WANANCHI MBINGA WAKUBALI KUVUNJA NYUMBA ZAO KWA HIARI KUPISHA UJENZI WA BARABARA - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 16, 2022

WANANCHI MBINGA WAKUBALI KUVUNJA NYUMBA ZAO KWA HIARI KUPISHA UJENZI WA BARABARA


Baadhi ya madaraja ya zamani ambayo yatavunjwa ili na kujengwa mapya katika mradi wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Amanimakolo-hadi Luanda wilayani Mbinga

Baadhi ya nyumba zilizovunjwa na wananchi wa kijiji cha Amanimakolo wilayani Mbinga kwa hiari yao ili kupisha ujenzi wa mradi wa barabara ya lami kutoka Amanimakolo hadi Luanda yenye urefu wa km 35.
upanuzi wa barabara unavyoendelea katika ujenzi wa mradi wa Barabara ya Amani makolo-Luanda wilayani Mbinga.

Na Muhidin Amri, Mbinga
WANANCHI wanaoishi kando kando ya barabara ya Kitai-Luanda- Lituhi inayojengwa kwa kiwango cha lami na wakala wa barabara Tanroads mkoa wa Ruvuma, wameanza kuvunja nyumba zao kwa hiari ili kupisha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema,wameamua kuvunja nyumba zao kwa kuwa mradi huo ni muhimu kuliko hata nyumba zao kwani kwa muda mrefu walikuwa wanapata mateso makubwa ya usafiri ,usafirishaji wa bidhaa na madhara ya kiafya.

Halfan Nambasi mkazi wa kijiji cha Amani makolo alisema,kile kinachofanywa na serikali kina thamani kubwa kuliko nyumbani zao, na ameipongeza sana serikali kupitia Tanroads mkoa wa Ruvuma kwa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani.

Alisema,kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kutaharakisha sana kukua kwa uchumi na kupungua kwa gharama ya usafiri kwa wananchi na usafirishji wa mizigo.

Nambasi alisema,barabara hiyo ni ukombozi mkubwa kwa wakazi wa vijiji mbalimbali kwa sababu licha ya itakwenda kuharakisha kukua kwa uchumi wa vijiji hivyo, itahamasisha wawekezaji wengi kwenda kuwekeza katika madini yanayopatikana kwa wingi katika ukanda huo.

Aidha,ameiomba serikali kupitia Tanroads kuwa karibu na mkandarasi ili aweze kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na ajenge kwa viwango ili kuepusha usumbufu unaoweza kutokea wa kufanya matengenezo ya mara kwa mara.

Alisema,barabara hiyo ndiyo uti wa mgongo kwa uchumi wa wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa sababu barabara ndiyo inayotumika kupita malori shehena ya makaa wa mawe kutoka kwenye migodi kwenda maeneo mbalimbali hapa nchini.

Osias Haule alisema, kwa muda mrefu walikuwa katika mateso na kupata madhara makubwa kiafya kutokana na vumbi kubwa linalotoka barabarani na kuingia majumbani pindi malori ya makaa ya mawe yanapopita na kuna baadhi ya watu wamepoteza maisha yao kwa sababu ya kutojua njia sahihi ya kujkinga na vumbi la makaa ya mawe.

Alisema,baadhi ya wananchi walichukia uwekezaji huo licha ya kuwa na manufaa makubwa yanayopatikana,lakini hawana uwezo wa kuzuia magari yasipite katika bara bara hiyo bali waliendelea kuumia huku wakimuomba Mungu awanusuru na mateso hayo.

Alisema, mara baada ya kuona serikali imeanza kujenga kwa lami sasa wananchi wengi wana furaha na kwa kuwa baada ya muda mfupi wataondokana na kero hiyo na kuipongeza serikali ya awamu ya sita kwa hatua hiyo.

Benedict Haule mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Amani makolo alisema, hiyo ni hatua kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo na wilaya ya Mbinga kwa ujumla na amewaomba wananchi ambao bado hawajabomoa nyumba zao kufanya hivyo ili kupisha kazi ya ujenzi ili iweze kukamilika kwa muda uliopangwa.

Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo kutoka wakala wa barabara mkoa wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Andrew Sanga alisema,barabara hiyo inajengwa na kampuni ya China Ralway Seventh Group Ltd(CRSG) kutoa nchini China.

Alisema,katika awamu ya kwanza itajengwa urefu wa km 35 kwa kiwango cha lami kutoka kijiji cha Amani makolo hadi Luanda,lakini katika mpango wa baadaye serikali inakusudia kujenga barabara hiyo hadi Lituhi.

Alisema,kwa sasa kazi inafanyika katika kipande cha Kitai kuelekea Luanda ambapo katika hatua ya awali mkandarasi ameanza kusafisha barabara na kuondoa udongo usiohitajika.

Alisema, mradi huo utahusisha ujenzi wa madaraja makubwa matano na madaraja mengine madogo kama sabini, ambapo kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kunakwenda kufungua shughuli za kiuchumi kwa wananchi na kumaliza kabisa changamoto ya usafiri iliyopo hivi sasa.

Alisema,kazi inakwenda vizuri na kasi ya mkandasari ni kubwa na mara barabara hiyo itakapokamilika itasaidia sana kiuchumi ikiwamo usafirishaji wa makaa ya mawe na kuongezeka kwa wawekezaji kwenye sekta ya madini ya makaa ya mawe.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad