HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, September 11, 2022

Seriakli ya Awamu ya Nane imekusudia kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya Elimu

 

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo katika mkutano na walimu wakuu wa skuli za sekondari, Msingi, maandalizi na wenyeviti wa kamati za skuli kwa Mkoa wa Kusini Unguja uliofanyika katika ukumbi Mkutano wa Dkt. Ali Muhammed Shein Tunguu.

Ameeleza kuwa serikali imeamua kuipa kipaombele sekta ya elimu kulingana na mahitaji ili kuzalisha wataalamu walio bora.

Mhe. Hemed amewataka walimu wakuu kuwajibika, kufatilia na kusimamia vyema walimu walio chini yao pamoja na wanafunzi ili kujenga nidhamu na mustakabali mwema.

Amesema kuwa kila mwalimu mkuu lazima asimamie kwa kufuata misingi ya sheria, haki na wajibu ili kufanikisha azma ya serikali ya kutatua changamoto ya elimu kwa mikoa yote ukiwemo mkoa wa kusini unguja.

Aidha makamu wa pili wa rais ameutaka uongozi wa wizara elimu kuangalia upya vigezo vya upatikanaji wa walimu wakuu kulingana na sifa, zilizowekwa kisheria ili kuirejeshea heshima sekta ya elimu Zanzibar.

“kuna walimu wakuu hawana sifa ya kuwa mwalimu mkuu,hana ufatiliaji hana usimamizi nzuri wala ushirikiano na wenziwe mwalimu kama huyu hafai lazima awajibishwe” amesema

Mhe. Hemed amesema wizara ni lazima kuhakikisha wanawasimamia ipasavyo walimu wakuu wote kwa lengo la kuboresha elimu na kuongeza ufaulu ili kupata viongozi bora na wataalamu wa baadae.

Aidha makamu wa pili ameutaka uongozi wa mkoa kushirikiana na kamati za skuli za mkoa kuhakikisha wanaimarisha nidhamu kwa wanafunzi ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa mkoa huu.

“ Ni lazima kuhakikisha tunasonga mbele kwenye upasishaji wa wanafunzi kwani serikali imedhamiria kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekata ya Elimu kwa mikoa yote ikiwemo mkoa wa kusini Unguja” amesema

Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dkt. Hussen Ali Mwinyi itahakikisha inatatua changamoto zote za walimu ikiwemo vifaa vya kusomeshea ili kurahisisha ufanyikaji wa kazi kwa maslahi ya taifa.Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhakikisha katika ajira mpya za walimu ni vyema kuwapa kipaombele walimu wanaokaa maeneo husika ili kuondosha changamoto za ufanyaji wa kazi.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. LEILA MOHAMED MUSSA amesema wizara imejipanga kufungua kitado cha tano na cha sita katika skuli ya Hasnuu Makame ili kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wanaofaulu kufata elimu hiyo maeneo ya mbali.

Mhe Leila amesema wizara itahakikisha inazitatua changamoto zote zinazowakabili walimu ili yale malengo ya serikali ya kutoa elimu bora wananchi na kupata wataalamu bora liweze kufikiwa.

Kwa upande wao walimu wakuu na wenyeviti wa skuli za Mkoa wa kusini Unguja wameiomba Serikali kuondosha changamoto zote zinazowakabili walimu wa mkoa huo ikiwemo uhaba wa walimu, uhaba wa vitendea kazi , pamoja na kupatiwa stahiki zao ili kuleta ufanisi.

Katika hatua nyingine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amekutana na madaktari na wahudumu wa afya wa mkoa wa kusini Unguja katika ukumbi Mkutano wa Dkt. Ali Muhammed Shein Tunguu na kuuwagiza uongozi wa Wizara ya Afya kuwalipa maafisa ambao wana madai mbali mbali si zaidi ya wiki moja.

Mhe. Hemed ameutaka uongozi huo kumchukulia hatua za kisheria mtu yeyote kwenye miradi ya wizara ya afya ambae ni kikwazo cha maendeleo ili kuleta ufanisi mzuri wa kazi.

Mhe.hemed amewataka wale wote waliopewa dhamana ya kutunza vifaa kinga na tiba kuwa waaminifu kwani serikali haitomvumilia mtu yeyote ambae ataenda kinyume na kinyume na taratibu za kiutendaji ikiwemo wizi, wabadhilifu wa mali za umma na wengineo.

Aidha makamu wa pili wa rais amemtaka mkurugenzi utumishi wa wizara ya Afya kuwapatia vitambulisho wafanyakazi wote pamoja na kusimamia uthibitisho wa wafanyakazi wapya kisheria ili waweze kupatiwa haki zao kama wafanyakazi wengine.

Amesema serikali imeamua kuboresha maslahi ya madaktari na kuimarisha vitendea kazi ili kuleta ufanisi mzuri katika kazi zao hivyo amewataka kufanya kazi kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia utaalamu na uzoefu wao.

Aidha Mhe. Hemed amewataka wataalamu hao kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa wanaofika hospitalini ili kupata faraja na uponaji wa maradhi waliyonayo

Mhe. Hemed amesema kuwa Serikali imejipanga kutatua changamoto zote zinazoikabili sekta ya Afya ikiwemo upatikanaji na vifaa tiba pamoja na malipo ya fedha za likizo kwa watendaji ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Mhe.Hassan Khamis Hafidh amesema kuwa Wizara imejipanga kuhakikisha kila mfanyakazi analipwa stahiki yake ikiwemo posho la mazingira magumu na kupeleka madaktari bingwa kila hospitali ya wilaya.

Mhe.Hassan amesema kuwa Serikali imejipanga kuajiri kwa wilaya ili kuondosha changamoto za usafiri kwa watendaji kulindana na maeneo wanaoishi na sehemu zao za kazi.

Aidha Mhe. Hassan amewataka watumishi wa afya ambao wamepetiwa nyumba za makaazi kuzitunza nyumba hizo ili ziweze kuwasaidia kwa wafanyakazi wa sasa na baadae.

Nao madaktari wa mkoa huo wameiomba Serikali kuwapatia haki zao zote ili kuweza kutoa huduma bora kwa kila mwananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad