HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, July 22, 2022

MANISPAA YA TEMEKE YATENGA MILIONI 998 KUENDELEZA MAENEO YA WAZI

Mkuu wa Wilaya Temeke, Jokate Mwegelo,  akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Mshauri wa Mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam (DMDP) wilayani humo, Selemani Hamduni, kuhusu mradi wa ujenzi wa bustani na viwanja vya michezo katika viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam.
Na Mwanadishi Wetu

HALMASHAURI ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam imetenga zaidi ya Shilingi milioni 998 kuendeleza maeneo ya wazi na upandaji miti 1927 katika Manispaa hiyo.

Akizungumza alipotembelea eneo la wazi la Mwembeyanga, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Jokate Mwegelo amesema, mradi huo ni sehemu ya  lengo la Jiji la Dar es Salaam la kuboresha maeneo yake na kuyafanya kuwa ya kijani ' Green Dar'.

Jokate amesema mradi umeshaanza ambapo kwa  sasa wanaboresha eneo la wazi la Mwembeyanga kwa kujenga viwanja vya michezo, upandaji miti maeneo hayo ya wazi, ukarabati wa mifereji kwenye baadhi ya barabara pamoja na kupanda miti na maua kwenye mfereji wa Serengeti na kandokando ya barabara ya Mtoni Kijichi kuelekea Toangoma ndani ya Manispaa hiyo.

" Kuhusu upandaji wa miti, miti 1427 itapandwa na Halmashauri katika maeneo hayo yaliyotajwa, miti 500 watapewa wananchi kwenda kupanda kwenye maeneo yao.Manispaa ya Temeke inatekeleza wa vitendo maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos ya Makalla ya kutaka Jiji kuwa Safi na maeneo ya wazi ya kupumzika wananchi.

"Sasa pamoja na usafi tunaofanya, uwepo wa maeneo haya ya wazi yakiwa kwenye ubora mzuri si tu tutapendezesha Jiji, lakini pia tutakuwa tumewapa wananchi maeneo ya kupumzika.Mradi huo umewazingatia wakazi wa Halmashauri hiyo kwa kuwa baadhi ya vibarua ni wakazi wanaozunguka maeneo ya mradi huu,"amesema Jokate.

Aidha, amewataka wananchi wa Manispaa hiyo kutunza mazingira na miundo mbinu hiyo pindi mradi huo utakapokamilika.

Kwa upande wake Mratibu  wa mradi huo ambaye pia ni Meneja wa Wakala wa ujenzi wa barabara Mjini vijijini (TARURA) Manispaa Temeke, Injinia Paul Mhere amesema mpaka sasa utekelezaji wa  mradi huo ulioanza wiki mbili zilizopita umefikia asilimia 25.

Amesema mara baada ya kukamilika ujenzi wa maeneo hayo ya wazi yatakuwa chini ya Halmashauri lakini wananchi hawatatozwa malipo kutumia maeneo hayo.

" Kwa wale waliokuwa wakifanya shughuli mbalimbali katika eneo la Mwembeyanga wataendelea na shughuli zao ingawa Halmashauri itaweka utaratibu mzuri na hakutakuwa na kiingilio."

Wakati huo huo Msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya ukandarasi ya Group Six International Seleman Hamduni, amesema  mradi huo utakamilika baada ya miezi miwili.

" Kazi kubwa kwenye maeneo haya ya Mwembeyanga ni ujenzi wa miundombinu ya maeneo haya ya wazi kama maeneo ya michezo, tumeanza na tumeshafikia asilimia 25 ya ujenzi wake, mkataba wa mradi huu ni miezi miwili na utakamilika kwa wakati," amesema.



Matukio mbalimbali katika picha wakati Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo akikagua maendeleo ya utekelezaji wa uboreshaji eneo la Mwembeyanga wilayani humo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mkakati wa kuboresha miundombinu na kupendezesha maeneo ya wazi na barabarani kwa kupanda miti na maua.
 


 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad