Na Gasto Kwirini wa Jeshi la Polisi Arusha.
JESHI la Polisi kupitia dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Arusha limeitaka jamii kuacha tabia ya kuwadhihaki na kuwafanyia mizaa watu wote wenye ulemavu hususani wa ngozi.
Hayo yamesemwa leo Septemba 30, 2022 na Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto mkoa wa Arusha Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Happiness Temu wakati akitoa elimu ya ukatili kwa wazazi na watoto wenye ulemavu wa ngozi katika ofisi za taasisi ya Tumain Mission zilizopo Sakina Jijini Arusha.
ASP TEMU alisema kuwa kuna baadhi ya watu wamekua na tabia ya kuwafanyia vitendo vya ukatili watu hao wenye ulemavu ikiwemo kuwatolea maneno ya dhihaka hivyo akawataka kuacha tabia iyo kwani watachukuliwa hatua za kisheria.
“Jamii inatakiwa kufahamu kuwa wale ni watu na wana haki zao, wengine wamekua wakitembea barabarani na kutolewa maneno mbalimbali ambayo ni ya kuwakatisha tamaa na ni sawa na kuwanyanyapaa hivyo wananchi wanapaswa kuwachukulia kuwa ni sehemu ya jamii” Alisema ASP Temu.
Mkuu huyo wa dawati la jinsia alibainisha kuwa katika kikao hicho washiriki walipata fursa ya kuelimishwa maana halisi ya ukatili, aina za ukatili, madhara yatokanayo na ukatili na hatua za kuchukua pindi watakapo kuwa wamefanyiwa vitendo vya ukatili.
Naye bwana Herri Mollel kwa niaba ya wenzake alisema wanalishukuru Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu hiyo ambayo itawasaidia kujitetea wenyewe na usalama wao kwa ujumla ambapo wamehamasika na kujiona kuwa wana haki sawa na watu wengine.
Sambamba na hilo alitoa wito kwa watu wenye ulemavu kutokuwa na wasiwasi, watambue kuwa wao ni binadamu wa kawaida na kufanya kazi kwa kushirikiana na pindi wakisikia wito wowote kwa ajili ya kushiriki elimu mbalimbali zinazotolewa wasiache kwenda kwani usalama wao upo na kumalizia kwa kusema kuwa wataendelea kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusiana na matukio ya kihalifu.
Katika tukio hilo watoto hao pamoja na wazazi walipewa msaada wa mafuta kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi toka taasisi ya Tumaini Mission iliyopo Jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment