HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, December 5, 2021

Watafiti wapendekeza sera, sheria zilinde sekta isiyo rasmi

Mtafiti na Mratibu Mwandamizi katika Utafiti wa “Sekta isiyo Rasmi na Hifadhi ya Jamii”, Dkt. Godbertha Kinyondo akinyanyua kitabu kuhusu sekta isiyo rasmi na hifadhi ya jamii Kusini mwa Jangwa la Sahara kuashiria kuzinduliwa kwake.Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
UTAFITI wa miaka minne uliofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya na Roskilde cha nchini Denmark umependekeza kuwepo kwa sera na taratibu madhubuti zitakazopelekea sekta isiyo rasmi kupitia vyama vyao kufaidika na huduma za hifadhi ya jamii.

Malengo makuu ya utafiti yalilenga kufahamu namna wafanyakazi wasio rasmi kwenye sekta za usafiri, ujenzi na wafanya biashara wadogo Kenya na Tanzania wanavyopata huduma rasmi na zisizo rasmi za hifadhi ya jamii, bima za afya, pensheni, fursa za mikopo, mafunzo mbalimbali kama ya afya na usalama na namna vikundi walivyojiundia vinavyosaidia katika juhudi hizo.

Utafiti huo “Sekta Isiyo Rasmi na Hifadhi ya Jamii” ulioanza 2017-2020 ulifadhiliwa na shirika la kimataifa la maendeleo la Denmark (DANIDA) na kufanywa katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Nairobi na Kisumu.

Akiongea wakati wa warsha ya kuwasilisha matokeo ya utafiti huo kwa wadau mbalimbali jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mtafiti na Mratibu Mwandamizi katika Utafiti huo toka Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Godbertha Kinyondo, alisema upo umuhimu kwa taasisi za serikali na wadau kujifunza na kushirikiana na vyama vya wafanyakazi wasio rasmi katika kutunga sera za hifadhi za jamii ili waweze kufaidika na huduma muhimu za kijamii.

“Hilo likifanyika litaongeza tija katika sekta zao za kazi, wafanyakazi hawa ni kiungo muhimu katika uchumi,” alifafanua.

Alisema ni muhimu sasa kwa serikali kupitia taasisi zake mbalimbali kujenga uwezo na kushirikisha vyama vya wadau hao katika kutunga sera zinazogusa maisha yao na kupitia upya programu za hifadhi za jamii ili zikidhi mahitaji mapana ya wafanyakazi hao katika sekta isiyo rasmi, hususani ya usafirishaji inayokua kwa kasi Tanzania na Afrika ya Mashariki kwa ujumla.

“Serikali ipange kuwa na huduma stahiki za hifadhi ya jamii na rahisi inayoendana na hall halisi kwa wafanyakazi wa kada hii katika sekta ya usafirishaji,” alisema Dkt. Kinyondo.

Mtafiti mwingine wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Aloyce Gervas alisema sekta ya ujenzi ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu katika kuchangia pato la taifa kwa asilimia 13 bado ina watu wasio na ujuzi rasmi. Sekta hiyo pia ndio inayoongoza katika kusababisha ajali za kazini kwa asilimia 23.7 kulinganisha na sekta nyingine.

Alisema upo umuhimu wa kupitia upya sera ya taifa ya sekta ya ujenzi ili kuwatambua vyema mafundi ujenzi wasio na taaluma rasmi na mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF kutoa elimu ya kutosha kwa mafundi nchini juu ya faida za mifuko hiyo.

“Sera ya Afya na Usalama mahali pa kazi irejewe ili kutambua watu wasio rasmi wanaofanya kazi katika maeneo rasmi kama wajenzi,” alisema.

Mtafiti Mwandamizi toka Chuo Kikuu cha Nairobi, Prof. Winnie Mitullah alisema juhudi za kuboresha sekta isiyo rasmi zinahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali na ushirikiano kati ya nchi na nchi ili kufanikiwa.

“Ni muhimu watafiti, maafisa wa serikali, wadau wa maendeleo, wafanyakazi sekta isiyo rasmi kukaa na kuja na suluhisho litakalokuwa endelevu kwa faida ya nchi zetu,” alisema

Mtafiti, Anne Kamau wa Chuo Kikuu Nairobi alisema swala la hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi bado ni changamoto kubwa nchini Kenya.

“Eneo hili linahitaji mjadala mpana utakaohusisha wadau wengi zaidi ili kuhakikisha sekta isiyo rasmi inafaidika na huduma za hifadhi ya jamii kwa kiasi kikubwa,” alisema Bi. Anne.

Akichangia, Bi. Rehema Hassan Chuma, Meneja, Kitengo kinachoshughulikia sekta isiyo rasmi, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) alipongeza juhudi za utafiti huo na kusema tayari shirika hilo linafanya kazi ya kuongeza wigo wa wanachama kupitia sekta isiyo rasmi tangu mwaka 2018.

“Tutaisaidia serikali kuhakikisha kuwa sera ya hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi inakamilika,” alisema. Aliseshauri kuwa umefika wakati sasa kwa makundi kama madereva bodaboda, daladala na wajenzi kujirasimisha katika vyama vitakavyotambulika na kufaidika na huduma kama hifadhi za jamii, na mikopo.

Bw. Gaston Kikuwi, Mwenyekiti wa chama mwamvuli wa vyama vya sekta isiyo rasmi Tanzania (VIBINDO) kilicho na vyama 741 na wanachama zaidi ya 68,000 nchini alisema mjadala wa huduma za hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi sekta isiyo rasmi ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi.

“Panatakiwa dhamira ya kweli katika kutekeleza mapendekezo ya utafiti huu kwa faida ya nchi yetu,” alisema Bw. Kikuwi.

Awali, akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Lughano Kusiluka; Dkt. Mary Rutenge alisema utafiti huo unaolenga kuboresha maisha ya wananchi katika nchi hizo mbili ni muhimu na kushauri mamlaka husika kufanyia kazi mapendekezo yake.

Kati ya matokeo mengine muhimu ya utafiti huo ni kuchapishwa kwa kitabu kuhusu hifadhi ya jamii na sekta isiyo rasmi Kusini mwa Jangwa la Sahara kikiangazia mifano halisi katika nchi za Tanzania na Kenya. Uzinduzi wa kitabu hicho ulifanyika katika warsha hiyo. Pia, utafiti huo umepelekea kupatikana kwa wanazuoni wawili ngazi ya uzamivu Tanzania na Kenya.

Jumla ya madereva daladala 250 na waendesha bodaboda 158 walihusishwa katika utafiti huo Tanzania, wakati wajenzo 212 walihusishwa. Kwa upande wa Kenya, wafanyakazi 200 katika sekta ya usafirishaji walihusishwa katika utafiti huo.Mtafiti na Mratibu Mwandamizi katika Utafiti wa “Sekta isiyo Rasmi na Hifadhi ya Jamii”, Dkt. Godbertha Kinyondo akinyanyua kitabu kuhusu sekta isiyo rasmi na hifadhi ya jamii Kusini mwa Jangwa la Sahara kuashiria kuzinduliwa kwake. Kitabu hicho kilizinduliwa wakati wa uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti huo kwa wadau mbalimbali jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Wengine ni watafiti, Bw. Aloyce Gervas wa Tanzania (wa pili kulia), Bi. Anne Kamau (kushoto) na Bi. Paschalin Basil (kulia) wa Kenya.
Mtafiti na Mratibu Mwandamizi katika Utafiti wa “Sekta isiyo Rasmi na Hifadhi ya Jamii”, Dkt. Godbertha Kinyondo akisisitiza jambo wakati wa uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti huo kwa wadau mbalimbali jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.


Wachangiaji mbalimbali kutoka sekta rasmi na isiyorasmi wakichangia maada.



























No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad