Ujumbe wa Maafisa Waandamizi
kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Malawi (MACRA) ukiongozwa na Mkurugenzi
Mkuu Daud Suleman umeihakikishia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuwa
inayo nia ya kushirikiana na Serikali ya Tanzania kufikisha huduma za
data zenye gharama nafuu na salama nchini Malawi.
Wakizungumza
na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania aliewakilishwa na
Kaimu wake Modestus Ndunguru kwenye ofisi za makao makuu ya TCRA jijini
Dar es salaam hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa MACRA alibainisha kuwa
huduma za data nchini Malawi ni rasilimali adimu hivyo wameazimia
kuondoa changamoto za mtandao hasa upatikanaji wa intaneti nchini mwao
kwa kushirikiana na Tanzania ili kufikisha huduma nafuu za data/intaneti
nchini Malawi.
“Lengo la ziara yetu ni kuona namna tunavyoweza
kushirikiana katika kuimarisha huduma za Mawasiliano nchini kwetu,
Malawi matumizi ya intaneti yapo kiwango cha chini na ni watu wachache
wanaofikiwa na huduma hizi” alibainisha Daud.
Ujumbe huo
ulibainisha kuwa ni kiasi cha takribani watu milioni kumi pekee ndio
wameunganishwa na huduma za mtandao wa intaneti, hivyo lengo la ziara
yao ni kujifunza na kwa kadri itakavyofaa kuona namna wanavyoweza
kuingia makubaliano na Tanzania kupitia taasisi zake za Mawasiliano ili
kufikisha huduma za Mawasiliano Malawi.
Huduma za Mkongo wa
Taifa wa Mawasiliano hadi sasa zinazifikia takribani nchi nane
zinazoizunguka Tanzania, ambapo hatua ya Malawi kuonyesha nia ya
kuhitaji huduma hiyo kunaongeza idadi ya nchi jirani kwa Tanzania
zinazofikishiwa huduma za Mawasiliano kupitia mkongo wa taifa wa
Mawasiliano hadi kufikia tisa.
Haya yanajiri wakati serikali
ikiwa tayari imebainisha kuboresha mbinu za kusambaza kwa haraka mkongo
wa Mawasiliano ikiwa ni pamoja na kupitisha nyaya za Mawasiliano kupitia
miundombinu ya Shirika la Ugavi wa Umeme TANESCO kwa mujibu wa Waziri
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Moses
Nnauye aliyebainisha haya wakati akiwasilisha bajeti ya wizara
anayoiongoza hivi karibuni.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa TCRA Modestus Ndunguru aliueleza ujumbe huo kuwa, TCRA ipo
tayari kuwapa ushirikiano stahiki ili kufanikisha azma hiyo ya kufikisha
huduma za data nchini Malawi kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania.
“Tayari
tunashirikiana na nchi kadhaa jirani katika Mawasiliano na bila shaka
suala hili litafanikiwa na tutaona nchi zetu hizi zikipiga hatua katika
sekta ya Mawasiliano” aliongeza Ndunguru.
Katika ziara hiyo
ambayo pia ililenga kujifunza masuala mtambuka ya Mawasiliano ujumbe huo
ulipata fursa ya kuwatembelea watoa huduma za Mawasiliano kadhaa
zikiwemo kampuni za simu na watoa huduma za data likiwemo shirika la
Mawasiliano Tanzania TTCL.
“Kwa kweli tumefurahia ziara yetu
imekuwa yenye mafanikio kwa kuwa tumejifunza mengi na kuona uwezekano wa
kuongeza ushirikiano baina yetu; tunakwenda nyumbani kubainisha
uchaguzi na kipaumbele chetu kwa kadri tulivyojifunza na kuona ili
turejee kukamilisha makubaliano ya ushirikiano huu muhimu” alinasbisha
Andrew ACN mratibu wa ziara hiyo.
Ujumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Malawi (MACRA)
ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu Daud Seleman (mwenye koti jeusi alieketi)
ukiwa katika Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) jijini Dar es salaam ulipowasili kwa ajili ya mazungumzo
yanayolenga kuipatia Malawi huduma za data kutoka Tanzania. PICHA NA
TCRA
Ujumbe wa Menejimenti ya Mamlaka ya Mawasiliano ya Malawi (MACRA)
katika mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Modestus Ndugu wakati
walipofika kwa ziara ya kujifunza na kudumisha ushirikiano. Malawi
imeonyesha nia ya kuunganishiwa huduma za mtandao/data kutoka Tanzania.
PICHA NA TCRA
Monday, May 23, 2022
MACRA Yabainisha Utayari kushirikiana na Tanzania kufikisha ‘Data’ Malawi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment