HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 8, 2022

WAZIRI SIMBACHAWENE AKUTANA NA VIONGOZI WA MTANDAO WA THRDC

 





Charles James

WAZIRI wa Katiba na Sheria George Simbachawene, amesema serikali ya Tanzania ipo katika mchakato wa kurudi kuwa wanachama wa Mahakama ya Afrika baada ya kujitoa kwa muda sasa kutokana na sababu mbalimbali.

Simbachawene, alibainisha hayo juzi mara baada ya kikao cha pamoja na viongozi wa Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu Tanzania (THRDC) kilichofanyika katika ofisi za wizara ya Katiba na Sheria Mtumba jijini Dodoma.

Alisema, suala la Tanzania kujitoa katika Mahakama ya Afrika, zilikuwepo sababu lakini haziwezi kuwa za kudumu.

Waziri Simbachawene, alieleza kuwa mazungumzo yanaendelea ndani ya serikali na anaamini nchi itarudi tena katika Mahakama hiyo.

"Mahakama hii ipo Tanzania, inakuwa si vizuri sana kama tena sisi Watanzania tutakuwa hatupo kwenye hii Mahakama tupewe muda, mchakato unaendelea nina imani si muda mrefu maamuzi yatatolewa na serikali"alisema Simbachawene

Aidha, alisema Tanzania ni nchi ambayo inatambua, inaheshimu, inatunza na kulinda haki za binadamu, na itaendelea kushirikiana na wadau wa masuala ya Haki za Binadamu.

“Katika mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia ameonyesha nia ya kutunza haki maeneo ambayo yameonyesha kuwa na shida katika maeneo ya haki za binadamu anafanya hivyo kwa vitendo, pamoja na nadharia.

“Wizara ya Katiba na Sheria imefurahi kuona mpo na itaendelea kushirikiana na nanyi katika kila jambo ambalo mtapenda tushirikiane." alisema Simbachawene

Pia, aliwataka Watetezi wa Haki za Binadamu nchini kuhoji na kuzungumza na wizara, kuliko kupeleka katika majukwaa ya kimataifa na kuiondolea heshma nchi.

Vilevile, alisema Wizara itashiriki kwa pamoja na AZAKI katika majukwaa ya kimataifa ili kuhakikisha Tanzania inajengwa kwa mashirikiano thabiti na yenye tija kati ya pande zote mbili.

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, katika kikao hicho alitaja baadhi ya maeneo ambayo yanaweza kufanyiwa maboresho na wizara ikiwemo kuwa na utataratibu mzuri wa kufahamu, kuripoti na kutambua kazi za watetezi wa Haki za Binadamu kama wadau muhimu wa wizara hiyo.

“Pia, kufanyika kwa maboresho katika maeneo ya utoaji wa msaada wa kisheria,uboreshwaji wa mifumo ya utoaji haki nchini,maboresho ya baadhi ya sheria ikiwemo sheria ya NGO, hasa katika upatikaji wa vibali vya tafiti inayoyataka mashirika kupitia TAMISEMI ili kupata pamoja na sheria zingine,ushiriki wa wizara katika mikutano na majukwaa ya kimataifa,Tanzania kurudi katika mahakama ya Afrika Mashariki”alisema

Pamoja na meneo hayo ya maboresho THRDC pia imetoa mapendekezo ya kufanyiwa kazi na wizara katika kuboresha shughuli za utetezi wa Haki za Binadamu nchini.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kuboreshwa kwa mfumo wa utekelezaji (Human Rights Enforcement Mechanism - BRADEA) sheria iliyokuwa inaweka utaratibu wa kulinda haki za kikatiba.

Olengurumwa, alisema mabadiliko yaliyofanyika yameweka vikwazo vingi kwa mtanzania mmoja mmoja au taaisisi zao kutekeleza agizo la ibara ya 26/2 ya kulinda katiba.

“Kumekuwa na vigingi vingi ambavyo tunaweza kufanya majadiliano na maboresho kupitia wizara hii ambavyo yatatoa fursa ya watanzania kwenda moja kwa moja na Taasisi za Haki za Binadamu kwenda mahakamani kulinda na kutetea haki za Binadamu kupitia mlango wa kikatiba.

“Kuwepo kwa National human rights Action plan (Mpango wa Taifa wa Haki za Binadamu, serikali iangalie namna ya kuharakisha kukamilika kwa mchakato huo ili kuwa na andiko litakalotoa mwongozo utawaunganisha wadau wa haki za Binadamu na serikali."alisema Olengurumwa

Hata hivyo, alisema kuwepo na Sera ya Haki za Binadamu ambayo inaweza kutoa mwongozo kwa taasisi binafsi na serikali kuhusiana na masula ya haki za binadamu.

“Sera hii itawatambua na kuwalinda watetezi wa Haki za Binadamu. Hii ni kuwawezesha Wadau pamoja na serikali wawe na uelewa wa pamoja wa maswala ya utetezi na Watetezi wa Haki za Binadamu nchini.

“Kumekuwa na changamoto za utekelezaji wa maamuzi wa Mahakama za ndani na nje hasa katika maeneo ya access to justice katika kesi za Haki za Binadamu, lazima uje Dar es Salaam. Tunapendekeza serikali iruhusu kila high kort yenye hadhi ya Mahakama Kuu iwe na uwezo wa kusikiliza kesi hizo katika Mikoa kesi hizo ziliporipotiwa." Alisema Olengurumwa.

Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene akizungumza na viongozi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma.

Waziri wa Katiba na Sheria George Simbachawene akikabidhiwa mapendekezo na Viongozi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, THRDC ofisini kwake Mtumba Jijini Dodoma.
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC, Onesmo Olengurumwa akizungumza katika kikao baina ya Mtandao huo na Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene jijini Dodoma.
 
Waziri wa Katiba na Sheria, George Simbachawene akiwa katika picha ya Pamoja na Viongozi wa Wizara hiyo ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad