HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 6, 2022

BALOZI MULAMULA APOKEA NAKALA ZA HATI ZA UTAMBULISHO

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema kuwa Serikali haiwezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo bila ya kuwa na sekta binafsi iliyoimarika.


Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 5 Julai 2022 jijini Dar Es Salaam wakati akipokea nakala za Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Uganda hapa nchini, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye.

Balozi Mulamula amesema kuwa Tanzania na Uganda zina uhusiano mzuri wa kihistoria na umekuwa ukiimarika siku hadi siku kutokana na masuala mbalimbali ya ushirikiano yanayoendelea, yakiwemo ziara za viongozi wa kitaifa.

Alisema kuwa hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan alifanya ziara nchini Uganda ambapo makubaliano na ahadi mbalimbali zilitolewa katika ziara hiyo. Makubaliano hayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa sekta binafsi za nchi hizi mbili zinawekewa mazingira mazuri ya kufanya uwekezaji na biashara kwa faida ya wananchi wake.

Alielezea matumaini yake kuwa Balozi Mteule atahakikisha kuwa ahadi na makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande mbili hizo yanatekelezwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga unatekelezwa kama ulivyopangwa.

Mhe. Waziri alimalizia kwa kumuhakikishia Balozi huyo kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla itampa ushirikiano wa kutosha ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Balozi Mwesigye aliahidi kuwa atatumia ujuzi na maarifa aliyopewa kwa kushirikiana na wenzake balozini kuhakikisha kuwa makubaliano na maelekezo yaliyotolewa wakati wa ziara za viongozi wa kitaifa na majukwaa mengine yanatekelezwa ipasavyo.
Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye akiwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula jijini Dar Es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiendelea na mazungumzo na Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiwa katika mazungumzo na Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye baada ya kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula na Balozi Mteule wa Uganda nchini Tanzania, Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wao baada ya kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad