HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 30, 2022

SIMBACHAWENE AZINDUA UTAFITI WA VIASHIRIA NA MATOKEO YA UKIMWI NCHINI

Waziri,George Simbachawene (wa tano kutoka kulia),viongozi mbalimbali wa serikali,wizara na taasisi pamoja na baadhi ya wadau wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuzinduliwa kwa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania. Picha na Baltazar Mashaka NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA

SERIKALI imezindua Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS 2022-2023) na kueleza kuwa kiwango cha maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI kimeshuka na kufikia asilimia 4.7.

Pia imedhamiria kudhibiti maambukizi ya VVU kwa kuongeza uelewa kwa wananchi,kujua hali zao za maambukizi ya VVU, kujiunga na huduma za matibabu ya VVU,kuongeza uelewa na ujuzi wa kukabiliana na janga hilo nchini.

Aidha utafiti uliofanywa mwaka 2016/17 ulionyesha idadi ya wanaoishi na virusi vya Ukimwi waliojitambua ilikuwa 61%, waliokuwa kwenye tiba 92% na waliofikia ufubazaji VVU 87%, matokeo ambayo umuhimu wake ulisaidia kuunda mkakati wa Kitaifa wa mwitikio wa VVU na UKIMWI.

Akizindua utafiti huo leo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene amesema utaiwezesha serikali kufahamu tabia hatarishi zinazochangia kuenea kwa VVU na viashiria vinavyotoa taarifa hizo vitazingatia umri,jinsia, maeneo na nchi kwa ujumla.

“Tunafahamu takwimu bora ni muhimu katika kufahamu ukubwa wa janga la UKIMWI katika nchi yetu,tunaendelea kukusanya takwimu bora zitakazotupa uelewa wa hali ya maambukizi na namna ambavyo programu na afua za VVU zinavyofanya kazi ili kufikia malengo ya 95 ya Shirika la UKIMWI duniani na kudhibiti janga hili ifikapo 2030,”amesema.

Simbachawene amesema,serikali inahitaji kuendelea kutathmini na kufuatilia kiwango cha maambukizi mapya,idadi ya watu wenye maambukizi ya VVU na walio kwenye matibabu ya ARV za kufubaza VVU.

“Utafiti wa viashiria vya VVU na UKIMWI mwaka 2022/2023 utakuwa wa tano kufanyika nchini baada ya utafiti wa mwaka 2016/2017 uliotoa mwanga juu ya namna tulivyoelekeza nguvu zetu kufikia malengo yaliyokusudiwa katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI,”amesema.

Pia utafiti huo ulionyesha kiwango cha maambukizi nchini, kushuka na kufikia asilimia 4.7 na ulionyesha idadi ya wanaoishi na virusi vya Ukimwi waliojitambua 61%,walio katika tiba 92% na waliofikia ufubazaji VVU 87%.

Simbachawene amesema tangu mwaka 2018,serikali inatekeleza kwa kasi afua zinazolenga kuwatambua wanaoishi na virusi vya Ukimwi na kuwaunganisha kwenye tiba za ARV wafikie ufubazaji wa VVU,hivyo serikali ina jukumu la kuwahakiki wanaoishi na virusi vya Ukimwi kupitiatafiti ngazi ya jamii na taifa kwa ujumla.

Amesema serikali kwa utafiti huu kama ulivyokuwa wa mwaka 2016/2017 utatoa takwimu za VVU zitakazotupa uelewa zaidi wa kukabiliana na janga la UKIMWI,takwimu zitatuongoza kuboresha mipango ya afya na mgawanyo wa rasilimali fedha katika program mbalimbali za VVU.

Waziri huyo amesema si kila mtu anayeishi na VVU nchini anafahamu hali yake,hivyo THIS 2022-2023 utatoa fursa kwa kaya takriban 19,000 kupimwa VVU majumbani na kujua hali zao siku hiyo hiyo,watapimwa ugonjwa wa homa ya ini ‘B’ na ‘C’ na watakaokutwa na maambukizi watapata huduma za afya.

“Watakaokutwa na maambukizi ya VVU kwenye utafiti huu wataunganishwa na vituo vya afya watakavyochagua ili kuanza matibabu,huduma za ARV zinapatikana bure katika vituo vyetu vya afya,na matibabu yanasaidia watu wanaoishi na VVU kuishi maisha marefu yenye afya na kupunguza hatari ya kuambukiza watu wengine,”amesema.

Mkurugenzi Mkazi wa ICAP,Haruka Mayaruma amesema utafiti huo ni sehemu ya mradi unaosimamiwa na ICAP unalenga kuongeza jitihada za kupambana na VVU zisingefanikiwa bila serikali,Kituo cha Dharura cha Magonjwa cha Marekani kwa kuwezesha tiba na matunzo kwa wanaoishi na VVU ili kupunguza vifo na maambukizi mapya.

Amesema kaya 20,000 sawa na watu 40,000 wa umri kuanzia miaka 15 na kuendelea kote nchini zitafikiwa na utafiti huo utakaosaidia kufikia malengo ya 95-959-95.

Balozi wa Marekani nchini,Dr. Donald Right amesema jitihada zinazofanywa na serikali ya Tanzania zitasaidia mapambano dhidi ya UKIMWI ingawa eneo la mambukizi ya mtoto kutoka kwa mama hatufanya vizuri na kusistiza tujifunze kwa matokeo ya nyuma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kifua Kikuu na UKIMWI,Fatuma Towafiq alisema Bunge litaendelea kuishauri na kuisimamia serikali itenge bajeti ya VVU na anaamini utafiti huo ukifanyika kwa weledi na umakini utatoa matokeo sahihi yenye tija na kuwawezesha Watanzania kuwa an afya bora.

Naye Naibu Katibu Mkuu Seif Shekilaghe, kwa niaba ya Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu, amesema utafiti huo wa tano kufanyika utaonyesha namna ya kutekeleza mapambano ya VVU na utangalia magonjwa mengine ikiwemo homa ya ini ili kufikia malengo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) Dr.Leonard Maboko amesema za mwaka 2017 zilionyesha watu milioni 1.4 walikuwa na maambukizi mapya na mwaka 2021 watu milioni 1.7 walikadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU.

“Asilimia 84 wanafahamu hali zao,73 asilimia wanafikiwa na huduma za afya na 66 asilimia wanatumia dawa za kufubaza virusi (ARV),hivyo takwimu za THIS 2022-2023 zitasaidia kutupima na kuwa na ujuzi wa masuala ya VVU,”amesema Maboko.

Henry Karugendo wa Taasisi ya Takwimu la Taifa (NBS) amesema watashirikiana na Wiara ya Afya kupanga mipango ya afya kwa kutumia takwimu bora za VVU ambazo ni nyenzo muhimu ya kuiwezesha serikali na wadau kuandaa sera, mipango na takwimu rasmi za mapambano ya VVU kuhakikisha watu wanapata huduma za matibabu.
“Takwimu za utafiti wa THIS 2022-2023 zitaonyesha kiwango cha maambukizi mapya ya VVU, kiwango cha watumiaji dawa, kiwango cha homa ya ini B na C na uelewa wa wananchi na kuisaidia serikali kuboresha huduma za afya,VVU na ustawi wa wananchi,”amesema
Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) George Simbachawene akizungumza na wadau wa masuala ya afya na ukimwi (hawapo pichani) kabla ya kuzindua Utafiti wa Viashia na Matokeo ya Ukimwi Tanzania.
Mkurugenzi Mkazi wa ICAP,Haruka Mayaruma, akiwaeleza wadau (hawapo pichani) Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania (THIS 2022-2023) utakavyofanyika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad