HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 31, 2022

TEKNOLOJIA ILIYOLETWA NA MWEKEZAJI DIASPORA ANAYEISHI NCHINI CANADA YAVUTIA SEKTA ZA UJENZI NCHINI

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaratibu ziara ya wiki mbili ya Mwekezaji Diapora kutoka nchini Canada, Bw. Joseph Katallah ambaye ameonesha nia ya kuwekeza katika miundombinu ya barabara.

Bw. Katallah anashirikiana na Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani inayomilikiwa na Bw. Rodney Zubrod ambayo imebuni teknolojia mpya ya ujenzi wa barabara za lami na madaraja yanayotumia teknolojia hiyo. Pia teknolojia hiyo hutumia mabaki ya uchafu wa migodini na viwandani hususani viwanda vinavyotengeneza alumina na vioo. Uchafu huo kitaalamu huitwa matope mekundu.

Aidha, kampuni hiyo imefanikiwa kuwa na bidhaa nyingine zaidi ya barabara katika nchi za Canada, Uingereza na Uholanzi ambapo wametengeneza vifaa vya kuzimia moto, kupiga plasta na kuzuia kutu kwenye majengo na matanki ya kuhifadhia bidhaa mbalimbali.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago ameeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imefanikiwa kuwakutanisha wawekezaji hao na sekta za ujenzi nchini kwa lengo la kuinadi teknolojia hiyo mbadala ya geopolymer na matumizi yake ambayo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa nchini Canada, Marekani na Uingereza.

Akaongeza kuwa Bw. Katallah ni mmoja wa wanadiaspora ambaye amehamasika kurudisha ubunifu wake nyumbani. Pamoja na kuonesha nia ya kuwekeza katika miundombinu ya barabara pia amewekeza katika miradi ya kilimo, ujenzi wa shule (iitwayo shamba darasa kwa vijana walioishia darasa la saba hadi kidato cha sita) pamoja na ujenzi wa barabara ya mfano inayotumia teknolojia ya “nano” mkoani Singida.

Kadhalika uwezo wa teknolojia hiyo mbadala ya Geopolymer kutumia uchafu wa migodini na viwandani ni sehemu ya mikakati ya utunzaji wa mazingira. Bila kuathiri taratibu za ujenzi unatumika sasa imeelezwa kuwa teknolojia hiyo mpya italeta unafuu wa gharama za ujenzi kufuatia uwepo wa rasilimali za kutosha nchini na hivyo kuhitaji utaalamu na vifaa.

Idara za ujenzi zilizokutana na wawekezaji hao ni pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tarehe 28 Machi 2022; Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini –TARURA tarehe 30 Machi 2022; Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) tarehe 30 Machi 2022 na Wakala wa Barabara Tanzania - TANROADS wanatarajia kukutana na wawekezaji hao tarehe 1 April 2022.

Pamoja na Mwekezaji huyo Diaspora Wizara kupitia idara ya Diaspora inaendelea kuhamasishaji Diaspora wengine wenye malengo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini na inawahakikishia ushirikiano katika hatua za kurasimisha uwekezaji.
Kulia ni Mkurugenzi wa Miundombinu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Gilbert Mwoga; kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago; Rais wa Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC kutoka nchini Marekani, Bw. Rodney Zubrod; Mhandisi Idara ya Miundombinu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhandisi, Gilbert Mfinanga na Mwekezaji mzawa kutoka nchini Canada, Bw. Joseph Katallah.
Mazungumzo yakiendelea.
Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Tagie Daisy Mwakawago akiteta na Mkuu wa Kitengo cha Tafiti na Udhibiti Ubora - TARURA, Dkt. Philemon Msomba wakati wa kikao pamoja na wawekezaji kilichofanyika tarehe 30 Machi 2022 kwenye ofisi za makao makuu ya TARURA jijini Dodoma.

Kikao kikiendelea.

Mwekezaji kutoka nchini Canada, Bw. Joseph Katallah (kushoto) akifafanua juu ya teknolojia mpya ya Geopolymer na matumizi yake, pembeni yake ni Rais na mmiliki wa Kampuni ya Geopolymer Solutions LLC ya nchini Marekani, Bw. Rodney Zubrod.Kikao kikiendelea


Kikao kikiendelea.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad