HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 3, 2022

TCRA yaanza kufatilia Luninga na Mitandao vinavyotoa maudhui ya mapenzi ya jinsia moja

 

Mjumbe wa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)Jacob Tesha akizungumza na waandishi wa habari juu ya vituo vya Luninga na Mitandao ya kijamii vinavyotangaza maudhui ya mapenzi ya jinsia moja kufatiliwa, jijini Dar es Salaam.


*Yasema wanatoa onyo na hata vile vipindi vya katuni wanafuatilia kwa ukaribu

Na Chalila Kibuda, Michuzi TV
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema inaanza kufanya uchunguzi kwa vituo vyote vya luninga na mitandao ya kijamii vinavyorusha maudhui ya katuni zinazohamasisha mapenzi ya jinsia moja kwamba hayaendani na maadili ya Kitanzania.

Imesema watakapobaini kukiukwa kwa sheria, kanuni na maadili ya utangazaji kwa kurusha katuni hizo zinazotoka nje ya nchi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui,Habbi Gunze, Mjumbe wa kamati hiyo,Jacob Tesha alisema kamati imepewa mamlaka ya kufanya hivyo kwa mujibu wa kifungu cha 27(3)(a) cha Sheria ya TCRA.

Alisema pamoja na mambo mengine kamati hiyo ina jukumu la kusimamia maudhui yanayorushwa na vituo vya Utangazaji nchini.

"Siku za karibuni, kumekuwa na taarifa inayosambazwa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii yenye maudhui yanayohamasisha mapenzi ya jinsia moja kinyume na sheria, kanuni, maadili na miiko ya utangazaji nchini,"alisema Tesha.

Alieleza kuwa wanatambua ushawishi mkubwa uliopo kwa vyombo vya utangazaji ikiwemo mitandao ya kijamii, katika kuelimisha na habarisha jamii na kwamba madhara ya maudhui yasiyozingatia kanuni kwa jamii hususan vijana na watoto ambao ni sehemu kubwa ya wafuatiliaji wa vyombo hivyo ni makubwa.

"Kamati inaviagiza vyombo vyote vya utangazaji nchini ikiwemo mitandao ya kijamii kuzingatia matakwa ya sheria, kanuni na masharti ya leseni ya utangazaji kwa kuhakikisha vituo haviendi kinyume na misingi ya utangazaji hasa kuepuka kutangaza maudhui yasiyofaa kwa jamii na hususan watoto," alifafanua.

Alisema kamati hiyo inakemea vikali urushwaji na usambazaji wa maudhui hayo potofu na kuvitaka vyombo vya utangazaji pamoja na mitandao ya kijamii kuzingatia wajibu wao wa ulinzi wa taifa dhidi ya maudhui hasi na yasiyo na staha, yenye uwezekano wa kuharibu mila, desturi na utamadumi wa Taifa.

Aidha, alisema ni wajibu wa jamii nzima ikiwemo wazazi, walezi, viongozi wa dini na walimu ambao watoto hutumia muda mwingi wakiwa masomoni, kuhakikisha wanalinda watoto dhidi ya maudhui yasiyofaa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad