HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 16, 2022

TANZANIA NA OMAN KUSHIRIKIANA KUKUZA SEKTA YA NISHATI

WAZIRI wa Nishati Mhe.January Makamba amekutana na Mhe. Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud Hilal Al Shidhani na kuzungumzia fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi hususani katika miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini.


Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi ndogo ya Wizara ya Nishati Jijini Dar es salaam leo tarehe 16 Agosti,2022 na yalijikita katika kuzungumzia makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan yaliyofanyika nchini Oman Juni, 2022 ambayo aliambatana na Mhe. Makamba na Waziri wa Utalii na Maliasili Dkt. Pindi Chana.

Kupitia Mazungumzo hayo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) litashirikiana na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Oman (OQ) kufanya biashara ya mafuta ya jumla (fuel supply), kujenga vituo vikubwa vya gesi za mitungi (LPG) na kushirikiana na Kampuni Tanzu ya TPDC (TANOIL) ili kufanya biashara ya rejareja ya mafuta.

Halikadhalika, wataalamu kutoka nchini Oman kuendelea kuja nchini Tanzania kuangalia miundombinu ya Bandari na kutazama maeneo ya kuwekeza kwenye miundombinu ya kupokea, kushusha, kuhifadhi na kutoa mafuta katika Bandari na Ghala za dhamana ya forodha pamoja na kubadilishana uzoefu na Tanzania.

Waziri wa Makamba wakati wa mazungumzo hayo amesema Tanzania inatafuta Washirika wa kimkakati ambao watashirikiana na TPDC katika kutafuta mafuta na gesi katika vitalu vilivyopo ili kuchochea ukuaji wa viwanda na kuongeza ukuaji wa uchumi nchini hususan katika miradi ya kimkakati ukiwemo wa Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza katika Mkutano huo Mhe. Balozi Saud Hilal Al Shidhani pamoja na kutoa salaam za Rais wa Oman amemshukuru Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa utayari wake wa kushirikiana na Oman katika kuendeleza sekta ya nishati.

Aidha, amesema Oman ina ujuzi mkubwa katika masuala ya mafuta hivyo amemhakikishia Waziri Makamba kuwa watashirikiana vyema katika kukuza sekta hiyo nchini Tanzania.






No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad