HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 19, 2022

MAHAKAMA SPORTS KAA LA MOTO

Mahakama Sports wanawake wakishangilia mara baada ya mchezo wao na Ocean Road.


 *Yawageuza Ocean Road, TPDC mlenda mchezo wa kuvuta kamba


Na Faustine Kapama-Mahakama, Dodoma
TIMU ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) leo tarehe 19 April, 2022 imeanza vizuri kwenye mashindano ya Mei Mosi yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa mara baada ya kuziadhibu vikali timu za Ocean Road na TPDC katika mchezo wa kuvuta kamba kwa upande wa wanawake na wanaume.

Ilikuwa timu ya wanawake iliyoanza kuingia uwanjani majira ya saa moja asubuhi kupambana na Ocean Road ambapo katika hatua ya kwanza mara baada ya mchezo kuanza Mahakama Sports ilichukua takribani sekunde tatu tu ndani ya dakika moja kuwanyofoa wapindani wao kwenye mstari na kuwaacha wakigalagala chini bila kuamini kilichotokea.

Kazi ilikuwa nyepesi kwenye hatua ya pili mara baada ya refa kupuliza kipenga kuashiria kuanza kwa mchezo huo ambapo Mahakama Sports kwa mara nyingine tena ilionekana kuwazindi nguvu na mbinu za kiushindani wapinzani wao, hivyo kufanikiwa kunyakua pointi zote mbili.

Baada ya mchezo huo kwa upande wa wanawake kumalizika, Mahakama Sports wanaume ambayo ndiyo timu pekee inayoogopwa katika mashindano hayo iliingia kwenye uwanja wa chekecheo na kufanikiwa kuwachekecha wapinzani wao TPDC ambao hapo awali walionekana kujiamini kuwa watatoka na ushindi mzito.

Hata hivyo, TPDC waliangukia pua mara baada ya kibao kugeuka na jahazi lao kuanza kuzama, hivyo kuondolewa kwenye mstari bila wao kutarajia katika hatua zote mbili, kitendo kilichowafanya kuanza kulaumiana kwa kushindwa kutekeleza mikakati waliyokuwa wamepanga na kuachia pointi zote mbili kwa washindani wao.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema ushindi wa leo kwa timu zote mbili ni onyo kwa timu zingine pinzani ambazo zimepangwa katika makundi yao. Timu ya wanawake ipo kundi A huku timu ya wanaume ikiwa imepangwa kundi B.

“Sisi tunachokiangalia hapa ni ushindi tu na tupo tayari kupambana na yoyote tutakayekutana naye. Tumekamilika kila idara na kutokana na maadalizi mazuri chini ya mwalimu wetu Spear Mbwembe tutatoa kipigo ambacho hakitasahaulika kwa wapinzani wetu. Hata wao wanajua sisi ni moto wa kuotea mbali,” alisema.

Kwa upande wake, Mwalimu Mbwembwe aliwataka vijana wake kutokubweteka kwa ushindi huo kwa vile washindani wao wameonyesha kuwa na nguvu za kiushindani, hivyo wanapaswa kuchukulia kila mchezo kama fainali.

“Tunamshukuru mungu kwa kupata ushindi huu, mchezo hasa kwa upande wa wanaume ulikuwa mgumu. Hivyo lazima tuchukulie kila anayekuja mbele yetu ni fainali, nawomba vijana wangu wasibweteke, tuendelee kupambana,” alisema.

Katika mechi zijazo zitakazochezwa, Mahakama Sports wanawake watapambana na Tanesco kesho tarahe 20 Aprili, 2022 na baadaye tarehe 22 Aprili, 2022 kukutana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, huku timu ya wanaume ikikutana uso kwa uso na timu ya Tanesco siku hiyo ya tarehe 22 Aprili, 2022.

Katika mashindano hayo kwa upande wa wanawake, timu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliibuka na ushindi dhidi ya Tanesco, Afya nayo ikaigalagaza Hazina huku Uchukuzi ikiibuka kidedea dhidi ya Sanaa, Tamisemi wakashinda dhidi ya Ngorongoro na TPDC wakapata ushindi wa bure mara baada ya Tarura kuingia mitini na Kilimo kupata ushindi dhidi ya Maji.

Kwa upande wa wanaume, Ngorongoro waliibuka na ushindi dhidi ya wenzao Maliasili, Mipango wakaishinda Maji, huku Kilimo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakipata ushindi wa bure dhidi ya Tarura na Ukaguzi, mtawaliwa, ambao hawakutokewa uwanjani, Uchukuzi wao wakaibuka na ushindi dhidi ya Utamaduni huku Hazina wakiangukia pua dhidi ya Mambo ya Ndani iliyopata ushindi.

Mbali na Mwenyekiti, viongozi wengine ambao wameambatana na timu hiyo ni Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Naibu Katibu Mkuu Theodosia Mwangoka, Wajumbe wawili Rajab Mwariko na Mchawi Mwanamsolo, Afisa Michezo Nkuruma Katagira, Meneja wa Timu Antony Mfaume na Meneja Vifaa Teresia Mogani.
Mahakama Sports wanaume wakichuana vikali na wapinzani wao TPDC (hawapo katika picha) leo tarehe 19 Aprili, 2022 kwenye mchezo wa kuvuta kamba katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Mahakama Sports imejizolea pointi zote mbili mara baada ya kuwashinda wapinzani wao katika hatua zote mbili.
Mahakama Sports wanaume wakishangilia mara baaya ya kuwanyoa wapinzani wao TPDC (hawapo katika picha).
Mahakama Sports wakishangilia wakiwa jukwaani mara baada ya mchezo wa kuvuta kamba dhidi ya TPDC.
Mahakama Sports wanawake wakichuana vikali na wapinzani wao Ocean Road (hawapo katika picha) leo tarehe 19 Aprili, 2022 kwenye mchezo wa kuvuta kamba katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Mahakama Sports imejizolea pointi zote mbili mara baada ya kuwashinda wapinzani wao katika hatua zote mbili.
Mahakama Sports wanawake wakishangilia wakiwa jukwaani mara baada ya kuwapa kipigo kikali Ocean Road kwenye mchezo kuvuta kamba.
Wachezaji wa Ocean Road wakiwa hawaamini kilichowatokea.
Mahakama Sports wanawake wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wao kabla ya mchezo.
Mahakama Sports wanaume wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuchuana na wapinzani wao TPDC.
Mahakama Sports wakiwa jukwaani mara baada ya mashindano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad