HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 1, 2022

WATANZANIA TUILINDE NA KUTUNZA MISITU YETU - MAJALIWA

 WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika utunzaji wa misitu kwa kutekeleza azma ya uhifadhi na uendelezaji misitu kwa vitendo.


Amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) imeendelea kuratibu utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji na utunzaji wa miti inayotekelezwa nchini kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

“Katika kipindi cha mwaka 2020/21, Halmashauri 27 kati ya 184 zilivuka lengo la kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka ambapo idadi ya miti 202,923,907 ilipandwa na miti 165,501,119 ilistawi, ambayo ni sawa na asilimia 81.6”

Amesema hayo leo (Jumatano, Juni 01, 2022) wakati akizindua zoezi la upandaji miti katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma. “Watanzania tuendelee kupanda na kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa miti na misitu kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu.

Amesema kuwa suala la upandaji wa miti na kuitunza ni la muhimu kwa ustawi wa mazingira ya Taifa kwani hatua hiyo inakwenda sambamba na uhimili wa mabadiliko ya tabia ya nchi na kuwezesha mazingira kuwa ya kijani na mandhari mazuri ya kuvutia.

“Ndege wa angani na wanyama wa porini wote wanategemea miti kwa chakula na wengine kwa makazi. Hata mifugo na binadamu tunategemea miti kwa chakula na mahitaji mengine.”

Aliongeza kuwa sekta ya misitu huchangia asilimia 45 ya mahitaji ya malighafi ya ujenzi, hulinda vyanzo vya maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kwa kutambua umuhimu huo Serikali ya Awamu ya Sita imeweka kipaumbele katika utunzaji wa misitu na imekuwa ikitekeleza azma ya uhifadhi na uendelezaji misitu kwa vitendo. “Tayari Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania imeshaanzisha mashamba makubwa ya miti.”

“Misitu huchangia kuinua pato la Taifa na pato la mtu mmoja mmoja, Serikali kwa kutambua hilo imeendelea kutekeleza mikakati ya kuwanufaisha wananchi wanaoishi jirani na misitu kupitia miradi ya ufugaji nyuki na miradi ya ufundi seramala.”

Akizungumzia kuhusu kampeni ya kukijanisha Dodoma Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2021/2022 jumla ya miti 692,247 ilipandwa katika wilaya zote za Mkoa wa Dodoma.

“Dodoma Mjini imepandwa miti 584,790; Wilaya ya Mpwapwa miti 21,450; Wilaya ya Bahi miti 20,720; Wilaya ya Chemba miti 4,000; Wilaya ya Kongwa miti 45,587; Wilaya ya Kondoa miti 11,200; na Wilaya ya Chamwino miti 4,500.”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kwa kushirikiana na timu inayosimamia na kuratibu ujenzi wa Mji wa Serikali zihakikishe miti ya aina mbalimbali inapandwa na kutunzwa katika maeneo yaliyoainishwa ikiwemo kuhakikisha mifumo ya umwagiliaji inafungwa mapema iwezekanavyo.

Pia, amewaagiza wataalamu wa mazingira waielimishe jamii juu ya upandaji bora wa miti kwa kuzingatia hali ya hewa ya eneo husika ili upandaji huo uwe na tija. “Kumekuwa na jitihada nyingi sana za upandaji miti, nisisitize miti ipandwe kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wetu. Nitoe wito kwa wataalamu kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu bora ili upandaji miti uwe na tija zaidi.”

Kwa upande wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jaffo amesema kuwa wamejipanga kuendelea kuipa kipaumbele ajenda ya utunzaji wa mazingira. “Hatuwezi kuupeleka uchumi wetu mbele kama tutadharau na kuacha kutunza mazingira yetu”.

Kaulimbiu ya Siku ya Mazingira Duniani itakayoadhimishwa Juni 05, 2022 ni ‘Tanzania ni Moja Tu, Tunza Mazingira’
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua zoezi la upandaji wa miti katika Mji wa Serikali, eneo la Mtumba jijini Dodoma, Juni 1, 2022.
Wasanii wa kikundi cha Mchoya kutoka Chalinze Nyama Dodoma wakicheza ngoma ya asili ya kabila la Wagogo katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika Mji wa Serikali, eneo la Mtumba jijini Dodoma Juni 1, 2022. Mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad