Mkurugenzi
wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,) Lilian Liundi akizungumza wakati
wa mjadala wa bajeti ya fedha ya Taifa kwa mwaka 2022/2023 na kueleza
kuwa jitihada zaidi zinahitajika katika sekta ya kilimo ambayo ushiriki
wa wanawake ni mkubwa lakini ukuaji wake umekuwa mdogo, Leo jijini Dar
es Salaam.
· Wanawake Kishapu walia na changamoto ya Maji
MTANDAO
wa Jinsia Tanzania (TGNP,) umeendelea kuamini katika nguvu ya pamoja
kwa kukutana na wadau na wanachama wa mtanda huo na kufuatilia mgawanyo
wa rasilimali kwa kupitia bajeti kwa jicho la kijinsia.
Akizungumza
wakati wa tafakari ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia jukwaa
la Kijiwe cha Kahawa Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP,)
Lilian Liundi amesema kuwa jukwaa hilo litawasaidia wanajamii na wadau
wa maendeleo kutambua fursa na vipaumbele vilivyoainishwa katika bajeti
pamoja na mapungufu ya kijinsia yaliyopo katika bajeti ya mwaka husika
na kutoa mapendekezo kwa watunga sera na wahusika kuboresha zaidi ili
kuwa na bajeti yenye kujenga uchumi na maendeleo endelevu kwa taifa.
Lilian
amesema kuwa, bado kuna changamoto katika sekta za maji na kilimo
katika bajeti ya mrengo wa kijinsia na takwimu zimekuwa zikiangalia
changamoto hizo kwa maeneo ya mjini pekee na kuishauri Serikali kuu kwa
kushirikiana na Serikali za mitaa kupitia Sensa ya watu na makazi
inayokwenda kufanyika ilete takwimu sahihi ya wananchi, mahitaji yao
pamoja na mgawanyo wa rasilimali kwa mrengo wa kijinsia.
Amesema
katika sekta ya kilimo ambayo ina uhakika wa chakula na ushiriki wengi
wa wanawake ukuaji wake ni kati ya asilimia 3 hadi 5 na bado uwekezaji
wake hauna mkazo na kushauri maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Rais
Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake ya kwanza Bungeni juu ya kutumia
malighafi za viwandani kutoka kwa wakulima wazawa litiliwe mkazo ili
kujenga uchumi shindani kwa maendeleo endelevu.
Mwanamtandao wa
TGNP kutoka Kishapu, Shinyanga Bi. Fregina Said katika kueleza
changamoto wanazokumbana nazo akina Mama kujenga uchumi wa taifa kwa
mrengo wa kijinsia amesema, upatikanaji wa maji safi na salama bado
imeendelea kuwa kikwazo kwa wanawake katika kushiriki katika shughuli za
kiuchumi katika Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Amesema
kuwa Kata nyingi wilayani humo nyingi zimepitiwa na mradi mkubwa wa
maji kutoka Ziwa Viktoria ila bado hazijafikiwa na huduma hiyo kutokana
na gharama ambazo wananchi hawawezi kuzimudu.
‘’Mimi natoka Kata
ya Kiloleni kuna kata nyingi ambazo nyingine hazifanyi kazi na TGNP ila
zina changamoto kubwa ya maji kuna Kata nyingi hazijapata huduma ya
maji licha ya kupitiwa na mradi huo mkubwa…Gharama za kuunganishiwa maji
zimefikia hadi shilingi laki mbili na themanini na unit moja inalipiwa
shilingi elfu mbili kiasi ambacho mwanamke wa kijijini hawezi
kukimudu.’’ Amesema.
Ameeleza kuwa katika harakati za kumtua
Mama ndoo kichwani Serikali kupitia bajeti lazima iangalie namna bora ya
kutatua changamoto za umbali na gharama ili wanawake ambao ndio
wazalishaji wakubwa wajikite katika shughuli za uzalishaji mali.
‘’Baadhi
ya Kata zinafuata maji kwa umbali wa Kilomita 15 na maji hayo sio
salama na katika harakati hizo hukumbana na unyanyasaji wa kijinsia,
mimba za mapema na hata kwa utoro kwa mabinti kutokana na hedhi na
shuleni hakuna taulo wala maji ya kuwasitiri.’’ Amesema.
Raheli
Misesi kutoka Kishapu, Shinyanga ameeleza katika sekta ya kilimo ambayo
wanawake wanashiriki kwa asilimia 80 ni vyema Serikali ikaweka mkazo na
juhudi mahususi katika kuboresha kilimo cha umwagiliaji hasa kwa
wakulima wadogo vijijini.
‘’Kwa Wilaya ya Kishapu kwa mwaka huu
kumekuwa na ukame hakuna mazao kwa sasa debe moja la mahindi linauzwa
shilingi elfu kumi na nne hiki ni kiashiria kikubwa cha njaa ni vyema
Serikali ikaweka juhudi kwa kuboresha kilimo cha umwagiliaji pamoja na
teknolojia za kilimo ikiwemo matumizi ya trekta kwa wakulima wadogo na
hiyo ni pamoja na kufanya tafiti kwa mbegu na mbolea za asili ambazo
zinafanya vizuri katika ukuaji wa mazao.’’ Amesema.
Aidha
amesema kuwa katika kuhakikisha bajeti inakuwa katika mrengo wa kijinsia
wametembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuzungumza na
wanawake na akina baba vinara kuhusu changamoto hizo na kushauri namna
ya kuongeza bajeti kama TGNP wanavyofanya.
Kuhusiana na sekta ya
afya ameishukuru Serikali kwa jitihada za ujenzi wa vituo vya afya na
kuiomba kuelekeza nguvu zaidi kwa kupeleka wahudumu wa kutosha pamoja na
vifaa tiba.
Jukwaa hilo lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP,) umewakutanisha wananchi, wanajamii, wachambuzi,
wanasiasa na wanachama wa mtandao huo na kusikiliza kwa pamoja
uwasilishwaji wa bajeti ya Taifa na kutafakari na kujadili kwa mrengo wa
kijinsia kwa namna ambavyo bajeti kuu imeakisi kupitia sauti za
wanajamii.
Afisa Kiongozi wa Programu kutoka TGNP Bi. Joyce Mkina akiwasilisha mada katika jukwaa hilo.
Mtafiti wa masuala ya bajeti na mwanachama ya TGNP Edward Mhina akiwasilisha mada katika jukwaa hilo.
Mhandisi
Wilhelma Malima kutoka shirika la Sanitation and Water Action (SAWA,)
akichangia mada katika jukwaa la Kijiwe cha Kahawa maalumu kwa bajeti ya
fedha ya mwaka 2022/2023.
Matukio mbalimbali wakati wa mjadala huo.
No comments:
Post a Comment