HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 5, 2022

SERIKALI YATANGAZA MSAMAHA WA RIBA KWA WAAJIRI

 

 Baadhi ya Watumishi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wakifuatilia matukio mbalimbali katika mkutano huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
SERIKALI imetangaza msamaha wa riba kwa waajiri wote nchini waliochelewa kuwasilisha michango katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuanzia Oktoba mosi, 2017 hadi Agosti 31, 2021.

Akitangaza msamaha huo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako amesema waajiri wote Tanzania Bara wanawajibika kuwasilisha michango ya Wafanyakazi hao katika mfuko huo kila mwezi kupitia kifungu 75 (5) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Sura 263).

Prof. Ndalichako amesema viwango vinavyopaswa kuchangiwa na Waajiri ni asilimia 0.5 (0.5%) ya mishahara ghafi kwa mwezi kwa Sekta ya Umma na asilimia 0.6 (0.6%) ya mshahara ghafi katika Sekta binafsi.

“Michango ya kila mwezi, inatakiwa kuwasilishwa katika mfuko ndani ya mwezi husika au kipindi cha mwezi unaofuata, michango hiyo huo inatozwa riba kisheria, tangu Julai 2015 hadi Agosti 2021, michango iliyochelewesha imetozwa riba ya asilimia 10 kwa mwezi, kuanzia Septemba 2021, riba hiyo imeshushwa kutoka asilimia 10 hadi asilimia mbili kwa mwezi”, amesema Prof. Ndalichako.

“Kufikia Agosti 2021, takribani Waajiri 13,468 wa Sekta binafsi na Waajiri 191 wa Sekta ya Umma wlikuwa kwenye orodha ya madeni ya riba”, amesema


Hata hivyo, Prof. Ndalichako amesema Serikali imeendelea kupokea maombi kutoka kwa Waajiri wakieleza kuwa kiwango cha awali cha riba (10%) kimezalisha asilimia kubwa ya malimbikizo ya madeni, kutokana na kuyumba kwa mwenendo wa Biashara na mtikisiko kwenye masuala ya Uchumi.

“Mhe. Rais Samia amesikia kilio cha Wafanyabiashara na kupunguza kiwango cha riba kutoka asilimia 10 hadi asilimia mbili, lakini yale malimbikizo ndio imebaki kilio cha Waajiri nchini”, amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma ameishukuru Serikali kukubali kutoa punguzo hilo na kurahisisha usimamizi na utakelezaji wa majukumu ya mfuko huo.

“Tunaishukuru Serikali na tunaamini msamaha huu utasaidia utekelezaji wa majukumu yetu kama Mfuko, pia kuhamasisha Waajiri nchini kuitikia kwa hiari”, amesema Dkt. Mduma.

Watakaonufaika na msamaha huo ni Waajiri wote waliolipa malimbikizo ya michango wanayodaiwa na mfuko isipokuwa hawajalipa riba na tayari wapo wameandika barua ya kuomba msamaha wa riba kwa michango iliyocheleweshwa, sanjari waajiri watakaolipa malimbikizo ya michango ya miezi ya nyuma wanayodaiwa na Mfuko kabla ya June 30, 2022.

Wengine ni waajiri kutoka Sekta ya Umma na binafsi ambao mpaka sasa hawajajisajili kwenye mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Waandishi wa Habari na Watumishi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wakati akitoa tamko la msamaha wa riba kwa Waajiri wote waliochelewa kuwasilisha michango katika Mfuko huo. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi za Mfuko huo jiji Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma akitoa neno la shukran kwa Serikali baada ya tamko hilo la msamaha wa riba kwa Waajiri wote waliochelewa kuwasilisha michango katika Mfuko huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad