HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 18, 2022

TANROADS MKOA WA RUVUMA KUJENGA UPYA BARABARA KUU YA SONGEA-MAKAMBAKO

 

Na Muhidin Amri, Songea
SERIKALI kupitia wakala wa Barabara Tanzania(Tanroads) mkoa wa Ruvuma,inatarajia kuanza kujenga upya barabara ya lami kutoka Songea hadi Njombe kutokana na barabara hiyo kuwa nyembemba na kuisha muda wake.

Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi alisema, kwa kuanzia barabara hiyo itajengwa urefu wa km 97 kutoka Msamala Manispaa ya Songea hadi kijiji cha Lutikila Halmashauri ya wilaya Madaba.


Alisema, kwa sasa maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo yako katika hatua ya manunuzi na fedha kwa ajili ujenzi wa mradi huo zimepatikana ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia.


Alisema,katika eneo hilo la Msamala kutajengwa Round About na ndiyo itakuwa makutano ya barabara hiyo na ile ya Songea ByPass maarufu kama (Mtwara Corridor) yenye urefu wa km 14.3.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Songea wamesema,ujenzi wa barabara hiyo utasaidia kupunguza ajali zinazotokea mara kwa mara kutokana na barabara hiyo kwa sasa kuwa nyembamba na yenye mashimo kufuatia kujengwa siku nyingi.

Benjamini Haule alisema,barabara hiyo imekuwa chanzo cha ajli nyingi na kupoteza maisha ya watu ambapo ameiomba serikali kuharakisha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi.

Alisema kama serikali itafanikiwa kujenga upya barabara hiyo,ajali zinazoendelea kutokea mara kwa mara zitapungua kwa kuwa madereva wataendesha magari kwa usalama.

Alisema,tofauti na sasa ambapo baadhi ya madereva wanalazimika kupitisha magari yao hadi maeneo ya watembea kwa miguu ili kukwepa mashimo yaliyopo katikati ya barabara.

Prasida Mbogofela alisema, barabara ya Songea-Makambako kwa sasa imechoka na ina mashimo mengi, jambo linalosababisha kutokea kwa ajali nyingi hasa kwa watembea kwa miguu kugongwa na magari.

Mmoja wa madereva wa malori anayetumia barabara hiyo Mussa Shaban alisema, changamoto kubwa ya barabara hiyo ni utelezi pindi jua linapowaka na hivyo kusababisha ajali za mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad