HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, September 26, 2022

Msitu uliotunzwa zaidi ya miaka 800 wa NYUMBANITU (Nyumba nyeusi) waingia kwenye orodha ya vivutio vya utalii Tanzania

 Njombe

WIZARA ya Mali asili na Utalii kupitia makumbusho ya taifa imetangaza rasmi msitu wa NYUMBANITU uliopo katika kijiji cha Mlevela halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe kuwa miongoni mwa kivutio muhimu cha utalii na utamaduni Tanzania.

Waziri wa Mali asili na Utalii Dkt,Pindi Chana amebainisha hilo wakati wa zoezi la kuweka bango la taarifa katika msitu huo wa asili na mapango ya NYUMBANITU na kuagiza jamii kuendelea kutunza maeneo hayo yenye historia kubwa kutokana na mashujaa wa vita ya Maji Maji kuyatumia kwa ajili ya kujificha wakati wa vita.

“Ni mategemeo yangu kwamba sasa NYUMBANITU inaingia katika orodha ya wizara ya vivutio muhimu vya utalii na utamaduni,ni mategemeo yangu kuwa sasa kituo chetu cha kijiji cha Makumbusho kitashirikiana na wazee wa mila na desturi kuhifadhi na hivyo kutanua wigo wa vivutio vya utalii vilivyopo hapa NYUMBANITU”amesema Pindi Chana

Awali akitoa taarifa kwa niaba ya bodi ya Makumbusho ya Taifa mwenyekiti wa bodi hiyo Dkt,Oswald Masebo amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano wa Makumbusho ya Taifa unaoelekeza kutekeleza uhifadhi endelevu wa mali kale.

Ameongeza kuwa mpaka sasa Makumbusho ya Taifa ina vituo 7 vya Makumbusho na maeneo ya mali kale zaidi ya 90 yaliyohifadhiwa nchini huku ikiwa imeshaandaa taarifa ya Awali ya kutambua juhudi za wananchi,taasisi mbali mbali za kuanzisha Makumbusho na kuhifadhi mali kale kwa kuwa zaidi ya Makumbusho 40 zinasimamiwa na jamii,halmashauri,mashirika mbali mbali.

“Zoezi la leo ni kufungua ukurasa mpya wa mpango wa kutambua juhudi za wanajamii wa Wanging’ombe na Njombe za kuhifadhi na kuendeleza mali kale”amesema Masebo

Julius Msigwa ni mzee wa mila na destuli wa msitu huo amesema wamekuwa wakiulinda msitu huo huku wakiutumia kwa shughuli mbalimbali ikiwemo ibada za mila huku wakiiomba serikali kuunga mkono matarajio yao ya ujenzi wa chuo cha sanaa na utamaduni na Makumbusho jirani na mapango ya NYUMBANITU.
Waziri wa Mali asili na Utalii Dkt,Pindi Chana akikata utepe mara baada ya zoezi la kuweka bango la taarifa katika msitu wa asili na mapango ya NYUMBANITU yaliyopo wilayani Wanging’ombe.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad