HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, April 12, 2022

JAJI MKUU ATETA NA WAJUMBE WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA

 Na Faustine Kapama, Mahakama

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 12 Aprili, 2022 amekutana na baadhi ya wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini ofisini kwake jijini Dar es Salaam na kuzungumza nao mambo mbalimbali, ikiwemo utoaji wa adhabu mbadala na mfumo wa utekelezaji wa mchakato wa makubaliano (plea bargaining process).

Wakiwa katika mazungumzo yao, wajumbe hao ambao waliongozwa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe wamemweleza Jaji Mkuu kuwa kuna sheria nyingi zimetungwa na zingine kufanyiwa marekebisho kuruhusu Mahakama kutoa adhabu mbadala kwa mtuhumiwa yoyote anapotiwa hatiani kwa kosa la jinai.

Wamesema kuwa kutokana na utafiti walioufanya kutoka kwa wadau mbalimbali wamebaini utekelezaji wa sheria hizo umekuwa hafifu, kwa vile watu wachache ndiyo wanaonufaika na utaratibu huo. Hivyo wajumbe hao wakaomba kufahamu maoni yake kama Mkuu wa Mhimili na mambo gani yafanyike kuhakikisha Mahakama inautumia vizuri mfumo huo ili watu wengi hasa wale waliohukumiwa vifungo ambavyo havizidi miaka mitatu waweze kunufaika.

Wajumbe pia waliomba maoni ya Mhe. Prof. Juma kuhusu mfumo wa ‘plea bargaining’ ulivyo, kama una kasoro na kama kuna kasoro, ipo katika ngazi gani. Jaji Mkuu alianza kueleza uzoefu wake kuwa katika ziara mbalimbali alizozifanya amegundua Mahakimu hupata shinikizo kutoka kwenye jamii ambayo inapenda kwamba adhabu kali ndiyo inayopaswa kutolewa kwa wahalifu.

“Lazima tuangalie jamii yetu, hata Wabunge wanapenda adhabu kali. Adhabu zetu kwanza ni kubwa ukilinganisha na Kenya. Utakuta hata zile jitihada za utashi wa kupenda kutoa adhabu mbadala haziungwi mkono na ukubwa wa adhabu ambazo zinatolewa na Mahakimu mara nyingi hupata lawama kutoka kwa jamii. Hivyo Mahakimu wanakuwa makini na jamii inayowazunguka,” alisema.

Amebainisha vile vile kuwa ukiongea na Wakuu wa Wilaya utagundua wengi kwenye Kamati za Ulinzi na Usalama hupendelea kuweka watu ndani badala ya kutoa adhabu mbadala. Hivyo Jaji Mkuu akasema changamoto iliyopo siyo kwa Mahakimu, ambao hujaribu kusoma jamii inayowazunguka. Mhe. Prof. Juma amesema kuwa pamoja na kutekeleza sheria pia huangalia utayari wa jamii kupokea wafungwa watakao hukumiwa kutoa huduma katika jamii.

“Mfano kama Hakimu akiwaruhusu pengine wafungwa 50 kwenda kutoa huduma za kijamii, je taasisi za umma zina ule utayari wa kuwapokea na pengine kuwahudumia kwa sababu wale ni binadamu? Jamii ipo tayari kuwapokea na kuwapa nafasi ya kutoa hizo huduma? Mimi naona ni msukumo kutoka kwa jamii ambayo uelewa ni mdogo. Kwa hiyo, hili ni suala la elimu kwa jamii na hata Wabunge wanaotunga hizi sheria,” alisema.

Kuhusu ‘plea bargaining process’, Jaji Mkuu amewaeleza wajumbe wa Tume hiyo kuwa mchakato huo, ambao ni zao la Kamati ya Kanuni ya Jaji Mkuu ni mzuri katika mfumo wa haki jinai na kwamba tatizo alilopo siyo kwenye sheria yenyewe bali utekelezaji wa sheria husika. Amesema kitu kilichopotosha suala hilo ni watu kuchukulia dhana hiyo kama biashara.

“Hii dhana ya plea bargaining imechukuliwa kama una shilling ngapi, utanipa shilingi ngapi, badala ya mhusika pengine anakubaliana taarifa za kihalifu, hivyo akiachiwa kwenye kosa fulani atawapa taarifa ya magenge ya uhalifu, dhana hiyo imejikita katika kupata fedha. Nadhani wale waliotekeleza mara ya kwanza hawakuelewa dhana halisi ya plea bargain, ndiyo maana haikushuka kwa watu wa kawaida, ilihusu fedha kuliko makosa mengine na ilijikita Dar es Salaam zaidi,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, ukiangalia sheria husika mfumo huo ulitakiwa kusambaa nchi nzima na siyo mashauri yote kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ambaye hana uwezo wa kufika huko na kwamba mchakato lazima uwahusishe wale waliofanya upelelezi, kwa vile wao ndiyo wanaofahamu makosa ambayo upelelezi wake bado wanaufanyia kazi.

Wajumbe wengine wa Tume waliohudhuria mazungumzo hayo ni Naibu Katibu-Idara ya Utafiti, Bw. Kharist Luanda, Naibu Katibu-Idara ya Mapitio, Bw. Lusungu Hongoli na Mtafiti na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Cleophase Morris.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisistiza jambo alipokutana na baadhi ya wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini leo tarehe 12 Aprili, 2022 ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe akifafanua jambo wakati wa mazungumzo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Naibu Katibu-Idara ya Utafiti kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria nchini, Bw. Kharist Luanda akiomba maoni ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kuhusu changamoto zinazoikabili Mahakama kutoa adhabu mbadala kwa watuhumiwa wanaotiwa hatiani kwenye makosa ya jinai.Naibu Katibu-Idara ya Mapitio kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria nchini, Bw. Lusungu Hongoli akieleza mfumo wa utekelezaji wa mchakato wa makubaliano (plea bargaining process) mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.

Mtafiti na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Cleophase Morris akifuatilia kwa kina mazungumzo kati ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini.
Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe akisaini katika kitabu cha wageni alipokuwa katika ofisi ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Naibu Katibu-Idara ya Utafiti kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria nchini, Bw. Kharist Luanda akisaini katika kitabu cha wageni alipokuwa katika ofisi ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini wakiwa ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mhe. January Msoffe.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad