MUDATHIR, AGGREY WAREJESHWA KIKOSINI, SURE BOY ASHINDIKANA AZAM FC - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 21, 2021

MUDATHIR, AGGREY WAREJESHWA KIKOSINI, SURE BOY ASHINDIKANA AZAM FC

  Beki wa kati wa Azam FC, Aggrey Moris Ambros akiwa kwenye mazoezi ya timu hiyo inayojiandaa na mchezo wa raundi ya 10 ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting FC, mchezo utakaopigwa siku ya Alhamisi katika dimba la Azam Complex, Chamazi majira ya Saa 1:00 Usiku.

Kiungo wa Azam FC, Mudathir Yahya Abbas akiwa kwenye mazoezi ya timu hiyo inayojiandaa na mchezo wa raundi ya 10 ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting FC, mchezo utakaopigwa siku ya Alhamisi katika dimba la Azam Complex, Chamazi majira ya Saa 1:00 Usiku. Kushoto ni Beki wa pembeni, Pascal Msindo.

 
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
KLABU ya Azam imewarejesha kikosini Wachezaji wake wawili, Kiungo Mudathir Yahya Abbas na Beki Aggrey Moris baada ya taarifa kudai wamesamehewa, kwa kile kilichoelezwa kuwa walikuwa na mwenendo wa utovu wa nidhamu huku Salum Abuubakar (Sure Boy) akigoma kurejea kikosini hapo.

Kupitia mahojiano yake na Kituo cha Radio cha Clouds FM, Afisa Habari wa timu hiyo, Thabit Zacharia amesema Wachezaji hao wawili, Mudathir na Aggrey wamerejea kikosini na tayari wameanza mazoezi na wenzao kujiandaa na mchezo unaokuja dhidi ya Ruvu Shooting FC utakaopigwa siku ya Alhamisi kwenye dimba la Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam majira ya Saa 1:00 Usiku.

“Sure Boy hajaungana na wenzake, yeye ameonyesha nia kwa mdomo wake, baada ya kusema muda umefika kuondoka Azam FC, na anataka kuvunja mkataba. Kwa sasa anasubiriwa kuleta barua rasmi ili Viongozi wa Klabu wakae na Wanasheria, viangaliwe vipengele vya kuvunja mkataba, alafu Viongozi wetu wa juu, wataamua baada ya Wanasheria kutoa muongozo wao kisheria na ushauri wao”, ameeleza Thabit Zacharia.

Hata hivyo, tetesi zinaeleza kuwa Kiungo huyo, Sure Boy anawindwa na Wanajangwani Klabu ya Yanga katika dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 16, 2021 hadi Januari 15, 2022.

Azam FC iliwasimamisha Wachezaji hao watatu kwa muda usio na ukomo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu kwa Meneja wa timu hiyo, Wachezaji wenzao, Benchi la Ufundi na Viongozi wa Klabu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo, Septemba 18, 2021 siku ya mchezo wa pili wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Horseed FC ya Somalia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad