Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa msamaha wa riba na adhabu ya kodi kwa
wamiliki wa vyombo vya moto vilivyoingizwa nchini bila kufuata taratibu
za forodha kuanzia leo tarehe 25 Aprili hadi Juni 30, 2022.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma
na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo amesema kwamba, vyombo hivyo
vinahusisha vile vilivyoingizwa kwa njia za magendo, vilivyokusudiwa
kwenda nchi jirani lakini vikaingizwa nchini kinyume na taratibu,
vilivyoingizwa nchini kwa muda na kuzidisha muda wa kukaa nchini na
vilivyotumia msamaha wa kodi kinyume na sheria au kubadilishwa umiliki
bila kufuata taratibu.
“Lengo
la msamaha huu ni kutoa unafuu kwa wamiliki wa vyombo hivyo vya moto
vyenye madeni ya kodi na adhabu kwa kulipa kodi waliyokadiriwa tu bila
adhabu na riba,” Amesema Mkurugenzi Kayombo.
Amelitaja
lengo lingine la msamaha huo kuwa ni kujenga ushirikiano na uhusiano
mwema kati ya TRA na wamiliki hao, kuwapa motisha ya kulipa kodi kwa
hiari na wakati pamoja na kuweka kumbukumbu au taarifa sahihi za umiliki
wa vyombo hivyo.
Mkurugenzi
Richard Kayombo ametoa wito kwa wamiliki hao wa vyombo vya moto
kujitokeza ndani ya muda wa msamaha uliotolewa na Kamishna Mkuu ili
waweze kulipa kodi halisi inayodaiwa na hatimaye kukomboa vyombo yao.
“Nachukua
fursa hii kutoa wito kwa wamiliki wote wa vyombo vya moto
vilivyoingizwa nchini kwa njia nilizozitaja, kuchangamkia msamaha huu
ili waweze kukomboa vyombo vyao kwa kulipia kodi halisi isiyokuwa na
riba wala adhabu,” alieleza.
Mamlaka
ya Mapato Tanzania imetoa msamaha huu kwa mujibu wa kifungu cha sheria
namba 70 (2) cha Sheria ya usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015, kama
ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 pamoja na
kifungu cha 249 cha Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Forodha ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 ambazo zinampa Kamishna Mkuu wa TRA
mamlaka ya kusamehe riba na adhabu.

Baadhi
ya waandishi wa habari wakifuatilia taarifa ya msamaha wa riba na
adhabu ya kodi kwa wamiliki wa vyombo vya moto vilivyoingizwa nchini
bila kufuata taratibu za forodha iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Bw. Richard Kayombo wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
No comments:
Post a Comment