HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 16, 2022

WADAU WASHAURI SUALA LA BIMA LA AFYA KWA WOTE KUWA AJENDA YA KITAIFA

 


Mbunge wa Jimbo la Mbozi mkoani Songwe Mh. George Mwenisongole akieleza jinsi uwepo wa bima ya afya kwa watu wote itakavyowasaidia wananchi hasa wanaoishi vijijini, wakati wa uzinduzi wa mkakati wa bima ya afya kwa wote inayojumuisha magonjwa yasiyoambukiza.


Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeshauriwa kujumuisha matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza katika bima ya afya kwa wote ili kupunguza vikwazo vinavyowakumba watu wanaoishi na magonjwa hayo, kuokoa maisha yao.

Aidha, tathmini ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inabainisha kwamba zaidi ya asilimia 45 ya vifo vinavyotokea duniani hutokana na magonjwa hayo na kwamba kipindi cha Uviko-19 viliongezeka kwa kuwa wanaougua magonjwa hayo waliathiriwa zaidi.

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA) Prof. Kaushik Ramaiya aliyasema hayo hivi karibuni kwenye uzinduzi wa mkakati wa utetezi kuhusu bima ya afya kwa watu wote inayojumuisha magonjwa yasiyoambukiza, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Prof. Ramaiya alisema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), unatoa huduma aina mbalimbali ambazo zimekuwa zikitoa matibabu ya magonjwa mengine, ingawa baadhi ya huduma za matibabu hazipatikani katika bima kwa wanaougua magonjwa hayo, hivyo kuwanyima fursa ya huduma kamili hospitalini.

“Magonjwa yasiyoambukiza yanagharama kubwa katika kuyatibu, kupitia NHIF, wananchi wamekuwa wakikata bima za afya za aina mbalimbali lakini kadi hizo zimekuwa zikitoa baadhi ya huduma, na huduma nyingine kama dawa, upasuaji na vifaa kutokuwapo katika bima hivyo kuwanyima fursa wagonjwa ya kupata matibabu kamili.

“Ninaiomba Serikali iliangalie hili kwani tathmini iliyofanywa na WHO inaonyesha baada ya miaka mitano hadi 10 ijayo, vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza vinaweza kuongezeka na kuwa zaidi ya asilimia 55.

“Magonjwa yasiyoambukiza yasipotibiwa vizuri husababisha mtu kupata madhara mengine kama vile kudhuru figo, mishipa ya damu, macho, kupata kiharusi na madhara mengine mengi ambayo humsababishia mtu kupoteza uhai wake,” alisema Prof. Ramaiya.

Aidha Prof. Ramaiya aliiomba serikali kuratibu upatikanaji wa matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza katika maeneo yote yenye zahanati na vituo vya afya, ili jamii ipate huduma maeneo ya karibu na kwa wakati na kupunguza madhara yanayoweza kutokea kama magonjwa hayo hayatatibiwa mapema.

“Kama wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza watapata huduma za matibabu kwa wakati katika vituo vya karibu vya afya wataweza kuendelea na shughuli zao za kiuchumi hivyo kukuza vipato vyao na pato la taifa.

“Jamii inapaswa kujikinga na magonjwa haya yasiyoambukiza kwani utafiti uliofanywa na WHO unaonyesha kila dola moja unayoiweka katika kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza unapata nafuu ya dola saba hadi 12 kwa kila dola uliyotumia kuwekeza katika kinga,” alisema Prof. Ramaiya.

Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mkoa wa Songwe, George Mwenisongole alisema suala la bima ya afya kwa wote likawe ajenda ya kitaifa ili kutoa fursa kwa kila Mtanzania kuwa na matumaini ya kupata matibabu pale wanapougua magonjwa mbalimbali.

“Bima ya afya kwa wote inapaswa kuwa bima isiyobagua lakini bima inayotoa huduma zote za matibabu ili Watanzania wafaidike na huduma za matibabu hasa wale wenye magonjwa yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakitibiwa kwa gharama kubwa.

“Nimepata nafasi ya kushiriki semina iliyoandaliwa na TANCDA na kujifunza mengi kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza, wito wangu kwa serikali ni kuhakikisha tunapata sera ya kitaifa ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ambayo itaweza kuzuia uvutaji wa sigara hadharani ili kuokoa maisha ya watu wanaoathirika na moshi wa sigara,” alisema Mwenisongole.

Mwanahabari, Gloria Tesha aliiomba serikali kuwekeza katika elimu ya magonjwa yasiyoambukiza, kuanzia ngazi ya shule za msingi ili watoto wanapokua wawe na ufahamu wa kutosha juu ya magonjwa hayo, na itawasaidia kujikinga na magonjwa hayo.

“Waandishi wa habari tupo tayari kutumia kalamu zetu kupaza sauti ili jamii ifahamu athari za magonjwa yasiyoambukiza na namna ambavyo itaweza kujikinga na magonjwa hayo. Ninaiomba serikali pamoja na taasisi zinazojihusisha na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kututumia ili tuweze kuzifikia jamii na kuziokoa.

“Wadau na serikali kwa pamoja tukubaliane kupiga vita magonjwa yasiyoambukiza kwa kuyafanya magonjwa haya kuwa ajenda ya kitaifa katika kila kikao kinachofanyika kuanzia ngazi za mitaa, kata, wilaya na mikoa ajenda hiyo ikipewe kipaumbele ninaamini tutaweza kupunguza ama kuyaondoa kabisa magonjwa haya,” alisema Gloria. 

Meneja Mradi kutoka TANCDA, Happy Nchimbi, alisisitiza kwamba wakati nchi ikijiandaa kuelekea kupata huduma ya afya kwa watu wote, suala la kuzuia magonjwa yasiyoambukiza lipewe kipaumbele.

Alisema bajeti itengwe ya kupambana na kuzuia magonjwa yasiyoambukizwa ili kuwakwamua Watanzania wanaougua magonjwa hayo.

Uzinduzi wa mkakati wa utetezi juu ya bima ya afya kwa watu wote inayojumuisha magonjwa yasiyoambukiza uliandaliwa TANCDA na kushirikisha wadau mbalimbali wakiwamo Wizara ya Afya, wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, watu wanaoishi na magonjwa yasiyoambukiza na wanahabari.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad