HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, May 29, 2022

NSSF YAFIKISHA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU, WENYEWE WACHANGAMKIA FURSA KUJIUNGA

NA MWANDISHI WETU, MOROGORO

WANAFUNZI wa Chuo cha Mzumbe na Chuo cha Jordan  Mkoani Morogoro wamehamasika kujiunga na Mfuko wa NSSF kupitia Mpango wa Taifa  wa Sekta Isiyo Rasmi chini ya kampeni ya “Boom Vibes na NSSF” iliyotua mkoani Morogoro Mei 28, 2022.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanachuo hao,  Meneja wa Sekta Isiyo Rasmi, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bi. Rehema Chuma amewahakikishia kuwa hawatajutia uamuzi wa kujiunga na Mfuko huo kwani utawasaidia katika maisha yao ya sasa na baadaye.

“Ni muhimu wewe kama mwanachuo kuanza utamaduni wa kujiwekea akiba kupitia NSSF, ukianza kuweka akiba mapema itakuwezesha kuwa na akiba ya kutosha inayoweza kuwa mtaji wa biashara pindi utakapomaliza elimu yako.”

Alisema unapokuwa mwanachama wa NSSF unatakiwa kuhakikisha unachangia kiasi kisichopungua shilingi elfu ishirini (20,000/=) kila mwezi au zaidi na uwasilishaji michango ni rahisi kupitia mitandao ya simu na benki.

Alisema Hifadhi ya Jamii ipo makhususi kwa ajili ya kuikinga jamii dhidi ya majanga mbalimbali hasa yale yanayosababisha upungufu wa kipato katika jamii zetu.”

Akieleza zaidi  alisema  “NSSF inatoa huduma za Hifadhi ya Jamii kwa makundi mawili ya wanachama, kundi la kwanza ni lile la wanachama walioajiriwa katika sekta binafsi ambao kwa mujibu wa sheria wanachangia asilimia 20% ikijumuisha makato ya asilimia 10% kutoka kwenye mshahara wa mfanyakazi na asilimia 10% kutoka kwa mwajiri.” Alisisitiza Bi. Rehema Chuma na kuendelea..“Kundi la pili ni la wanachama kutoka sekta isiyo rasmi yani mtu binafsi aliyejiajiri mwenyewe na anachangia NSSF kuanzia kima cha chini cha shilingi elfu 20,000/=  kwa mwezi na ninyi wanafunzi mnaingia kwenye kundi hili,” alifafanua.

Aidha katika kampeni hiyo pia walikuwepo baadhi ya wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambao ni Mhe. Agness Hokororo, Mhe. Omar Ali Omar na Mhe. Noah Lembris ambapo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwakilishwa na Bw. Frank Kilimba.

Kwa upande wao wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walitumia nafasi hiyo kuweka msisitizo wa kujiwekea akiba kwa wanachuo hao kupitia NSSF kwani itawasaidia katika kutafuta mitaji mbalimbali ya kibiashara.

Kampeni hiyo ilipambwa na wasanii mbalimbali akiwemo msanii maarufu wa Bongo Fleva GNAKO ambaye aliwahi kuwa Mwnachama wa NSSF.

“Hata mimi nilikuwa mnufaika wa NSSF, kabla ya kuingia katika muziki nilikuwa nimeajiriwa Jijini Arusha, mwajiri wangu alikuwa ananikata sehemu ya mshahara wangu, kwa hakika nilikuwa sipendi kukatwa mshahara wangu lakini siku mkataba wangu wa kazi ulipomalizika niliamua kuendelea na harakati zangu za muziki ambapo nilichukua mafao yangu kutoka NSSF na yalinisaidia kulipia studio na hata video zangu za mwanzo,” alisema GNAKO.

 

Meneja wa Sekta Isiyo Rasmi, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),         Bi. Rehema Chuma.
Mhe. Omar Ali Omar, Mbunge wa Wete, Pemba
Mhe. Agness Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, Mtwara.
Mhe. Noah Lembris, Mbunge jimbo la Arumeru Magharibi.
Afisa Mkuu Sekta Isiyo Rasmi, NSSF, Bi. Asha Sadick akitoa maelezo jinsi kujaza fomu ya kujiunga uanachama wa NSSF kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Mwanachuo akiweka dole gumba kukamilisha fomu aliyojaza ya kujiunga na NSSF.
Baadhi ya wanachuo wakijaza fomu za kujiunga na NSSF.
Wanachuo wakifurahia burudani iliyokuwa ikitolewa na GNAKO.
Msanii wa Bongo Fleva, GNAKO akiburudisha na kutoa ushuhuda.


 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad