagua msimamizi wa mirathi anayempendekeza,Wosia unatoa maelezo ya kuhifadhi mwili wako na kwa jinsi gani mali yako igawanywe kwa mujibu wa sheria, kuondoa migogoro baina ya wanafamilia, kutoa muongozo wa kila mrithi apate kiasi gani cha sehemu ya mali iliyopo pamoja na kuandaa maisha bora kwa familia na ndugu wa marehemu.

Hatahivyo watanzania wengi wamekuwa na mawazo potofu juu ya kuandika wosia wengi wao wakiamini ni sawa na kujichulia ambapo mtu akiandika wosia basi muda si mrefu atafariki dunia kitu ambacho hakina ukweli wowote ndani yake.

Akizungumzia jambo hilo ambalo limekuwa ni changamoto kwa RITA, Bi. Anatory anasema kwa masikitiko kuwa “Mbali na kuendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali lakini kiukweli jambo hili limekuwa ni changamoto  kwa Wakala kutokana na watu wengi katika jamii yetu ya kitanzania kuwa bado hawana ufahamu tosha juu ya wosia hata kutokujua umuhimu wake kwa familia na jamii nzima, hivyo kupelekea kuwa na imani potofu kitu ambacho hakifai” alisema Bi. Anatory.

Wosia ni kauli au maandishi rasmi inayotolewa na mtu wakati wa uhai wake kwa hiari yake mwenyewe ili kuonesha nia yake jinsi gani angependa mali yake igawanywe baada ya kuondoka duniani. Hatahivyo mpaka sasa jumla ya wosia 1011 zimeandikwa na kuhifadhiwa RITA. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad