HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 16, 2022

Shule za sekondari mkoa wa Njombe zapatiwa msaada wa taulo za kike

 Meneja mkuu wa kampuni ya Mtewele Traders Sady Mwang'onda akizungumza lengo la kukabidhi taulo za kike wa wanafunzi.Na Amiri Kilagalila,Njombe

SHULE za sekondari za serikali zipatazo 18 mkoani Njombe zimepatiwa msaada wa katoni 2600 za taulo za kike ambazo thamani yake ni zaidi ya shilingi 83 milioni ili kuwasaidia wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakikosa masomo kwasababu ya hedhi.

Akizungumza wakati wa kukabidhi taulo hizo kwenye hafla iliyofanyika katika shule ya sekondari Mpechi meneja mkuu wa kampuni ya Mtewele Traders Sady Mwang'onda alisema kampuni hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Rospa International iliyopo nchini Japan wameamua kutoa taulo hizo ili kuwasaidia wanafunzi wa kike katika shule za sekondari ambao wamekuwa wakikosa masomo kutokana na hedhi.

Amesema mtoto wa kike anapokuwa katika hedhi anaweza kukumbana na changamoto ya kukosa au kutoshiriki vema kwenye masomo yake kati ya siku tatu hadi tano kwa mwezi ambapo kwa mwaka mzima anakuwa amekosa masomo kati ya siku 36 hadi 60.

Amesema kwa kuona ukubwa wa tatizo hilo kampuni hiyo imeamua kuunga mkono jitihada za serikali kutoa taulo za kike kwa shule hizo za sekondari za serikali mkoani Njombe ili wanafunzi hao wafanye vizuri kwenye masomo yao.

Alisema kitendo kilichofanyika cha kutoa taulo hizo za kike ni moja ya kurudisha fadhila kwa jamii kutokana na shughuli ambazo kampuni hiyo inafanya ya uuzaji wa pembejeo za kilimo.

"Tukio hili la leo ni kubwa kwasababu linakwenda kugusa maisha ya kila mwanafunzi wakike ambaye anasoma shule za sekondari za mkoa wa Njombe" alisema Mwang'onda.

Afisa tarafa wilaya ya Njombe mjini Lilian Nyemele kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Njombe alisema kupatikana kwa taulo hizo kunapaswa kuwafanya wanafunzi wanafunzi kuongeza bidii kwenye masomo kwakuwa changamoto ya hedhi inapungua siku hadi siku.

Alisema kwa kuzingatia uwepo wa wanafunzi wa kike katika shule mbalimbali serikali imeendelea kuboresha miundo mbinu ili kupunguza changamoto ambazo wanakutana nazo wakiwa shuleni.

'Tusome kwa bidii tuache visingizio maana saa nyingine huumwi tumbo la hedhi lakini unasongizia kisa umeona somo la hesabu

Mwakilishi wa afisa elimu sekondari halmashauri ya mji Njombe Augusta Wellah alisema wanafunzi wapo wa makundi mbalimbali wanaoweza na kutumia taulo za kike na wengine ambao hawana uwezo kabisa.

Aliishukuru kampuni hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwasaidia watoto wakike wanaosoma katika shule za sekondari mkoani hapa.

"Serikali ina shule nyingi zenye wasichana wengi kwenye maeneo mbalimbali lakini wameona waiunge mkono serikali kwa kuwapatia hawa watoto taulo za kike tunawapongeza na kuwashukuru sana" alisema Augusta.

Baadhi ya wanafunzi wa kike waliopatiwa msaada huo wa taulo za kike kutoka shule za sekondari Mpechi na Viziwi zilizopo mkoani Njombe Lusiana Mgani na Asunta Mwesongo walisema changamoto za maisha zimekuwa zikiwasababisha baadhi yao kukosa masomo kutokana na ukosefu wa fedha za kununulia taulo za kike.

"Tumetoka kwenye familia tofauti na zipo ambazo hazina uwezo hivyo wanalazimika kukosa vipindi darasani kwasababu ya kukosa taulo za kike" alisema Lusiana.

Wanafunzi wa mpechi sekondari kwa niaba ya wanafunzi wengine wa shule za sekondari wakipokea taulo za kike katika uwanja wa shule hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad