Serikali kudhibiti viwanda bubu vya kuzalisha dawa za mifugo - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, January 23, 2022

Serikali kudhibiti viwanda bubu vya kuzalisha dawa za mifugo


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) akiongea na mmoja wa madaktari wa dawa za Mifugo wa Kampuni ya Farmbase alipokuwa akikagua baadhi ya dawa zinazozalishwa na Kampuni hiyo muda mfupi baada ya kukagua eneo watakalojenga Kiwanda kikubwa cha kuzalisha Dawa za mifugo lililopo Wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam Jana. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Farmbase, Bw. Suleiman Msellem.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Farmbase, Bw. Suleiman Msellem(kushoto) akimpatia maelezo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) kuhusu mchoro wa Kiwanda kikubwa cha kuzalisha Dawa za Mifugo kitakachojengwa Wilayani Kigamboni, jijini Dar es Salaam alipotembelea eneo hilo Jana. 
 
Na Mbaraka Kambona,

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Serikali inaendeleza jitihada za kudhibiti utengenezaji holela wa dawa za mifugo pamoja na zile dawa feki za mifugo zinazoingizwa  ili kuwalinda wafugaji nchini.

Waziri Ndaki alibainisha hayo jana alipotembelea eneo la Kampuni ya Uzalishaji, Usambazaji na Uingizaji wa pembejeo za mifugo na Kilimo( Farmbase) lililopo Wilayani Kigamboni, Jijini Dar es Salaam ambalo wanataka  kujenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha dawa za mifugo nchini.

Alisema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wafugaji kuwa kuna baadhi ya dawa wanazozitumia kutibu mifugo yao haziwapi matokeo wanayoyatarajia, na ndio maana serikali inaendelea kudhibiti uuzwaji holela wa dawa hizo na kuimarisha utaratibu mzuri wa kupatikana dawa halisi za mifugo.

“Hivi karibuni tuna mpango wa kuweka maduka ya kuuza dawa katika kila mnada ili kuwahakikishia wafugaji wetu kwamba dawa aliyonunua kutoka katika maduka hayo ni sahihi kuitumia, mpango wetu haya maduka yaendeshwe na watu binafsi chini ya usimamizi wa serikali,” alisema Mhe. Ndaki

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Farmbase, Bw. Suleiman Msellem alisema kuwa wao wapo tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha dawa halisi kwa ajili ya mifugo zinapatikana kwa wingi hapa nchini.
“Njia moja ya kuondosha dawa feki ni kupatikana kwa dawa halisi, sisi tupo tayari kushirikiana na serikali yetu, na hata hayo maduka yakianzishwa tupo tayari kushirikiana katika kuzisambaza dawa kwenye maduka hayo,”alisema Msellem

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad