HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 16, 2022

KUMBI ZA MIHADHARA, MABWENI TAASISI YA MAENDELEO YA JAMII TENGERU ZAIKOSHA KAMATI YA BUNGE


 

Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii walipotembelea miradi ya Maendeleo katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru iliyoko Mkoani Arusha.
Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis akiiongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii walipotembelea miradi ya Maendeleo katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru iliyoko Mkoani Arusha.
 Mkuu wa Taasisi ya Mandeleo ya Jamii Tengeru Dkt. Bakari George akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii walipotembelea miradi ya Maendeleo katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru iliyoko Mkoani Arusha

 

Na WMJJWM- Arusha

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeeleza kuridhishwa na miradi ya Maendeleo katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru iliyoko Mkoani Arusha.

 

Akizungumza katika ziara ya kukagua miradi hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Aloyce Kamamba amesema Kamati yake imefarijika na maendeleo yaliyofikiwa kutokana na ujenzi wa miradi katika Taasisi hiyo.

 

Miongoni mwa miradi inayoendelea ni Ujenzi wa Kumbi Pacha za mihadhara yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,008 pamoja na Bweni la wasichana linaloweza kuchukua wanafunzi 568 kwa wakati mmoja.

 

"Pamoja na mafanikio haya Taasisi ihakikishe inafanya ukarabati wa majengo yaliyojengwa miaka zaidi ya hamsini iliyopita ili kuendana na wakati uliopo sasa na hadhi ya Taasisi hiyo" amesema Kamamba 

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis ameahidi kuwa Wizara itaendelea kuongeza jitihada za kuhakikisha elimu inayotolewa katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na vyuo vingine vya Maendeleo ya Jamii vilivyo chini ya Wizara inaendana na uhitaji wa soko la ajira nchini.

 

Naibu Waziri Mwanaidi ameipongeza Kamati hiyo kwa jitihada na maelekezo kwa Serikali hadi kufanikisha mipango ya Maendeleo kama ilivyopangwa kwa kusimamia utoaji wa fedha hasa katika miradi ya Maendeleo.

 

Akijibu baadhi ya maswali ya wajumbe wa Kamati, Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula amesema tayari Wizara imeanzisha utaratibu wa kuwawezesha wahitimu kupitia dhana ya uanagezi yenye lengo la kuwasaidia wahitimu katika kuajiriwa, kujiajiri na kuajiri wengine.

 

Aidha, amesema Wizara tayari inashirikiana na wadau wa Maendeleo kuhakikisha Taasisi zilizo chini ya Wizara na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vinakuwa katika mwonekano na hadhi thabiti.

 

Baadhi ya Wabunge wameshauri wakati jitihada zinaendelea kuwawezesha wanafunzi wa kike, wanafunzi wa kiume wasiachwe kando ili kuwa na kizazi chenye usawa.

 

Naye Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Dkt. Bakari George amesema miradi ya Ujenzi wa kumbi na Bweni utakuwa umekamilika ifikapo Septemba mwaka huu. 

 

Tarehe 17 Machi, 2022 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii itaendelea na ziara katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rungemba kukagua shughuli za Maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad