HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, June 21, 2022

MWENGE WAZINDUA MRADI WA MAZINGIRA MGUTWA SEKONDARI

 


MWENGE wa uhuru umezindua mradi wa kuhifadhi mazingira wa shule ya sekondari Mgutwa iliyopo Kata ya Shambarai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wa thamani ya shilingi 18,210,000.

Mkuu wa shule ya sekondari Mgutwa Donald Lema akisoma taarifa ya mradi huo kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu Sahili Nyanzabara Geraruma, amesema mradi huo una miti 2,150 iliyopandwa.

Mwalimu Lema amesema matarajio yao kwa mwaka huu ni kupanda miti ya matunda 350.

"Mradi unaendelea vizuri na mafanikio yaliyopatikana ni kurejea kwa uoto katika eneo la shule, upatikanaji wa kiviuli na kufanya shule kuwa na mandhari nzuri zaidi ya kujisomea na upatikanaji wa matunda kwa ajili ya wanafunzi," amesema mwalimu Lema.

Amesema wanaamini mradi huo unachangia katika kupunguza kiasi cha hewa ya ukaa kilichopo angani na kufanya eneo hilo kuwa mahalo pazuri zaidi kwa maisha ya binadamu na viumbe wengine hai.

Amesema hiyo ina wanafunzi 131 wasichana 63 na wavulana 68 na walimu saba.

Amesema shule hiyo ilitembelewa na mwenge wa uhuru mwaka jana na kuona mradi huo upandaji miti na utunzaji mazingira.
"Lengo la mradi ni kutunza mazingira ya shule na kuchangia juhudi za Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi," amesema mwalimu Lema.

Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu, Sahili Nyanzabara Geraruma ameipongeza shule ya sekondari Mgutwa kwa kufanikisha mradi huo wa kuhifadhi mazingira.

"Nawapongeza kwa mradi mzuri ila mnapaswa kuutunza na hii miti tuliyoipanda mimi na wakimbiza mwenge wenzangu wa kitaifa hakikisheni mnaitunza," amesema Geraruma.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dk Suleiman Serera amesema ukiwa wilayani humo  mwenge utatembelea miradi sita ya thamani ya shilingi bilioni 1.3.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad