HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, May 29, 2022

MEMBE AFUNGUKA KURUDI KWAKE CCM

 

 
*Aeleza sababu zilizomsukuma, ampongeza na kumshukuru Rais Samia
*Nape amtaja jinsi alivyomsaidia safari yake ya siasa kutwaa jimbo
*Shaka aongoza mapokezi yake ya kishindo na kumkabidhi kadi


Na Mwandishi Wetu, Lindi
ALIYEKUWA mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kupitia Chama cha ACT Wazalendo ameeleza sababu zilizomfanya arejee CCM ikiwemo kuondoka kwa sababu ambayo ilimfanya atimkie upinzani.

Aidha amefungunguka jinsi alivyoumia kutokana na uamuzi wa kumwondolea uanachama wa CCM, Chama alichokulia huku akiahidi kufia ndani ya CCM.

Membe ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Serikali ya Awamu ya Nne, alirejea rasmi CCM jana kupokelewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, katika mkutano wa Hadhara wa Mbunge wa Mtama, Nape Nape Nnauye uliofanyika katika Kata ya Chipomda, Jimbo la Mtama mkoani Lindi, alisema kurejea kwake kunatokana na dhamira ya kukitumikia Chama hadi kufa.

Akizungumza katika mkutano huo, katika Kijiji cha Rondo, alisema Machi 30 hadi Aprili 1, mwaka huu aliitwa Dodoma, kwenye Mkutano wa Kamati Kuu ya Maadili na Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu, alipewa nafasi na Mwenyekiti wa CCM Taifa kuzungumza na wana CCM.

“Mama yetu, Rais wetu na Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa alinipa nafasi ya kuzungumza na wajumbe wa kamati kuu ya Chama Taifa. Nashukuru kwa kupewa nafasi ile na wajumbe waliliridhia kwa kauli moja nirejee CCM.

“Nimerejea CCM kwa sababu kuu mbili, sababu ya kwanza nilishauriwa na viongozi wa dini zote, nilishauriwa na viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya na Mkoa, nilishauriwa na marafiki zangu wote nirejee CCM, nilishauriwa na wana CCM.

“Kutokana na ushauri wote huo sikuwa na namna nyingine zaidi ya kutii, nimekubaliana na ushauri wa wote waliosema nirudi CCM na sasa nimerudi CCM,” amesema Membe wakati akitangaza kurejea tena kwenye Chama.

Amesema sababu ya pili ya kurudi kwenye Chama hicho inatokana na dhamira yake ya kukitumikia Chama Cha Mapinduzi hadi atakapokwenda kaburini. “Nilipoondolewa CCM nilisikitika sana, nilisonekana sana, na ninyi wananchi msikitika, mlisononekana.

“Sababu ambazo zilinifanya niondoke CCM haziko tena, narudi sababu zilizoniondoa CCM haziko tena. Nimerudi, namshukuru Mwenyekiti wa CCM na wajumbe wa Kamati Kuu kunirudisha. Nimerudi kwenye Chama ambacho nimezaliwa na kukulia, chama ambacho kimenisomesha.



“Hivyo niahidi sitaondoka tena, nitabakia CCM hadi mwisho wa uhai wangu. Kurudi kwangu CCM nitaendelea kukitumikia Chama changu na sasa nitaendelea kushirikiana na Mbunge wangu Nape Nnauye. Mwaka 2015 nilisema nitawaletea Nape na kweli nilimleta, hivyo sasa Mtama mtakuwa na wabunge wawili, Mbunge wetu Nape na mimi mbunge wa chini chini.”



NAPE

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mtama ambaye pia ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema baada ya Membe kuondoka kwenye Chama wananchi wengi walichukia, lakini aliwaomba wasichukie kwani kuna siku moja atarejea.

“Leo mwenyezi Mungu ameturudishia faraja la Londo, ameturejeshea furaha Chiponda. Mtama ni wastaarabu na hatuna shida tena, tuna imani kubwa na Membe, alinikabidhi kijiti na kuvaa viatu vyake, kulikuwa na mambo yaliyokwama huku nyuma kwa sababu za kisiasa, lakini Mama Samia amekuja ameziondoa,” alisema.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Mtama kushikamana, fitina ambazo ziliingia kati zimekwisha. “Membe amenipigania katika mambo mengi, nilipotaka ubunge Ubungo baada ya kuonekana fitna zimeingia katikati Membe aliamua kuchora ramani.

“Ndio maana safari yangu ya ubunge imekuwa nyepesi. Kaka Membe amenipigania sana na bahati nzuri amerudi CCM. Niseme tu Mungu ameamua ugomvi,” alsema.

SHAKA AMKABIDHI KADI

Akizungumza katika mkutano huo, Shaka alisema Memembe amerejedushwa katika Chama baada ya kufuatwa kwa utaratibu ikiwemo kujadiliwa na tawi lake kisha na vikao vya juu.

Shaka alisema Membe na wanachama wengine zaidi ya 1670 waliovuliwa uanachama ambao wamejadiliwa katika vikao na kurejeshewa uanachama, sasa wanaweza kukabidhiwa kadi zao katika matawi yao.

Shaka alisema kurejea kwa Membe ndani ya CCM kuendelee kuwa chachu ya kudumisha umoja na mshikamano hususan kwa wanaccm wa Jimbo la Mtama.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka HAMDU Shaka akimkabidhi ya CCM,aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha ACT Wazalendo, Bernard Membe aliyerejea CCM, katika Mkutano wa mbunge jimbo la Mtaka, Nape Nnauye katika Kijiji cha Rondo, Mtaka mkoani Lindi (Picha zote na Fahad Siraji wa CCM).
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha ACT Wazalendo, Bernard Membe anayebusu kadi ya CCM baada ya kukabidhiwa na Shaka katika Mkutano wa mbunge jimbo la Mtaka, Nape Nnauye katika Kijiji cha Rondo, Mtaka mkoani Lindi (Picha zote na Fahad Siraji wa CCM).
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka HAMDU Shaka akimkaribisha CCM, aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha ACT Wazalendo, Bernard Membe aliyerejea CCM, wakati wa Mkutano wa mbunge jimbo la Mtaka, Nape Nnauye katika Kijiji cha Rondo, Mtaka mkoani Lindi (Picha zote na Fahad Siraji wa CCM).
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akipokipokea Kadi za Wanachama zaid ya 1600 Walio rejesha kadi za Vyama Vya Upinzani katika Mkutano wa mbunge jimbo la Mtaka, Nape Nnauye katika Kijiji cha Rondo, Mtaka mkoani Lindi (Picha zote na Fahad Siraji wa CCM).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad