HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, April 20, 2022

Benki ya CRDB yaeleza umuhimu wa filamu ya Royal Tour katika ukuaji wa utalii na uchumi

Filamu ya “Royal Tour” ambayo imezinduliwa siku ya jumatatu ya tarehe 18 April, 202 inatoa fursa za ukuaji wa uchumi kwa Tanzania, hayo amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, huku akibainisha namna ambavyo benki hiyo imejipanga katika kuwawezesha Watanzania kunufaika na fursa zitakazotokana na filamu hiyo.

Nsekela akiwa ni miongoni mwa ujumbe wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania (TBA) ambao wameambatana na Rais Samia katika safari yake ya Marekani, alisema Royal Tour itaongeza kwa kiasi kikubwa ujio wa watalii na uwekezaji nchini. 

“Tunatarajia The Royal Tour itafikia malengo yake ya kuitangaza Tanzania kama nchi inayoongoza kwa vivutio vya utalii duniani na hivyo kusaidia kuvutia watalii kuja Tanzania…Pia itakuza biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine na kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini,” alisema. 

Wakiwa kwenye ziara ya uzinduzi wa “The Royal Tour”, ujumbe wa Benki ya CRDB ulikutana na Citibank, pamoja na Shirika la Pegasus, ambapo walijadili masuala ya biashara ambayo yanaweza kuinufaisha Tanzania na Watanzania.
Ujumbe wa Benki ya CRDB ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Abdulmajid Nsekela (wa pili kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Moody's Investors Service Ana Arsov (katikati) walipotembelea Makao Makuu ya Moody's yaliyopo katika Jiji la New York Marekani. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa (wa pili kushoto), Meneja Mwandamizi wa Uwekezaji Endelevu wa Benki hiyo, Kenneth Kasigila (wa kwanza kushoto), na Afisa Uhusiano  wa Biashara, Iman Tassama.

Ujumbe wa Benki ya CRDB pia uliitembelea Moody's na kufanya majadiliano ya hali ya juu kulingana na msimamo wa soko, ikijumuisha kuwajengea uwezo, kupata taarifa na ufuatiliaji wa viwango vya mikopo.
Mkutano na watendaji wakuu wa Citibank ulijadili vipaumbele muhimu vya pamoja ikiwamo kusaidia uwezeshaji wa kiuchumi kwa wajasiriamali wadogo na wakati, kwa kuzingatia uwezeshaji wa wanawake na vijana, uwekezeaji katika huduma za kidijitali, na kusaidia ajenda ya Uchumi wa Bluu.

"Tulijadili pia msaada wa kiufundi kwa Benki ya CRDB ili kuimarisha uwezo wa Benki katika kuhudumia kundi la wajasiriamali ambao kwa kiasi kukubwa wameathirika na janga la COVID19 na kukidhi mahitaji yanayokua kwa kasi,” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa katika mkutano huo walijadili ushirikiano wa kibiashara katika kampuni tanzu ya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Katika kikao na watendaji kutoka Pegasus, kampuni ya Kimarekani inayowekeza kwenye biashara zinazozingatia utunzaji wa mazingira na zinazohusiana na afya, kampuni hiyo ilieleza nia yake ya kuingia katika soko la Tanzania na kujadilijinsi gani inaweza kushirikiana na Benki ya CRDB.
Filamu ya Royal Tour ambayo ilirekodiwa nchini Tanzania - itatumika kutangaza vivutio vya utalii vya nchi kwa kiwango cha kimataifa, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpya wa serikali za kukuza utalii baada ya janga la kimataifa la Covid-19. Baada ya kuzinduliwa kwa mara ya kwanza huko New York Aprili 18, filamu hiyo pia itazinduliwa mjini Los Angeles Aprili 21, Dar es Salaam Aprili 28, na baadaye Zanzibar.

Rais Samia alihusika katika kurekodi filamu hiyo mwaka jana alipokuwa akisafiri katika maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii akiwa na na mwandishi wa habari nguli aliyeshinda tuzo ya Emmy, Peter Greenberg.

Sekta ya utalii ya Tanzania ambayo iliathiriwa vibaya na janga la Covid-19, imekuwa katika hali ya ahueni, ambapo takwimu za Benki Kuu ya Tanzania zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka unaoishia Februari 2022, mapato ya fedha za kigeni kutoka sekta hiyo yaliongezeka hadi dola za kimarekani bilioni 1.457 kutoka dola za kimarekani bilioni 645.4 katika kipindi kama hicho mwaka jana. Ongezeko hilo lilitokana na ongezeko la asilimia 87.9 la watalii waliofika na kufikia wasafiri 958,173 katika kipindi kinachoishia Februari 2022.

Kwa mujibu wa Nsekela, filamu ya Royal Tour - ambalo Mhariri wa Wasafiri wa Habari wa CBS Peter Greenberg ametayarisha - itasaidia kuuelezea ulimwengu utajiri wa maliasili nyingi za Tanzania, ikiwa ni pamoja na rasilimali, utamaduni, mila na desturi za Taifa letu la Tanzania.
Ujumbe wa Benki ya CRDB ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji, Abdulmajid Nsekela (wa nne kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi Waandamizi wa Citibank walipotembelea Makao Makuu ya Citibank jijini New York. Nsekela aliongozana na Mkurugenzi wa Mawasiliano, Tully Mwambapa (wa pili kushoto), Meneja Mwandamizi wa Uwekezaji Endelevu wa Benki hiyo, Kenneth Kasigila (wa kwanza kushoto), na Afisa Uhusiano wa Biashara, Iman Tassama.

"Tuna madini ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee duniani kote...tuna hifadhi kubwa ya gesi asilia, makaa ya mawe, mito, maziwa, bahari na mapori ya akiba. Tuna zaidi ya makabila 100 ambayo yanaishi kwa amani. Tuna utamaduni tajiri na mila, vyakula asilia, historia na mavazi yetu. Haya yote yanaunda fursa ya kiuchumi," alisema.

Nsekela alidokeza kuwa Benki ya CRDB imejipanga vyema kunaweka mazingira wezeshi yatakayosaidia wananchi na Taifa kunufaika na fursa zitokanazo na filamu ya Royal Tour, kupitia huduma na bidhaa bunifu zinazotolewa na benki hiyo.

Baadhi ya huduma na bidhaa za Benki ya CRDB zitakazowezesha kusaidia wateja kunufaika na fursa hizo ni pamoja na huduma za uwezeshaji kupitia mikopo ya Uwekezaji na uendeshaji wa biashara, pamoja na mifumo thabiti ya malipo kupitia vifaa vya manunuzi (PoS), huduma za TemboCard, pamoja na mifumo ya malipo ya kidijitali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad