HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 29, 2022

RITA yasajili na kutoa Vyeti kwa watoto zaidi ya laki mbili Manyara

Na John Walter-Manyara
Mkuu wa mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere amewataka wananchi kujitokeza kuwaandikisha watoto wao wenye umri chini ya miaka mitano kupata vyeti vya kuzaliwa.
Makongoro ametoa kauli hiyo katika kikao cha Tathmini kuhusu utekelezaji wa mpango wa usajili wa vizazi kwa watoto wa umri chini ya Miaka Mitano mkoani Manyara, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano mkoani hapo.
Amesema Idadi ya watoto waliosajiliwa katika mkoa wa Manyara imeongezeka kutoka asilimia 6.3 na kufikia asilimia 80.2.
Mpaka sasa mpango wa usajili wa watoto unatekelezwa katika mikoa 23 ya Tanzania bara na zaidi ya watoto milioni 7.5 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa ambapo idadi hiyo imewezesha kuongeza kiwango cha usajili wa watoto kutoka 13% mwaka 2012 na kufikia 65% mwaka 2021.
Naye Katibu Mkuu wizara ya katiba na Sheria Mary Makondo amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuleta maboresho ya mfumo wa usajili kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu ambazo ni Vizazi, Vifo, Ndoa, Talaka na Watoto wa Kuasili.
Aidha ameziagiza Halmashauri zote za mkoa wa Manyara ambazo ndio zinataratibu usajili katika maeneo yao,kuanza kutenga fedha katika bajeti zao ili kuendeleza utekelezaji wa mpango huo kwa kuwa jukumu la usajili kwa sasa lipo juu yao kwa mujibu wa sheria.
Ameeleza kuwa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano ni uthibitisho wa sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha watoto wanasajiliwa na kupata nyaraka ya awali na ya msingi ya utambulisho ambayo ni cheti cha kuzaliwa.
Aidha ameahidi,wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano kila itakapohitajika ili kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanadumishwa kwa kuendeleza upatikanaji wa huduma.
Makondo, Kwa niaba ya serikali amewashukuru wadau wa maendeleo ambao ni shirika la umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto duniani (UNICEF),Serikali ya Canada na kampuni ya simu za mkononi ya TIGO kwa kuendelea kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.
Akizungumza katika kikao hicho cha Tathmini, Kabidhi Wasii mkuu na afisa mtendaji mkuu wa wakala wa Usajili,Ufilisi na udhamini (RITA) Angela Anatory, amesema mpango huo ulianza mwezi mei 2021.
Kwa mujibu wa takwimu,tangu mpango wa usajili ulipoanza kutekelezwa katika mkoa wa Manyara,zaidi ya watoto 259,317 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa sawa na asilimi 80.2 ya lengo ambapo kabla ya kuanza mpango huo ni asilimia 6.3 tu ya watoto walikuwa wamesajiliwa na kupata vyeti, hivyo kuna ongezeko la asilimia 73.9.
Amesema utekelezaji wa mpango huo umeleta maboresho makubwa katika mfumo wa usajili wa vizazi na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto kwani kwa sasa huduma zinapatikana katika ofisi zote za watendaji kata na vituo vya tiba.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad