Na Chalila Kibuda, Michuzi Tv
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amefungua mafunzo ya Utekelezaji wa mfumo uwekaji wa anwani za makazi unatakiwa kukamilika Mei mwaka huu ambapo itakuwa alama ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kukamilika kwa mradi huo kwa mwezi Mei mwaka 2022 kwa kila mtendaji atakuwa ameandika rekodi kutokana na mradi huo ulitakiwa kuisha Mwaka 2025.
Akizungumza katika ufunguzi kwa njia mtandao kwa wakuu wa mikoa kwa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa kuunganishwa na Ofisi TTCL Jijini Dar es Salaam Nape amesema utekelezaji wa mfumo huo ni moja kati ya mikakati ya kuiweka nchi katika mfumo wa kidigitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kurahisisha biashara ya mtandao.
“Mradi huu ni moja ya miradi ambapo Rais wa Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuacha alama na utekelezaji wake ulitakiwa ufanyike kwa miaka mitano lakini kwa sababu ya umuhimu wake mpaka mwezi Mei mwaka huu zoezi hili litakuwa limekamilika”, Amesema Waziri Nape.
Amesema utekelezaji wa Anwani za makazi itakuwa ni zoezi ambalo litarahisisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ambayo itafanyika Agosti mwaka huu na itakuwa rahisi kwa sababu ya upatikanaji wa anwani za makazi.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa mfumo wa anwani ya makazi ni muhimu sana kwa wananchi hivyo tunalo jukumu na wajibu mkubwa ili zoezi na mfumo huu liweze kukamilika kwa wakati.
Kwa upande wake Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo alieleza jinsi mfumo huu wa anwani za makazi utakavyorahisisha biashara mtandao ambapo kwa sasa Shirika la Posta lina Jumla ya maduka 600 kupitia duka lake Mtandao (Posta Online Shop) ambayo kwa uhakika yanategemea upatikanaji wa anwani za makazi katika maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi.
“Tumejipanga kimkakati kuhakikisha tuko tayari kwa matumizi ya anwani hizi, kwani tumeanzisha huduma ya duka mtandao ambalo limeunganishwa nchi zote duniani ambapo wananchi watakuwa wananunua na kuuza bidhaa zao duniani kote”, Macrice Mbodo.
Waziri wa Habari na Teknolojia ya Mawasiliano Nape Nnauye akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya anuani za Makazi kwa watendaji na wakuu wa Mikoa Tanzania Bara na Tanzania visiwani kwa njia ya Mtandao katika kuelekea.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano (TTCL) Waziri Kindamba akizungumza kuhusiana na uimarishaji wa mawasiliano kwa njia ya mtandao wakati wa kikao cha ufunguzi wa mafunzo ya anuani za makazi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano Dk. Jimmy Yonazi akizungumza kuhusiana na wizara hiyo ilivyojipanga utekelezaji wa anuani za makazi jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment