
Kuongezeka kwa mwamko na uelewa kuhusu taarifa za hali ya hewa ni muhimu kwani taarifa zikiifikia jamii kwa wakati, uhakika na usahihi itaisaidia mamlaka husika kupanga mipango ya kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa, upatikanaji wa chakula na lishe bora pamoja na afya kwa ustawi wa jamii.
Hayo yamesemwa leo Agosti 31,2022 na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi wakati akifungua warsha ya siku moja ya wanahabari kuhusu mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2022 iliyofanyika Kibaha, Mkoani Pwani
Amesema, mvua za Vuli ni mahsusi kwa maeneo ya kaskazini mwa nchi ambayo hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka hivyo ni vema wananchi wakifuatilia taarifa za hali ya hewa hasa katika kipindi hiki kwani mvua za Vuli zina mchango mkubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, nishati, maji n.k.
Ameongeza kuwa, kupatikana kwa taarifa sahihi za hali ya hewa pamoja na athari zake ni muhimu zitawawezesha wananchi na sekta mbali mbali kujipanga na kujiandaa katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.
"Kupatikana kwa utabiri huu kwa usahihi na kwa wakati itachangia katika jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hasan katika kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, nchi kwa ujumla pamoja na kuboresha miundombinu na huduma za kijamii, amesema Dkt. Kijazi
Amevipongeza vyombo vya habari Tanzania kwa kufanya kazi nzuri katika utoaji taarifa za hali ya hewa Zinazoiwezesha jamii na wadau mbali mbali yakiwemo mashirika, taasisi na sekta mbali mbali kupata taarifa na kuelewa kuhusu Utabiri wa hali ya hewa na namna taarifa hizo zinavyoweza kutumika katika shughuli za maendeleo ya nchi.
No comments:
Post a Comment