HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, June 27, 2022

Wanawake Tanzania wahamasishwa kujiunga na sekta ya madini

Bi. Sophia Mwanauta mchimbaji madini kutoka Mbeya na Mratibu wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini akichangia mada wakati wa mkutano mkuu wa kikatiba wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Kamisha wa Madini, Dkt. Abdul Rahman Mwanga (katikati) akizindua katiba mpya ya Chama cha Wanawake Wachimba Madini Tanzania (TAWOMA) wakati wa mkutano mkuu wa kikatiba wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki. Wengine ni Mwenyekiti mpya wa TAWOMA, Bi. Semeni John Malale (kulia) na Makamu Mwenyekiti wa chama, Bi. Rachel Njau (kushoto, mwenye miwani).
Mwenyekiti mpya wa Chama cha Wanawake Wachimba Madini Tanzania (TAWOMA), Bi. Semeni John Malale (wa pili kulia) akiongea na wajumbe wakati wa mkutano mkuu wa kikatiba wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Bi. Salma Ernest akisisitiza jambo wakati wa mkutano mkuu wa kikatiba wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Bi. Sarah Rusambagula, mchimbaji wa madini mkoani Kagera na Mratibu wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) Kanda ya Ziwa akichangia mada wakati wa mkutano mkuu wa kikatiba wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Naibu Katibu mpya wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Bi. Roshan Afzal akisisitiza jambo wakati wa mkutano mkuu wa kikatiba wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Na Mwandishi wetu, Dodoma
WANAWAKE wachimbaji madini nchini wamehamasishwa kujiunga na Chama cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) ili kupanua wigo wa sekta hiyo inayokua kwa kasi nchini.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko aliyewakilishwa na Kamisha wa Madini, Wizara ya Madini, Dkt. Abdul Rahman Mwanga wakati wa mkutano mkuu wa kikatiba wa TAWOMA uliofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.

“Tunafurahia ushiriki wa wanawake katika sekta hii na kwamba wameamua kuwa majasiri na kuingia katika eneo ambalo awali lilionekana kama kazi ya wanaume pekee,” alisema Dkt. Mwanga aliyekuwa mgeni rasmi na kuwataka wajumbe wa mkutano huo kujipanga zaidi kwani serikali imedhamiria kutatua changamoto zao.

Alitoa wito kwa chama kuendelea kushirikisha na kuwafundisha vijana kujihusisha na sekta ya madini aliyosema ina fursa nyingi zikiwemo uchimbaji, huduma, biashara na ushauri miongoni mwa nyingine.

Katika mkutano huo wa dharura, Dkt. Mwanga alizindua bodi ya wadhamini na katiba ya chama hicho. Wajumbe wa bodi hiyo ni pamoja na Dkt. Karim Baruti (Mwenyekiti), Dkt. Hawa Mshana, Bi. Hannah Kamau, Bi. Rita Kabati (Mbunge), wakili Ibrahim Shineni, Dkt. Winnie Samwel na Bi. Bupe Mwakan’gata (Mbunge).

Pia, wajumbe wa mkutano huo waliwachagua Bi. Semeni John Malale kama Mwenyekiti wa chama, Bi. Roshan Afzal kama Naibu Katibu Mkuu TAWOMA na waratibu wapya wa kanda tano nchini za chama hicho.

Akiongea kwa niaba ya wajumbe wa bodi wengine, Bw. Shineni aliwaambia waandishi wa habari kuwa ushauri na usimamizi wa bodi hiyo utasaidia chama kukua na kuwashirikisha wanawake wengi, kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania kuingia katika shughuli za madini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama, Bi. Salma Ernest alisema upatikanaji wa bodi mpya na viongozi wengine kutasaidia kuimarisha mikakati ya chama na kukipeleka ngazi nyingine ya maendeleo.

Wajumbe wa mkutano huo maalum walikubaliana kuanzisha SACCOS ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu, kufanya kongamano la miaka 25 ya TAWOMA mwezi Novemba mwaka huu litakaloendana na maonyesho kazi za wanachama pamoja na uhamasishaji wa ujenzi wa jengo la umahiri la chama hicho jijini Dodoma.

Mwenyekiti mpya, Bi. Semeni alisema ana lengo la kuwainua kina mama wachimbaji madini kuwa wachimbaji wa kisasa, wanaolipa kodi na kwa kufuata sheria za uchimbaji madini nchini. “Nahamasisha wanawake wengi kuchimba na kunufaika na rasilimali ya madini,” alisema.

Wajumbe wa mkutano walitoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.

TAWOMA ilianzishwa mwaka 1997 kwa malengo ya kuhamasisha wanawake wengi kuingia kwenye sekta ya madini na kuwakomboa kiuchumi kupitia elimu, mitaji na masoko. Chama kilianza na wanachama 22. Mpaka sasa kina wanachama zaidi ya 2,000 katika mikoa yote Tanzania bara.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad