HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 21, 2022

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AELEKEZA WANAWAKE KUJENGEWA UWEZO WA KUSHIKA NAFASI ZA MAAMUZI SERIKALINI

 

Na. James K. Mwanamyoto-Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemuelekeza kuhakikisha wanawake katika Utumishi wa Umma wanajengewa uwezo kiutendaji ili waweze kushika nafasi za uongozi na kufanya maamuzi kwa maendeleo ya taifa.

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dar es Salaam, wakati akizindua programu ya wanawake na uongozi katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.

Mhe. Jenista amesema, alimueleza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan juu ya uzinduzi wa programu ya wanawake na uongozi, hivyo miongoni mwa maagizo aliyompatia ni kuhakikisha wanawake wanajengewa uwezo wa kiutendaji kupitia Taasisi ya UONGOZI ili wawe na uwezo wa kushika nafasi za maamuzi.

Waziri Jenista amesema kwa asili, wanawake wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja, kwa ufanisi na ni waaminifu, hivyo wakipewa mafunzo na nafasi za uongozi watatekeleza majukumu yao kikamilifu.

“Kama wanawake wengi wamefanikiwa kuongoza makampuni na taasisi za umma na zikafanya vizuri, ina maana tukiwa na wanawake wengi katika nafasi za uongozi ni wazi kuwa taifa litapiga hatua kubwa katika maendeleo,” Mhe. Jenista amefafanua.

Ameongeza kuwa ni lazima kuwa na mipango ya kuwaibua wanawake wenye uwezo na kuwajengea hali ya kujiamini ili kuwa tayari kulitumikia taifa kwa bidii na uzalendo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo amesema Mhe. Samia Suluhu Hassan kutokana na utashi wa kisiasa alionao ameonesha dhamira ya dhati ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji wanawake kuwa viongozi na ndio maana taasisi yake imeanzisha programu ya kuwajengea uwezo wanawake ili kufikia ndoto ya Mhe. Rais na kuongeza kuwa, ni jukumu la wanawake kujitokeza ili kupata mafunzo.

Naye mshiriki wa programu hiyo ya wanawake na uongozi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Bi. Sharifa Nabalang’anya amesema, viongozi wanawake wanao wajibu wa kujifunza kupitia utendaji kazi wa Mhe. Rais na mafunzo wanayopatiwa na Taasisi ya UONGOZI ili wawe na mchango katika maendeleo ya taifa.

Programu hiyo ya Wanawake na Uongozi inayohudhuriwa na washiriki 50 kutoka katika taasisi za umma, inaratibiwa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Serikali ya Finland na Umoja wa Mataifa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizindua Programu ya Wanawake na Uongozi inayoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Serikali ya Finland na Umoja wa Mataifa inayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya washiriki wa Programu ya Wanawake na Uongozi inayoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Serikali ya Finland na Umoja wa Mataifa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati akizindua programu hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akielezea maudhui ya Programu ya Wanawake na Uongozi inayoratibiwa na taasisi yake kwa kushirikiana na Serikali ya Finland na Umoja wa Mataifa kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzindua programu hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Riitta Swan akitoa salamu za nchi yake kuhusu umuhimu wa Programu ya Wanawake na Uongozi inayoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Serikali ya Finland na Umoja wa Mataifa kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzindua programu hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya wanawake nchini, Bi. Hodan Addou, akitoa salamu za Umoja wa Mataifa kuhusiana na Programu ya Wanawake na Uongozi kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kuzindua programu hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Programu ya Wanawake na Uongozi inayoratibiwa na Taasisi ya UONGOZI kwa kushirikiana na Serikali ya Finland na Umoja wa Mataifa inayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad