HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, June 18, 2022

DKT. STERGOMENA AFUNGA KOZI YA UKAMANDA NA UNADHIMU, ASTASHADA NA SHAHADA


Wahimu wa Kozi ya Ukamanda na Unadhimu Duluti Wakiwa Kaika Maandamano Kuelekea Eneo la Ukumbi Chuoni hapo Wakati wa Mahafali.

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) ameongoza mahafali ya kufunga kozi ya Ukamanda na Unadhimu na Astashahada na Shahada ya Uzamili ya Mafunzo ya Ulinzi na Usalama yaliyofanyika katika Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (Command and Staff College) - Duluti.

Wahitimu hao wanatokana na Kozi tatu zinajumuisha maafisa wakuu 67, maafisa 51 kutoka Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania na wanafunzi 16 kutoka majeshi ya nchi rafiki za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Ambapo maafisa wawili wawili kutoka nchi za Burundi, Kenya, Malawi, Rwanda na Uganda. Mwanafunzi mmoja moja kutoka nchi za Bangladesh, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Misri, Falme za Eswatini, Msumbiji, na Njgeria.

Akihutubia maafisa wahitimu hao, Mheshimiwa Waziri aliwapongeza wahitimu hao kwa kufuzu kozi ya Ukamanda na Unadhimu, kujituma na kufanya kazi kwa bidii na katika mazingira magumu. “naomba niwapongeze sana nyote mnaohitimu leo na kufanikiwa kutunukiwa alama ya psc yaani passed staff college. Tuzo hii ni matokeo ya jitihada zenu na kazi kubwa mliyofanya kwa muda wa wiki 48, kipindi ambacho mlikuwa mkipata mafunzo ya kina kwa nadharia na vitendo”, alisema.

Aidha, Mheshimiwa Dkt. Stergomena aliwapongeza Timu ya Wakufunzi kutoka India, wakufunzi na wahadhiri wote kwa kufanikikisha wahitimu hao kufuzu mafunzo hayo. “Naomba pia niwapongeze wakufunzi na wahadhiri ambao kwa kipindi chote wamejituma na kutumia weledi wao kuhakikisha kuwa wahitimu wanapata elimu stahiki”, aliongeza. Elimu inayotolewa hapa, imelenga sio tu kuwaandaa wahitimu kutekeleza majukumu yao ya kawaida ya kila siku, lakini pia kuzikabili kwa ustadi na ufanisi changamoto mbalimbali mtakazokumbana nazo wakati wa amani na wakati wa vita, ikiwa ni sehemu ya kulinda amani na maslahi mapana ya Taifa”, aliongeza.

Mhe. Waziri alibainisha kuwa lengo mahsusi la vyuo vya ukamanda na unadhimu popote duniani, ni kuwajengea uwezo wa kujiamini na kuwapa weledi makamanda, maafisa wanadhimu na welekezi, hivyo Chuo hiki cha Ukamanda na unadhimu – Duluti si tofauti na hakina chaguo bali ni kutekeleza azima hiyo. Ni jambo la kujivunia kuwa, Chuo kimeendelea kutekeleza lengo hili.

Aidha, amewakumbusha viongozi wa Chuo kuwa pamoja na kazi kubwa wanayoendelea kuifanya na mafanikio waliyoyapata, wakumbuke azima ya JWTZ , ambayo ni kuwa na jeshi dogo la kisasa, lenye weledi na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kiulinzi na kiusalama zilizopo na zinazoweza kujitokeza. Kama sehemu ya ya JWTZ, kinao wajibu wa kutayarisha makamanda na maafisa wanadhimu wanaoendana na azima hii.

Mheshimiwa Dkt. Stergomena pia, alikumbusha kuwa “Dunia kwa sasa inakabiliwa na na mabadiliko makubwa katika nyanja zote. Mabadiliko yaliyoleta mahitaji mapya ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kijeshi, na hatuwezi kujitenga mna mabadiliko hayo. Pamoja na fursa zitakanazo na mabadiliko haya, mabadiliko haya yamepelekea pia mahitaji mapya na changamoto za kiusalama kitaifa, kikakanda na kidunia”, alikumbusha.

Vile vile, Mheshimiwa Waziri aliwatoa wasiwasi kuwa “Serikali inatambua kuwa, ili kutekeleza majukumu kwa ufanisi, Chuo cha Ukamnda na Unadhimu kinahitaji rasilimali ikiwa ni pamoja na rasilimali watu, rasilimali fedha, na vitendea kazi. Pamoja na changamoto mbalimbali, mnazokabiliana nazo, kama kama ilivyo kwa vyuo vingine nchini, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan itaendelea kukidhi mahitaji ya msingi kadri hali itakavyoruhusu”, alisema.

Akiwaasa wahitimu kutoka majeshi rafiki, Mheshimiwa Tax aliwapongeza kwa “nawapongeza kwa kuhitumu kozi hii hapa Tanzania, natambua kuwa, kwa muda mliokuwa hapa mmemkutana na changamoto mbalimbali, hata hivyo, ni matumaini yangu kuwa mmejitahidi kukabiliana nazo, na hii inatokana na nidhamu binafsi na ukomavu mlionao. Wakati huu mnatarajia kurejea nyumbani, nawaasa kuendelea kuwa waaminifu kwa nchi zenu, ni imani yangu kuwa mtatumia elimu mliyoipata kwa manufaa ya nchi zenu. Vile vile, mkumbuke kuwa, ninyi ni mabalozi wa Chuo popote mtakapokuwa, tunatarajia mtaitangaza vema taswira nzuri ya Chuo”, aliasa.

Akitoa taarifa ya chuo kwa Mheshimiwa Waziri, Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu Brigedia Jenerali Sylvester Damian Ghuliku, amesema Kozi ya Ukamanda na Unadhimu Kundi la 36/21-22 imeendeshwa sambamba na Astashahada na Shahada ya uzamili ya mafunzo ya Ulinzi na usalama (Diploma and Masters of Arts in Defence Studies) yaliyodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja. Mafunzo hayo yameendeshwa na Chuo baada ya kutambuliwa na kupewa ithibati na Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (National Council for Technical and Vocational Education and Trainnng - NACTEVET).

Mahafali hayo yalihudhuriwa pia, na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule, Wajumbe Wa Bodi inayosimamia uendeshaji wa chuo (SCCB), Wakuu wa Vyuo vya Ukamanda na Unadhimu vya Karen – Kenya, Kimaka - Uganda na Msumbiji, Wakuu wa Matawi na Wakurugenzi kutoka Makao Makuu ya Jeshi, Mkuu wa Kanda ya Arusha, Wakuu wa Vyuo, Shule na Makamanda Vikosi Kanda ya Arusha, Waambata Jeshi kutoka Majeshi ya Nchi Rafiki, Timu ya Wakufunzi kutoka Jeshi la India, Wahadhiri wa Astashahada na Shahada ya Uzamili, Maafisa Wakuu, Maafisa wadogo, Askari, waandishi wa Habari na familia za wahitimu.
Mgeni Rasmi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax Akitoa Zawadi kwa mmoja wa Wahitimu wa Kozi ya Ukamanda na Unadhimu Chuo Kilichopo Duluti Jijini Arusha.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax akizungumza na Wahimu wa Kozi ya Ukamanda na Unadhimu Duluti.


Picha ya Pamoja, Mgeni Rasmi Waziri wa Ulinzi na JKT, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Majenerali, Wahitimu pamoja na Wakufunzi Wakiwa mbele ya Jengo Kuu Katika Chuo Cha Ukamanda na Unadhimu Duluti Jijini Arusha.Wahimu wa Kozi ya Ukamanda na Unadhimu Duluti Wakifuatilia Hotuba ya Mgeni Rasmi Chuoni hapo Wakati wa Mahafali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad