Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ameagiza Mashirika
ambayo Serikali ina hisa kuhakikisha yanaanza kutoa Gawio kwa serikali
mara moja, pia Taasisi zinazotakiwa kutoa asilimia 15 ya mapato ghafi
kwa mujibu wa sheria zifanye hivyo kikamilifu na kwa wakati.
Makamu
wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya kupokea Gawio la shilingi
bilioni 30.7 kutoka kwa Benki ya NMB iliofanyika katika Ukumbi wa Hazina
Jijini Dodoma leo tarehe 15 Juni 2022. Amesema Mashirika ambayo
yanategemea ruzuku kutoka mfuko mkuu wa Serikali yanapaswa kuwa na
mikakati madhubuti na inayotekelezeka ya kupunguza utegemezi kwa
Serikali na kumuagiza msajili wa Hazina kuhakikisha wakuu wa taasisi
husika wanatekeleza maagizo hayo.
Aidha Makamu wa Rais amesema
Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira
rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha na sekta
zote nchini. Pia ameipongeza Benki ya NMB kwa kuendelea kuchangia
maendeleo ya jamii nchini (corporate social responsibility) sambamba na
kusaidia ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuimarisha mifumo ya
ukusanyaji mapato. Amewaasa kuendelea kushirikiana na Serikali katika
kuongeza fursa za ajira kwa vijana na wanawake pamoja na kuboresha
huduma za kijamii kwenye sekta mbalimbali kama afya,elimu na utunzaji wa
mazingira ikiwa ni pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi na tabiawatu.
Kwa Upande wake Waziri wa Fedha na
Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Wizara itaendelea
kusimamia maelekezo ya kuhakikisha taasisi za serikali na zile ambazo
serikali ina hisa zinatoa Gawio. Aidha amesema serikali itaendelea
kushirikiana na taasisi zote za sekta binafsi ili kuweza kuhakikisha
zinafanya kazi vizuri.
Awali Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB
Ruth Zaipuna amesema Gawio la Serikali kutoka Benki ya NMB limeendelea
kukua kila mwaka na kuwa endelevu mpaka kufikia bilioni 30.7 kwa mwaka
2022 kutoka bilioni 10.48 mwaka 2018. Amesema adhma ya NMB ni kuleta
tija kwa wawekezaji ikiwemo serikali ambayo inamiliki hisa za asilimia
31.8.
Aidha Bi Zaipuna ameongeza kwamba Benki ya NMB itaendelea
kuwa mdau mkubwa wa serikali katika kufanikisha maendeleo ya kijamii na
kiuchumi hasa kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo na biashara.
Amesema mpaka mwezi Desemba 2021 jumla ya mikopo ya shilingi Trilioni
4.3 imetolewa kwa wakulima na wafanyabiashara.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akipokea mfano wa hundi ya shilingi shilingi bilioni 30.7 ambayo ni Gawio la Serikali kutoka Benki ya NMB katika hafla iliofanyika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo tarehe 15 Juni 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na viongozi wa Serikali,viongozi wa Benki ya NMB pamoja na watumishi wa Benki hiyo wakati wa Hafla ya kupokea Gawio la Serikali la shilingi bilioni 30.7 kutoka Benki ya NMB iliofanyika katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma leo tarehe 15 Juni 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwasili katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma wakati wa Hafla ya kupokea Gawio la Serikali la shilingi bilioni 30.7 kutoka Benki ya NMB leo tarehe 15 Juni 2022.
No comments:
Post a Comment