HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, April 7, 2022

WAZO LANGU : Uber, Bolt wawekewe mazingira rafiki kibiashara

 


Na Joseph Sabinus


WAKATI kukiwa na ongezeko la bei ya mafuta katika nchi nyingi Tanzania ikiwamo, huenda mitandao ya usafirishaji kama Uber, Bolt, Taxify na mingine, ikawa mkombozi zaidi kwa watumiaji wa teksi, bajaji na pikipiki maarufu (bodaboda) mijini.

Hii ni kwa kuwa tangu sekta hii ianze kutoa huduma zake katika miaka ya hivi karibuni, licha ya kurahisisha upatikanaji wa usafiri na kwa bei nafuu zaidi kwa watumiaji ukilinganisha na taxi, bajaji au bodaboda za kawaida, unafuu wake wa bei unafanya kuwapo kwa mzunguko wa kasi wa pesa na hivyo, kuongeza ajira na kuchangia pato la taifa kupitia kodi huku wengi wakizingatia kanuni na sheria za usalama barabarani.

Si hivyo tu, uwepo wa mitandao hii ya usafirishaji mijini unachangia juhudi za serikali kupambana na tatizo la upungufu wa ajira kwa kuwa, umesababisha vijana wengi kupata ajira ama kwa kuajiriwa, au kwa kujiajiri wenyewe.

Hata hivyo, watoa huduma hawa wa teksi mtandao wakati mwingine wamekuwa wakikumbana na mazingira yanayowajengea hofu na pengine kujiona wanaokaribia kuwa katika mazingira yasiyo rafiki ya uwekezaji katika tasnia hii.
Miongoni mwa mambo yanayoonekana kuwa kikwazo cha ufanisi kwa tasnia hii, ni baadhi ya watu wasio waungwana kufanya miito kisha kuzima simu zao hali inayowapa usumbufu na kuwatia hasara madereva wanaoitikia miito.

Lingine linaloweza kuwa kikwazo kwao, ni kile wanachodai kuwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kuingilia makubaliano baina ya mtandao na madereva ambao kimsingi, wengine ndio wamiliki wa vyombo wanavyotumia.

Kinachoonekana kuwatia hofu zaidi madereva, ni azima ya kuweka kikomo cha kiwango cha mgao kwa waendeshaji wa mitandao hiyo ya usafirishaji kama ilivyotangazwa na LATRA hivi karibuni kupitia mkurugenzi wake huku akisisitiza kuwa, tozo au gharama zozote zinapaswa kwenda sambamba na gharama za uendeshaji, jambo ambalo kwa upande mwingine ni sahihi.
Mmoja wa madereva wanaotoa huduma hizo Dar es Salaam, Said Abdallah, anasema:

“Amri kama hizo zinaingilia moja kwa moja uendeshaji wa biashara katika soko huru, lakini pia zinaingilia makubaliano kati ya waendeshaji na madereva walioingia mikataba hiyo kwa hiari.”

Kimsingi, LATRA inapaswa na ina haki ya kutimiza wajibu wake ukiwamo wa kusimamia na kudhibiti utoaji wa huduma za usafiri ardhini kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, iongeze juhudi kuwashirikisha wadau katika uamuzi wowote ili kuondoa manung’uniko na kuimarisha uwekezaji katika tasnia ya usafiri na usafirishaji nchi kavu.

Hii ni kusema kuwa, wateja, watoa huduma kwa maana ya wawekezaji wajengewe mazingira rafiki zaidi kuvutia wawekezaji zaidi kama zilivyo juhudi za Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kukaribisha wawekezaji wengine ndani na nje ya nchi kuwekeza Tanzania.




 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad