Na Veronica Simba - REA
Waziri
wa Nishati January Makamba amewaelekeza viongozi na wafanyakazi wa
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuongeza nguvu katika aina nyingine za
nishati kama inavyofanyika kwenye umeme.
Alisema
kuwa REA imeendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa usambazaji nishati ya
umeme vijijini hivyo ni vyema pia ikifanya hivyo katika aina nyingine
za nishati zenye matumizi makubwa zaidi, hususan zinazotumika katika
kupikia.
Waziri
Makamba alikuwa akizungumza na wafanyakazi wa REA ili kutoa dira na
mwelekeo wa Wizara ya Nishati, ikiwa ni mara ya kwanza kukutana nao
rasmi tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo, takribani siku 100
zilizopita. Alizungumza na wafanyakazi hao jijini Dodoma, Desemba 20
mwaka huu.
Alisema
kuwa wengi wanaitafsiri REA kuhusika na nishati ya umeme pekee kutokana
na kuweka nguvu nyingi kwenye nishati hiyo, hivyo akasema ni muhimu kwa
Wakala hiyo kuzipa uzito unaostahili nishati nyinginezo ambazo ni
jukumu lake pia.
“Kazi
ya REA ni kubwa zaidi, siyo umeme tu. Mnafanya kazi nzuri sana kwa
upande wa umeme hivyo toeni uzito unaostahili kwa nishati nyingine zenye
matumizi makubwa.”
Akitoa
mfano, Waziri Makamba alieleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa
kwa Tanzania, matumizi makubwa ya nishati yako majumbani. Aidha,
aliongeza kuwa nishati inayotumika zaidi majumbani hususan katika
kupikia ni tungamotaka.
Alisema,
asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini na wanatumia nishati ya
tungamotaka katika kupikia. “Nataka mfanye mabadiliko kwenye nishati ya
kupikia maana ndiyo inagusa Watanzania wengi zaidi,” alisisitiza Waziri.
Akifafanua,
alieleza kuwa pamoja na kupeleka umeme vijijini, haitegemewi kuwa
wakazi wake watatumia nishati hiyo kupikia hivyo ni jukumu la Wakala
kufanyia kazi suala hilo.
Sambamba
na agizo hilo, Waziri Makamba aliitaka REA kuimarisha Kitengo chake cha
Utafiti na kianze mara moja kufanya tafiti mbalimbali zitakazoleta
mapinduzi makubwa katika sekta ya nishati, hususan vijijini.
“Mathalani,
kuna mawazo au fikra gani mpya kuwasaidia Watanzania wapate nishati
safi ya kupikia? Je, nishati ya kupikia ina mchango gani katika kuongeza
au kupunguza gharama za maisha? Hizi ni baadhi ya tafiti zinazopaswa
kufanyika,” alisisitiza Waziri.
Katika
hatua nyingine, Kiongozi huyo mwenye dhamana na sekta ya nishati
nchini, alitoa maagizo kuwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme
vijijini, wanapobainika kufanya udanganyifu kwenye miradi hiyo,
wachukuliwe hatua kali ikiwemo kuondolewa kabisa na wasipewe tena fursa
ya kufanya kazi hizo.
Vilevile,
washitakiwe kwa Mamlaka zote husika pamoja na kufanya ufuatiliaji ili
wasipewe kazi nyingine katika eneo lolote ili iwe fundisho kwao kwa
kuwaumiza wananchi na kuliingizia hasara Taifa.
Pamoja
na maelekezo hayo, Waziri aliipongeza REA kwa kazi nzuri ambayo imekuwa
ikifanya na kuitaka kuongeza juhudi zaidi katika kuwatumikia
Watanzania.
Alisema
kuwa Serikali inajivunia utendaji kazi wa REA na kwamba ni mojawapo ya
Taasisi zinazotegemewa sana hivyo akaiasa isiharibu sifa hiyo.
Awali,
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, akiwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa majukumu kwa Waziri, alieleza kuwa kazi kubwa imefanyika
ambapo hadi sasa upatikanaji umeme vijijini umefikia asilimia 69.6.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius
Kalolo, akizungumza kwa niaba ya Bodi, alimuhakikishia Waziri kuwa
maelekezo yote aliyoyatoa yatafanyiwa kazi.
Waziri
aliahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa
REA ikiwemo upandishwaji madaraja na kukaimu nafasi mbalimbali kwa muda
mrefu, kama alivyowasilisha Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi, Tawi la
REA, Swalehe Kibwana.
Waziri
wa Nishati, January Makamba (kulia) akipokea Taarifa ya Utekelezaji wa
Majukumu ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu
wa Wakala hiyo, Mhandisi Hassan Saidy. Waziri alizungumza na Wafanyakazi
wa REA, Desemba 20, 2021 jijini Dodoma. Kulia kwa Waziri ni Mwenyekiti
wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo na wa kwanza kushoto
ni Mjumbe wa Bodi, Mhandisi Styden Rwebangira.
Waziri
wa Nishati, January Makamba akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa
Nishati Vijijini – REA (hawapo pichani), Desemba 20, 2021 jijini Dodoma.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo akizungumza
wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, January Makamba na wafanyakazi wa
Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Desemba 20, 2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy
akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, January Makamba na
wafanyakazi wa Wakala hiyo, Desemba 20, 2021 jijini Dodoma.
Mwenyekiti
wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Tawi la Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Swalehe Kibwana (kushoto) akimkabidhi Waziri wa
Nishati, January Makamba, Risala aliyoisoma kwa niaba ya wafanyakazi.
Waziri alizungumza na wafanyakazi wa REA, Desemba 20, 2021 jijini
Dodoma.
Kamishna
wa Umeme na Nishati Jadidifu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi
Mramba akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, January
Makamba na wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Desemba 20,
2021 jijini Dodoma.
Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy
(kulia) akimwongoza Waziri wa Nishati, January Makamba (kushoto)
alipowasili Makao Makuu ya REA, Mtaa wa Makole jijini Dodoma, kuzungumza
na wafanyakazi, Desemba 20, 2021. Pamoja nao ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo.
Waziri
wa Nishati, January Makamba (katikati), akisaini Kitabu cha Wageni,
alipowasili Makao Makuu ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) jijini
Dodoma, kuzungumza na wafanyakazi, Desemba 20, 2021.
Wafanyakazi
wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakimsikiliza Waziri wa Nishati,
January Makamba (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza nao, Desemba 20,
2021 jijini Dodoma.
Waziri
wa Nishati, January Makamba (kushoto) akiongozwa na viongozi wa Wakala
wa Nishati Vijijini (REA) alipowasili Makao Makuu ya Wakala jijini
Dodoma, kuzungumza na wafanyakazi, Desemba 20, 2021. Kutoka kushoto ni
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo,
Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy na Mkurugenzi wa Huduma za
Ufundi, REA Mhandisi Jones Olotu.
No comments:
Post a Comment