Na Amiri Kilagalila, Njombe
MUUZA wa nyama ya kuchoma (Mishkaki), Mbaraka Madege katika mtaa wa Kibedange halmashauri ya mji wa Makambako mkoani Njombe amechomwa na kisu shingoni kwa kosa la kumdai shilingi elfu moja mteja wake.
Akizungumza kwa shida huku akiuguza jeraha lake bwana Madege amesema amechomwa na kisu na mteja wake Oswadi Kihombo aliyekuwa amefika katika eneo lake la kuuzia nyama mara baada ya kukataliwa kupewa nyama baada ya kukopa kutokana na kudaiwa kiasi cha shilingi elfu moja ya nyama ya awali.
"Alifika kwangu akakopa nyama nikamkatalia kwa kuwa ninamdai elfu moja nyingine,akanivamia tukio lilikuwa ndio hilo ila kwa sasa naendelea vizuri japo shingo inanisumbua"alisema Madege
Rajabu Shayo ni mwenyekiti wa mtaa wa Kibedange amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika mtaa wake na kufafanua kuwa aliweza kufika katika hospitali na kukuta kijana huyo akiendelea kupata matibabu huku mtuhumiwa akiwa tayari ameshikiliwa na jeshi la polisi kituo cha Makambako.
"Nilienda hospitali nikakuta yule mtu anaendelea kuhudumiwa lakini huyu aliyejeruhi alikuwa tayari ameshakamatwa yuko ndani,kwa kweli kama mtu anayetembea na silaha ina maana huyu mtu ni mbaya angemkosa huyu ina maana angemchoma hata mtu mwingine ila niwaambie tu wananchi kuwa dawa ya deni ni kulipa"alisema Shayo
No comments:
Post a Comment